Geita. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ameamua kuingilia kati sakata lililokuwa likiendelea baina ya wachimbaji wadogo na mwekezaji katika mgodi wa Msasa, Kata ya Runzewe wilayani Bukombe.
Uamuzi huo umetolewa leo Februari 04, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, baada ya kumalizika kwa vikao vya kamati ya wilaya baina ya wachimbaji hao na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskas Mragili.
Katika sakata hilo, kamati iliyokuwa chini ya Mkuu wa Wilaya ya Bukombe ilibaini kuwa wachimbaji 273 waliingia makubaliano na mwekezaji Cosmas Bongo kugawana asilimia 50 kwa 50 katika kila uzalishaji utakaopatikana katika maduara 324 yaliyo ndani ya uzio.
Kundi lingine ni lile linalohusisha wachimbaji walioingia makubaliano ya kugawana asilimia 40 kwa 60 na mwekezaji kufanya uchimbaji katika eneo lake la umiliki wa leseni.
Baadhi ya wachimbaji waliohudhuria kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela.
Aidha, kundi lingine la wachimbaji 51 waliingia makubaliano na mwekezaji huyo kwa kusaini mkataba ambao mgawanyo wake upo katika mfumo wa hisa, ambapo hata hivyo kamati haikubainisha kiwango cha asilimia ya hisa hizo.
Itakumbukwa kuwa Januari 22, 2026 Jeshi la Polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya baadhi ya wachimbaji waliokuwa wakiandamana wakilalamikia Serikali kupandisha kodi na hivyo kupelekea mgawanyo kuwa 50 kwa 50.
Hata hivyo, mwekezaji Cosmas Bongo aliyetajwa kuwa chanzo cha mgogoro, alikanusha malalamiko hayo akiitaja sababu ya kusitisha uchimbaji kuwa ilitokana na mvua kubwa kunyesha, hivyo kusitisha shughuli hizo ili kulinda usalama wao.
Eneo la mgodi wa Msasa uliopo kata ya Runzewe wilayani Bukombe.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskas Mragili, aliyezungumza na Mwananchi kwa njia ya simu ambapo alibainisha kuwa sababu za kiusalama ndizo zilizosababisha uzalishaji kusitishwa baada ya maduara kujaa maji huku akikanusha madai ya asilimia 50 kuwa chanzo cha sakata hilo.
Akiwasilisha maamuzi ya kamati hiyo, Shigela ametoa uamuzi wenye maagizo matatu baina ya wachimbaji wadogo na mwekezaji.
Katika uamuzi wa kwanza, wachimbaji waliokuwa wamesaini mkataba wa kuchimba dhahabu katika maduara yaliyo ndani ya uzio kwa makubaliano ya mgawanyo wa asilimia 50 kwa 50, wataendelea kufuata sharti hilo huku mwekezaji akitakiwa kuchangia pia gharama za uzalishaji.
“Mkichimba mifuko 100, mnalipa kodi ya Serikali, mnalipa asilimia 10 kwa mwenye ardhi, asilimia 10 mnalipa wazalishaji, asilimia 20 inalipwa kwa mwenye leseni na kiasi kinachobaki mnagawana sawa.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela akizungumza katika kikao kilichowakutanisha wachimbaji wadogo na mwekezaji kuhusu mgogoro wa mgawanyo wa mgawanyo wa maslahi katika mgodi wa Msasa wilayani Bukombe.
“Hatutakuwa na utaratibu wa mtu kuchukua asilimia 50 bila kutoa jasho na kama kutakuwa na maboresho ni aidha mwekezaji au mwanachama achangie asilimia 50.”
Uamuzi wa pili unawahusu waliosaini mikataba na mwekezaji ya mgawanyo wa faida kwa asilimia 40 kwa 60 ambao pia wataendelea na makubaliano hayo huku mwekezaji akitakiwa kuchangia gharama za uzalishaji.
Uamuzi wa tatu unawahusu wachimbaji walio nje ya uzio ambao kutokana na shughuli zao kuhatarisha usalama wa barabara kuu iendayo nchi jirani, Shigela amewataka kusitisha uchimbaji na watakaohitaji kuendelea kuchimba kuwasiliana na Tanroads kwa kuwa ndiyo wenye mamlaka ya usimamizi wa barabara.
Aidha, Shigela amewataka wachimbaji ambao hawaridhishwi na uamuzi uliotolewa kufika ofisini kwake kupata ufafanuzi na endapo watakuwa hawajaridhishwa zaidi, wameshauriwa kufuata taratibu rasmi badala ya kutumia fujo.
“Kama kuna mtu hatoridhika na maamuzi haya, njia ya amani haizuiliki na ukiona umwone Waziri mwenye dhamana hauzuiliwi, lakini kutumia vurugu kushinikiza mgodi kufungwa hakukubaliki; hatuwezi kufunga maduara 1,293 kwa sababu ya watu wachache,” amesema Shigela.
Naye Cosmas Bongo, ambaye ni mwekezaji, amekiri kuridhishwa na uamuzi wa Serikali unaozingatia maslahi ya pande zote, huku akiahidi kuwa atasimamia uamuzi uliotolewa na Serikali.
“Duara zilizokuwa na mgogoro ni 324 tu, lakini mgodi wangu una duara zaidi ya 1,000 na waliokuwa wanasumbua ni watu kama 51 tu. Niwaombe wachimbaji waache kusikiliza watu wanaotaka kuiba mali za watu, wasitugombanishe,” amesema Bongo.
Baadhi ya wachimbaji walioshiriki kikao hicho akiwemo Yusuf Elikana na Godfrey Miti, wamesema kuwa wamekubaliana na uamuzi uliotolewa kuwa umewapa ahueni katika shughuli zao za uchimbaji.