Dar es Salaam. Huenda simu janja zikawa ghali zaidi mwaka 2026, baada ya kuongezeka kwa gharama za uzalishaji zinazochochewa na upungufu wa vipuri muhimu na ongezeko la mahitaji ya simu zenye uwezo mkubwa wa akili bandia (AI).
Wataalamu wa teknolojia wamesema uwezekano wa kuongezeka kwa bei hizo za simu janja utachochewa na gharama za vichakataji vya AI, mahitaji makubwa ya kumbukumbu na shinikizo endelevu la biashara ya kimataifa linaloendelea kuvuruga minyororo ya ugavi.
Kiini cha ongezeko hilo la bei, kwa mujibu wa wataalamu hao, ni kasi ya kuingizwa kwa vichakataji vya AI vinavyofanya kazi moja kwa moja ndani ya simu.
Wataalamu wanasema vichakataji hivyo vimeundwa kuendesha kazi ngumu za akili bandia moja kwa moja kwenye simu bila kutegemea muunganisho wa intaneti.
Kutokana na hilo, simu za kisasa zina uwezo wa kufanya tafsiri za lugha papo kwa papo, kuunda picha, kufanya uhariri wa hali ya juu wa picha, kutoa msaada wa sauti na kutabiri mahitaji ya mtumiaji, yote yakifanyika bila intaneti.
Ingawa uwezo huu ni hatua kubwa ya kiteknolojia, wataalamu wanasema unakuja na gharama kubwa.
Ripoti kadhaa za kampuni ya utafiti wa masoko ya teknolojia ya Counterpoint Research, ikiwemo Smartphone Shipment Forecasts Revised Down as Memory Shortage Drives BoM Costs Up, Memory Solutions for Gen AI na Smartphone Processor (SoC) Market, zinaeleza kuwa usafirishaji wa simu janja duniani umepunguzwa kutokana na gharama kubwa za kuzizalisha ikilinganishwa na matarajio ya awali.
Counterpoint inaeleza licha ya idadi ya vichakataji vya simu vinavyotarajiwa kusafirishwa mwaka 2026 kupungua, mapato yanayotokana na mauzo ya vichakataji hivyo yanaongezeka.
Hali hiyo inatokana na wazalishaji kuhamia zaidi kwenye matumizi ya vichakataji vyenye nguvu kubwa na gharama ya juu, hususan vile vinavyosaidia utekelezaji wa kazi za akili bandia.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, bei za kumbukumbu zinaweza kupanda hadi kufikia asilimia 40 kufikia robo ya pili ya mwaka 2026, jambo litakaloongeza gharama za uzalishaji wa simu kwa kati ya asilimia nane hadi zaidi ya asilimia 15 juu ya viwango ambavyo tayari ni vya juu.
Kutokana na hali hiyo, usafirishaji wa simu janja duniani kote unatarajiwa kupungua kwa takribani asilimia 2.1 mwaka 2026, huku bei kubwa zikianza kupunguza uwezo wa watumiaji kununua simu mpya.
Wakati huohuo, kasi ya kuingizwa kwa teknolojia ya akili bandia inasukuma juu wastani wa bei ya simu sokoni, hata kama mauzo kwa idadi yanapungua.
Mwelekeo huu pia unatarajiwa kuongeza ukuaji wa soko la simu zilizotumika au zilizorekebishwa, kwani watumiaji wengi wanachagua kuendelea kutumia simu walizonazo au kununua simu zilizotumika badala ya kuboresha kwenda kwenye simu mpya.
Akizungumza na The Citizen, mchambuzi wa teknolojia, Dominic Dismas, amesema simu za kisasa sasa zinafanya mambo mengi zaidi ya mawasiliano ya kawaida.
“Kamera za hali ya juu, skrini zenye ubora mkubwa, chaji ya haraka, mifumo imara ya usalama na kazi za akili bandia zimekuwa viwango vipya,” amesema.
Amesema uwezo na kasi ya kumbukumbu ni mambo muhimu zaidi kwa sasa, kwani ndiyo huamua ulaini wa mfumo wa simu na uwezo wake wa kuendesha programu nyingi kwa wakati mmoja.
“Akili bandia ni moja ya sababu kuu zinazofanya simu kuwa ghali zaidi mwaka 2026,” amesema, akieleza kuwa tofauti na teknolojia za awali, Gen AI haiwezi kuongezwa tu kupitia masasisho ya programu.
“AI inayotumia mtandao ni nafuu zaidi kwa sababu kazi nzito hufanywa na seva, lakini Gen AI inayofanya kazi bila intaneti inalazimisha simu yenyewe kubeba mzigo wote wa uchakataji, na hilo linahitaji maboresho ya gharama kubwa ndani ya simu,” amefafanua.
Kwa upande wa wauzaji wa rejareja, athari zake zinaanza kuonekana tayari.
Muuzaji wa simu mtandaoni, Bruno Almas, amesema ongezeko la bei linaanza kujitokeza hata kwa simu mpya zilizoingia sokoni hivi karibuni.
“Tatizo hili limeanza kuonekana mapema, hata kwa simu ambazo tayari zipo sokoni,” amesema, akitaja kuongezeka kwa bei za Samsung S25 Ultra, iPhone 17 Pro Max, OnePlus 13 na Xiaomi 17 Pro Max.
Amesema mabadiliko ya thamani ya fedha na kupanda kwa bei za jumla ndizo zinazoendesha mwenendo huo.
“Baadhi ya mabadiliko haya yanahusiana na kuimarika kwa sarafu ya Dirham na kupanda kwa bei katika masoko ya jumla ya simu,” amesema.
Amesema taarifa zinazosambaa ndani ya sekta zinaonyesha gharama za RAM kupanda kwa kasi, hali inayosababisha hata bei za simu zilizopo sokoni kuongezeka.
“Tunasikia kuwa ongezeko la gharama za RAM ni changamoto kubwa, kiasi cha kusababisha hata simu zilizopo sokoni kupandisha bei,” amesema.
Muuzaji mwingine wa simu eneo la Makumbusho, Jumanne Rashid, amesema hali hiyo inaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa tabia za wanunuzi.
“Kuna uwezekano mkubwa watu wengi kuhamia kwenye simu zilizotumika,” amesema, akisisitiza kuwa ikiwa bei zitaendelea kupanda, mahitaji ya simu mpya yatashuka huku matumizi ya simu zilizotumika yakiongezeka.
Amewashauri watumiaji wasiharakishe kubadilisha simu zao bila sababu ya msingi.
“Wakati mwingine si lazima kubadilisha simu. Kama simu uliyonayo bado inakidhi mahitaji yako, ni bora uendelee kuitumia,” amesema.
Kwa wafanyabiashara wa jumla, hali si nafuu pia. Fatima Abdullatif, mfanyabiashara wa jumla wa simu, amesema ongezeko la bei linalotarajiwa linawaletea changamoto wauzaji na wateja.
“Kama wauzaji, tayari tunaona gharama za kuagiza simu kutoka nje zikiongezeka, hasa zile zenye kumbukumbu kubwa na uwezo wa AI,” amesema.
Amesema wafanyabiashara wengi sasa wanalazimika kufikiria upya mikakati yao ya biashara.
“Tunaweza kulazimika kuelekeza nguvu zaidi kwenye simu zilizotumika kuliko mpya, kwa sababu huko ndiko mahitaji yanapoelekea,” amesema.
Ongezeko la bei halitarajiwi kuathiri simu za bei ya juu pekee; hata simu za kati na za bei nafuu zinatarajiwa kuwa ghali zaidi mwaka 2026, huku wazalishaji wakikabiliwa na gharama kubwa za vipuri.
Kampuni ya teknolojia ya Nothing tayari imetoa ishara kuwa simu zake zitakuwa ghali zaidi mwaka ujao kutokana na kupanda kwa gharama za kumbukumbu kunakoikumba sekta nzima.
Katika chapisho lililowekwa kwenye LinkedIn, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Carl Pei, amesema shinikizo la gharama za kumbukumbu linafikia hatua ambayo wazalishaji wanashindwa kuhimili.
Kadiri watengenezaji wa simu wanavyoendelea kusukuma teknolojia za juu za akili bandia kwenye vifaa vyao, wachambuzi wanaonya kuwa bei kubwa huenda ikawa hali ya kawaida, jambo litakalobadili namna watumiaji wanavyonunua, kuuza na kutumia simu janja katika miaka ijayo.
