Uvuvi unategemewa kwa kiasi kikubwa katika maisha ya watu wa Zanzibar wanaoishi kandokando ya bahari.
Hata hivyo, uvuvi unapofanyika bila kuzingatia usalama na uhifadhi wa mazingira, huchangia kwa kiasi kikubwa kuangamizwa kwa rasilimali za baharini, yakiwemo matumbawe.
Kwa sasa, nchi nyingi zikiwamo zile zinazotegemea Bahari ya Hindi, zinakabiliwa na upungufu wa samaki na viumbe mbalimbali wa bahari kufuatia uharibifu wa matumbawe na miamba uliosababishwa na uvuvi haramu pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali za bahari.
Kutokana na ongezeko la uharibifu wa bahari, licha ya kuchukuliwa hatua mbalimbali za hifadhi ya bahari na kuwekwa kwa sheria za kulinda maeneo ya mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inazipitia upya sheria za hifadhi ya bahari, yakiwemo matumbawe na miamba.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Kikosi cha Kulinda Biashara ya Magendo na Kupambana na Uvuvi Haramu, Hassan Msingiri, Sheria ya Uvuvi ya Mwaka 2010 inafanyiwa mapitio ili kuandaliwa sheria itakayokidhi mahitaji ya sasa katika kulinda miamba na matumbawe.
Kazi hiyo inafanyika kwa kushirikiana na wataalamu wa masuala mbalimbali ya bahari pamoja na washirika wa ndani na nje ya Zanzibar.
Katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar zipo fukwe safi zenye mchanga mweupe zilizozungukwa na matumbawe, ambayo ndiyo chanzo kikuu cha uzalishaji wa samaki na viumbe wengine wa baharini katika bahari inayozunguka visiwa vya Unguja na Pemba. Hali hiyo imeifanya Zanzibar kufahamika pia kama Visiwa vya Matumbawe, ambapo matumbawe yaliyotunzwa vizuri husaidia ukuaji wa viumbe hai majini kwani ni sehemu asilia ya mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini.
Matumbawe yanapotunzwa ipasavyo, wananchi hupata samaki kwa wingi, shughuli za utalii hushamiri katika maeneo husika na kuchangia kukuza uchumi wa bahari (uchumi wa buluu), huku wavuvi wakipata kipato kizuri cha kujikimu kimaisha.
Katika mkutano wa hifadhi ya mazingira uliofanyika Zanzibar hivi karibuni, wataalamu walionya kuwa mabadiliko ya tabianchi, uvuvi usio endelevu pamoja na shughuli za utalii zisizopangwa vizuri vinaendelea kuathiri miamba ya matumbawe.
Katika miaka ya karibuni, kumefanyika juhudi kubwa za kuanzisha miradi ya kukarabati miamba katika baadhi ya maeneo, ikiwemo Mnemba na Fumba.
Miradi hiyo pia imelenga kushughulikia changamoto zinazokabili miamba ya matumbawe, zikiwemo shughuli zisizo endelevu za binadamu kama uvuvi haramu unaotumia baruti, nyavu zenye matundu madogo na mikuki.
Uharibifu wa miamba na matumbawe pia umekuwa na athari kubwa kwa maji ya bahari kusogea ufukweni, hali inayosababisha uharibifu wa nyumba zilizopo kandokando ya bahari pamoja na mashamba ya mpunga na mboga mboga.
Kwa miaka mingi kelele zimekuwa zikipigwa juu ya kuharibika kwa matumbawe, lakini juhudi zinazofanyika kudhibiti hali hiyo zinaonekana bado hazitoshi. Ni vyema katika mapitio ya sheria kukatafutwa mbinu bora zaidi za kukabiliana na changamoto hiyo.
Kwa sasa inaonekana kuwa sheria zilizopo ni dhaifu na usimamizi wa kuwabana waharibifu wa matumbawe ni mdogo.
Kwa mfano, ni rahisi kutambua samaki waliovuliwa kwa mabomu kwa kuwa huwa na dalili na harufu ya moshi, lakini ni mara chache mvuvi anayewapeleka samaki hao sokoni kuchukuliwa hatua za kisheria.
Zanzibar inapaswa kujifunza kutokana na hasara kubwa zilizopatikana katika nchi mbalimbali zilizoathiriwa na uvuvi haramu uliosababisha uharibifu wa matumbawe na mazingira ya bahari.
Kwa sasa, wavuvi katika nchi hizo wanapata samaki kwa kiasi kidogo na hali zao za maisha zinazidi kuwa duni.
Pamoja na kuwa ni mazalia ya samaki tunaowategemea kwa chakula, matumbawe pia ni kivutio kikubwa cha watalii, ambao kwa sasa wanachangia zaidi ya asilimia 25 ya pato la Zanzibar.
Hata hivyo, iwapo kasi ya uharibifu wa matumbawe haitadhibitiwa, Zanzibar itajikuta ikiwa na bahari isiyo na samaki, huku eneo lake dogo la ardhi likizidi kuliwa na bahari.
Hii ni hatari ambayo Serikali na wananchi wa Zanzibar wanapaswa kuishughulikia kwa haraka. Vinginevyo, vizazi vijavyo vitawalaumu waliotangulia kwa kushindwa kuwarithisha bahari salama, yenye rasilimali na iliyojaa samaki waliyoachiwa na wazee wao.
Miongoni mwa hatua muhimu zinazopaswa kwenda sambamba na mapitio ya Sheria ya Uvuvi ni kuongeza uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa kuachana na uvuvi haramu. Ni vyema suala hili likapewa kipaumbele kwa kuwaelimisha wavuvi na wanafunzi, hususan wale wanaoishi katika maeneo ya karibu na bahari.
