Ujenzi wa Stendi ya Mabasi Bondeni City Watajwa Kuibua Fursa Mpya za Kiuchumi Arusha

Na Pamela Mollel Arusha,

Mradi wa ujenzi wa Stendi ya Mabasi Bondeni City unaendelea kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuboresha huduma za usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Jiji la Arusha, baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Mhe. Paul Christian Makonda, kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza katika eneo la ujenzi wa stendi hiyo, Mhe. Makonda amepongeza uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa utendaji kazi mzuri na usimamizi thabiti wa miradi ya maendeleo, akibainisha kuwa kasi ya ujenzi inaakisi dhamira ya serikali katika kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.

Pia, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa haraka na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa, ili stendi hiyo iweze kutoa huduma bora, salama na za kisasa kwa wananchi pamoja na wageni wa Jiji la Arusha.

Aidha, Waziri Makonda ameuagiza uongozi wa mkoa kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa mipango miji ili kunufaika na fursa zitakazotokana na mradi huo, ikiwemo ujenzi wa maeneo ya biashara na shughuli za kiuchumi zitakazosaidia kuongeza ajira na kukuza uchumi wa jiji.

Ziara ya Waziri Makonda ilihusisha miradi ifwatayo ukaguzi  ujenzi wa Stendi ya Mabasi Bondeni City, ujenzi wa Barabara ya ESO, mradi wa Soko la Kilombero, pamoja na mradi wa ujenzi wa jengo jipya la Halmashauri ya Jiji la Arusha unaotekelezwa kwa mapato ya ndani.