Moshi. Ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya jinai ya makosa ya kimtandao inayomkabili Mchungaji Godfrey Malisa, unatarajiwa kuanza kutolewa Februari 11, 2026.
Leo Jumatano Februari 4, 2026 mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Ally Mkama wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wawili kuanza ushahidi wao ila ilishindikana kutokana na mshtakiwa huyo kupewa nyaraka zinazohusu kesi ikiwemo maelezo ya mashahidi wa Jamhuri na kuomba muda ili akazipitie nyaraka hizo na wakili wake.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 28411 ya 2025, Malisa anatuhumiwa kuchapisha taarifa kwenye mtandao wake wa YouTube, akimdai Rais Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu kwa kusimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.
Upande wa Jamhuri umewakilishwa na mawakili wawili ambao ni Ramadhani Kajembe na Frank Daud, ambao waliieleza Mahakama kuwa shauri limepangwa kwa ajili ya usikilizwaji na wako tayari kuendelea na kesi.
Hakimu Mkama amemuuliza Malisa iwapo yuko tayari kuendelea na shauri hilo, amejibu hayuko tayari kwa sababu amepewa nyaraka zinazohusu kesi hiyo leo asubuhi hajazisoma na wakili wake alikuwa njiani na angetarajiwa kufika Moshi saa saba mchana.
Upande wa Jamhuri ulieleza Mahakama kuwa ni kweli wamempa mshtakiwa huyo maelezo ya mashahidi na vielelezo leo asubuhi na kuwa suala la kuahirishwa kwa kesi hadi saa saba mchana wanaiachia Mahakama iwapo itakubali kusubiri au kama itatoa mwongozo mwingine.
Hakimu alimuuliza mshtakiwa huyo iwapo wakili wake anafika kwa ajili ya kuendelea na kesi au la ambapo Malisa alimweleza kuwa wakili wake anakuja ili washauriane na kuomba muda wa wiki moja ili waweze kuzipitia nyaraka hizo ambazo zilikuwa na kurasa 82.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Mkama alikubaliana na ombi la Malisa na kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 11, 2026 itakapoanza kusikilizwa.
“Nitakubali ahirisho lako kwa muktadha umepewa nyaraka asubuhi na idadi yake 82 tukisema tuahirishe kwa saa moja tutakuwa hatukutendei haki na baada ya wiki moja naomba tusiwe na sababu nyingine ya kuahirisha na baada ya kusomwa maelezo ya awali (PH) kesi ilipaswa kuanza kusikilizwa,” amesema.
Aidha, Hakimu huyo kabla hajaahirisha shauri hilo aliwaita mashahidi hao wawili waliotarajiwa kutoa ushahidi wao leo, ambao ni maofisa wa Jeshi la Polisi na kuwaonya kufika mahakamani hapo Februari 11, 2026.
“Mahakama iliwaita leo kupitia wito maalum kutoa ushahidi ila ni matakwa ya kisheria baada ya mshtakiwa kushtakiwa mahakamani nyaraka zote Jamhuri zinazokusudia kutumia kwenye shauri anapaswa apewe, bahati mbaya tangu shauri lifunguliwe leo mshtakiwa ndiyo amepewa nyaraka,” amesema na kuongeza;
“Kwa sababu Mahakama imefahamishwa kuwa nyaraka ziko kurasa 82 basi tumeona ili kuwe na kesi inayozingatia matakwa ya kisheria tumpe muda wa kutosha kuzipitia ili kuwa na nafasi ya kuwahoji mashahidi watakaotoa ushahidi, Mahakama inawaonya kufika bila kukosa Februari 11, 2026.”
Katika kosa la kwanza, upande wa mashitaka unadai kuwa Mchungaji Malisa alitenda kosa hilo Novemba 15, 2025 huko Miembeni katika wilaya ya Moshi na alichapisha maneno hayo katika akaunti ya YouTube yenye jina Godfrey Malisa.
Hati ya mashitaka iliyofunguliwa Novemba 3, 2025 inanukuu maneno aliyoyachapisha kuwa alisema: “Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu mara moja kwa kuwa amekuwa ni Rais aliyesimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.”
Upande wa Jamhuri unadai alichapisha maneno hayo akijua fika kuwa taarifa hizo hazikuwa sahihi na zilikuwa na lengo la kupotosha umma wa Watanzania.
Katika kosa la pili, anatuhumiwa kufanya uchochezi kinyume na kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Maelezo ya kosa ni kuwa Novemba 15, 2025 huko Miembeni wilaya ya Moshi, anadaiwa kuchochea umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutenda kosa la jinai ambalo ni kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria.
Mbali na kesi hiyo, Mchungaji Malisa anakabiliwa na kesi ya uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2023, akituhumiwa kuhamasisha mkusanyiko usio halali hapa Tanzania.
Kulingana na hati ya mashitaka, inadaiwa kuwa Novemba 16, 2025 huko eneo la Miembeni katika wilaya ya Moshi, akiwa na utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na akiwa ndani ya ardhi ya Tanzania, alitenda kosa hilo la uhaini.
Inadaiwa alitengeneza nia ya kuhamasisha umma kushiriki katika mkusanyiko usio halali kwa lengo la kumtisha mtendaji wa Serikali ya Tanzania na alidhihirisha nia hiyo kwa kitendo chake cha kutamka na kuchapisha maneno yafuatayo;
“Samia Suluhu Hassan… Kabla ya kufika tarehe 9 Desemba uwe umekwisha jiuzulu… Kama utang’ang’ania madaraka itakapofika tarehe 9 Desemba kutakuwa na maandamano ambayo hayajawahi kutokea katika bara la Afrika.”
Mchungaji Malisa anadaiwa kunukuliwa akisema “Lengo la maandamano ni kumuondoa Samia Suluhu Hassan madarakani na maandamano hayo yatakuwa ni maandamano ya muendelezo mpaka utakapotoka madarakani.”
Mshtakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa kosa hilo linaloangukia kifungu hicho cha 39(2)(d) ni kosa la uhaini kwa mujibu wa kifungu hicho.
Kifungu hicho kinasema mtu yeyote mwenye utii kwa Tanzania, endapo anaitisha Serikali na kubainisha nia hiyo kwa kuchapisha maandishi au machapisho au kwa kitendo chochote cha siri kinachojionyesha cha hali yoyote, atakuwa na hatia ya kosa na endapo atatiwa hatiani atawajibika kwa adhabu ya kifo.
Mchungaji Malisa alijitokeza kwenye siasa kwa mara ya kwanza mwaka 2010 alipogombea ubunge Moshi Mjini kupitia chama cha Tanzania Labour Party (TLP) na mwaka 2015 aligombea urais kupitia CCK na baadaye kugombea uspika.
Mwaka 2018 aligombea ubunge Kinondoni kwa chama cha TLP na mwaka 2020 aligombea ubunge jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya chama cha NCCR Mageuzi na baada ya uchaguzi ule alijiunga na CCM hadi mwaka 2025 alipotimuliwa.
Mwaka 2022 Malisa alijitosa kuchukua fomu na kuwa miongoni mwa makada tisa waliochukua fomu kugombea uenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Hata hivyo, Februari 10, 2025 Mchungaji Malisa ambaye ni mwanazuoni mwenye shahada ya Uzamivu (PhD), alifukuzwa uanachama wa CCM baada ya kupinga maamuzi ya Mkutano Mkuu wa CCM uliomteua Rais Samia kuwa mgombea urais.
Maamuzi ya kumfukuza uanachama yalitangazwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Merce Mollel, akiegemea maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro iliyomuondolea sifa ya kuendelea kuwa mwanachama.
“Malisa amefukuzwa kutokana na kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama kwa sababu mara kwa mara amekuwa akibeza maamuzi halali yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliofanyika Januari 19, 2025,” alieleza Mollel.
Katibu huyo alinukuliwa akidai Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na nchi kutokana na kudai mkutano huo uliomteua Samia kuwa mgombea pekee ulivunja Katiba jambo ambalo si la kweli.
Pamoja na kufukuzwa uanachama, bado aliendelea kupinga uteuzi huo kwa kujaribu kufungua kesi mahakamani ambazo hata hivyo hakufanikiwa, ambapo alihamia katika mitandao ya kijamii akiendelea kupinga uteuzi huo.
