Wabunge walia mpango kuwa na sheria za zamani, Tarimba ataka Dar ije kivingine

Dodoma. Mapendekezo ya Mpango wa Serikali ndani ya Bunge yameendelea kuibua hisia tofauti miongoni mwa wachangiaji lakini wengi wakitaka mpango uguse maisha ya wananchi moja kwa moja.

Maeneo ambayo yameguswa zaidi ni ardhi, maji, sheria za majiji, nishati na mwelekeo wa uchumi wa dola 1 trilioni ifikapo 2050.

Hata hivyo, Mbunge wa Kinondoni (CCM), Tarimba Abbas amesisitiza Jiji la Dar es Salaam lazima litungiwe sheria mpya kwa ajili ya uendeshaji wake kwani linapoendeshwa kwa Sheria za zamani maisha ya watu yanazidi kudidimia.

Leo Jumatano, Februari 4, 2026, akichangia mpango huo, Tarimba amesema maendeleo ya kweli hayapimwi kwa takwimu pekee bali kwa namna yanavyogusa maisha ya mtu mmoja mmoja katika jamii.

Tarimba amesema urasimishaji wa ardhi, hususan katika maeneo ambayo hayajapimwa ndani ya Dar es Salaam, akieleza kuwa hali hiyo imekuwa chanzo cha maumivu kwa wananchi kwa muda mrefu.

Mbunge huyo anasema kukosekana kwa urasimishaji kumeathiri usalama wa umiliki wa ardhi, mikopo, na mipango ya maendeleo ya makazi.

“Asilimia 70 ya wakazi wa Dar es Salaam wanaishi kwenye makazi yasiyo rasmi, hali si ya kuridhisha kwa jiji linalokuwa kwa kasi kubwa, Serikali ihakikishe Mpango mpya unatoa majibu hayo akipendekeza mfano wa yote lazima uanzie Kinondoni,” amesema Tarimba.

Amesisitiza ili Dar es salaam iwe eneo la kiuchumi la kikanda na kimataifa, Serikali inapaswa kufanya mapitio ya kina ya sheria za zamani, kufanya utafiti wa mifumo ya uendeshaji wa majiji makubwa duniani na kuja na sheria za kisasa zinazoendana na kasi ya ukuaji, uwekezaji, biashara na fursa za ajira.

“Dar es Salaam ni jiji la biashara na mhimili wa uchumi wa Taifa, lakini sheria na kanuni za uendeshaji wa serikali za mitaa bado zinaididimiza badala ya kulifungua jiji hilo kiuchumi, huu Mpango utusaidie kufungua fursa kwa wananchi,” amesema.

Amesema Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji yanayokua kwa kasi duniani, lakini bado inatawaliwa kwa sheria zilezile zinazotumika Sumbawanga, Tanga na miji mengine, hali inayopuuza upekee wake.

Katika sekta ya maji, Tarimba amesema ni jambo lisilokubalika kuwa miaka 61 baada ya Uhuru bado wakazi wake wanalia na hawana uhakika wa maji ya kutosha.

Kwa mujibu wa mwakilishi huyo, Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ina wakazi zaidi ya  milioni sita, hivyo suala la maji halipaswi kuchukuliwa kwa uzembe au kwa mtazamo wa kawaida, bali kama agenda ya kimkakati ya kiusalama na uchumi.

Kuhusu changamoto ya mikopo kwa wananchi, amesema bado kuna kusuasua licha ya agizo la Waziri Mkuu, hivyo akaomba serikali iweke utaratibu maalum wa kulegeza masharti ya mikopo ili kusaidia wananchi na watumishi kunufaika kikamilifu.

Ameeleza upekee wa Dar es Salaam unatokana na bandari, biashara ya kimataifa, idadi ya watu, miundombinu, sekta ya fedha na huduma, hivyo unahitaji mfumo maalum wa kisheria na kiutawala.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Mjini (CCM), Esther Matiko amesisitiza umuhimu wa Serikali kuwekeza zaidi katika sekta ya utalii wa kihistoria, akitaja makazi ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Matiko amesema makazi hayo yanapaswa kuboreshwa na kuendelezwa kwa kiwango cha Kimataifa, kama ilivyofanywa kwa makazi ya Hayati Nelson Mandela nchini Afrika Kusini.

“Mwalimu Nyerere ni kiongozi anayeheshimika Kimataifa, hivyo kuboresha eneo hilo kutaiweka Tanzania katika ramani ya utalii wa kihistoria na kielimu, sambamba na kuongeza mapato ya Taifa kupitia wageni wa ndani na nje ya nchi,” amesema Matiko.

Mbunge huyo amesisitiza uwekezaji huo hautakuwa wa kihistoria pekee bali kichocheo cha ajira, biashara ndogondogo na ukuaji wa uchumi wa maeneo yanayozunguka makazi hayo.

Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo akichangia kwa mtazamo wa kitaalamu wa uchumi na rasilimali, amesema maono ya serikali ya kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo 2050 yanawezekana endapo kutakuwa na mabadiliko makubwa ya kimkakati.

Hata hivyo, Profesa Muhongo amesema makisio ya kukua kwa uchumi yanahitaji uchumi kukua kwa wastani wa asilimia 10, au angalau asilimia 8, tofauti na hali ya sasa ya asilimia 6.

Waziri huyo wa zamani wa Nishati na Madini amesema ukuaji wa sasa wa asilimia 6 hadi 6.5. kwa zaidi ya miaka 20 ni kiwango ambacho hakitoshi kwa Taifa linalolenga kutoka kwenye kundi la nchi zinazoendelea.