Dar es Salaam. Tanzania imeendelea kushuhudia ongezeko la wanafunzi wanaodahiliwa katika mtalaa wa amali kila mwaka licha ya ufaulu wao kushuka katika baadhi ya masomo.
Matokeo yaliyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) yanaonesha kuwapo kwa ongezeko la wanafunzi waliofanya mtihani katika masomo ya mtalaa mpya huku wale wanaopata wastani wa daraja A hadi D wakipungua.
Mwananchi imefanya uchambuzi wa baadhi ya masomo hayo umebaini ongezeko la wadahiliwa licha ya kuhitajika nguvu ya ziada ili kuhakikisha ufaulu haushuki zaidi.
Kutokana na hilo, Serikali imeweka bayana itaendelea kusimamia ubora wa ufundishaji ili utoaji elimu hiyo uwe na ufanisi na lengo lililowekwa linatimia.
Somo la ujenzi watahiniwa waliongezeka hadi kufikia 521 mwaka 2025 kutoka 398 mwaka jana huku waliopata wastani wa A hadi D wakishuka hadi asilimia 93.09 kutoka asilimia 98.24.
‘Architectural draughting’ watahiniwa walifikia 485 ikiwa ni ongezeko kutoka 390 mwaka juzi huku waliopata daraja A hadi D wakiwa asilimia 93.61 kutoka asilimia 97.95 mwaka juzi.
‘Wood work and painting engineering’ watahiniwa waliongezeka kutoka 131 mwaka juzi hadi 164 mwaka jana huku waliopata daraja A hadi D wakifikia asilimia 87.2 kutoka asilimia 96.18 mwaka juzi.
‘Electronics and communications engineering’ watahiniwa waliongezeka hadi 295 kutoka 275 katika watahiniwa waliokuwapo mwaka juzi huku waliopata wastani wa A hadi D wakifikia asilimia 90.51 kutoka asilimia 92 mwaka juzi.
‘Electronic draughting’ waliofanya mtihani mwaka jana walikuwa 258 ikiwa ni ongezeko kutoka wanafunzi 234 wakati waliopata wastani wa A hadi D walishuka hadi asilimia 92.25 kutoa asilimia 94.87 mwaka juzi.
‘Automotive engineering’ katika mwaka 2025 ilikuwa na watahiniwa 191 ongezeko kutoka watahiniwa 169 mwaka juzi wakati waliopata daraja A hadi D wakishuka kutoka asilimia 100 hadi asilimia 92.67.
Katika mwaka 2024, somo la ‘Fine art’ lilikuwa na watahiniwa 1,793 walioongezeka hadi kufikia 2,712 mwaka 2025 wakati waliopata wastani wa daraja A hadi D walishuka kutoka asilimia 97.88 hadi asilimia 84 mwaka jana.
Alichokisema Profesa Nombo
Akizungumzia ongezeko la wanafunzi hawa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo amesema linatokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika kuboresha na kutanua wigo wa ufundishaji masomo ya amali.
Amesema Serikali imeendelea kujenga shule mpya za mchepuo wa amali ili kuhakikisha kunakuwa na miundombinu mizuri ya kujifunzia na kufundishia jambo linalokwenda sambamba na kuajiri walimu na kutoa mafunzo kwa waliopo kazini.
“Tulipoanza tulifundisha walimu ili wawe mahiri na tunaendelea kujifunza ili waweze kuwafanya watoto wajifunze kupitia mtalaa huu wa amali kama inavyotakiwa,” amesema.
Amesema hilo linafanyika kwa sababu inaonekana njia inayoweza kuwafanya watoto kujiajiri baada ya kumaliza masomo kupitia ujuzi walioupata shuleni badala ya kusubiri kuajiriwa.
“Tunahakikisha tunaboresha mazingira ya shule zilizojengwa na ndani yake tumeingiza teknolojia kama moja ya namna ya kufundishia,” amesema.
Amesema uwekezaji uliofanyika ulifanya masomo ya amali kupata ufaulu wa juu zaidi katika mitihani ya kidato cha pili kuliko ule mtalaa wa jumla huku akiweka bayana kuwa kwa matokeo hayo, Serikali haitakuwa tayari kuona ubora wa elimu wa mtalaa huo unarudi nyuma.
“Itakuwa ni bahati mbaya lakini ubora utazingatiwa hata kama hatutaongeza shule zile zilizopo tutahakikisha tunasimamia ubora unaotakiwa,” amesema Profesa Nombo.
Akizungumzia kupungua kwa ufaulu katika baadhi ya masomo ya mtalaa wa amali kwa mujibu wa matokeo ya Necta, Profesa Nombo ameomba kwenda kufanya uchambuzi wa takwimu ili kujua tatizo lilipo.
“Siamini kama kuna ushukaji katika ufaulu, labda somo kwa somo lakini kwa jumla kumeimarika sana. Nahitaji muda nipate data nione nijue, nashindwa kuzungumza katika hili moja kwa moja kwa sababu sina takwimu za mwaka jana na mwaka huu za kila somo,” amesema.
Katibu mkuu anaeleza hayo wakati ambao Serikali imewezesha ujenzi wa shule mpya 103 za sekondari za amali ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Kati ya shule hizo, shule 29 ni za amali za kihandisi na shule 74 ni za amali zisizo za kihandisi. Kukamilika kwa shule hizo kutawezesha kuongezeka kwa idadi ya shule za amali za sekondari kutoka shule tisa hadi shule 112 za sekondari za amali.
Pia, bajeti hiyo imeweka bayana kuwa ili kuimarisha utoaji wa elimu ya amali katika shule za sekondari nchini, Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania itawezesha upanuzi wa shule 55 za sekondari kuwa sekondari za amali.
Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu wa fani ya umeme, Ismail Mohammed amesema kuongezeka kwa wanafunzi kusoma masomo hayo kunatokana na hamasa kubwa iliyotolewa kuhusu masomo ya amali na ufundi katika miaka ya hivi karibuni.
Mohammed amesema hiyo inatokana na uwepo wa changamoto ya ajira hasa kwa vijana inayosababisha vijana kugeukia masomo ya ufundi ili waweze kujiajiri na hata kutengeneza fursa ya ajira kwa wengine.
“Ile dhana ya nisome ili niajiriwe inaendelea kupungua kwa vijana, wengi wao wanatafuta ujuzi ambao utawasaidia wao kujiajiri na kutengeneza kipato,” amesema.
Mtaalamu wa Ramani za Majengo, Selua Barabara amesema ongezeko hilo la wanafunzi pia limechangiwa na hamasa kutoka kwa watu waliofanikiwa kupitia ujuzi unaopatikana katika maeneo hayo.
Amesema baada ya kuibuka kwa mjadala katika majukwaa mbalimbali kuhusu changamoto ya ajira wapo watu kadhaa ambao baadhi yao ni maarufu walijitokeza na kueleza ni kwa namna gani wameweza kufanikiwa kiuchumi kupitia elimu ya ufundi.
“Itakuwa imechangia wanafunzi na hata wazazi kuangalia masomo hayo kwa jicho la pili na kuanza kujijengea msingi tangu wakiwa katika ngazi ya sekondari,” amesema.
Kwa upande wa teknolojia na mawasiliano, mtaalamu katika eneo hilo, Andrea Peter amesema hilo linaonesha namna ambavyo wanafunzi, wazazi, jamii na Serikali wanakwenda sambamba na dunia inavyokwenda.
Peter amesema kwa sasa mambo mengi duniani yanaendeshwa na kufanyika kwa kutumia teknolojia, hivyo elimu ya teknolojia na matumizi yake hayaepukiki katika maisha ya kila siku.
“Kimsingi ni jambo la kufurahisha kuona vijana wako tayari kuendana na uhalisia wa dunia ya sasa,” amesema.
Hata hivyo, ametoa ushauri kwa Serikali kuhakikisha wanatengeneza mazingira wezeshi na rafiki kwa wanafunzi wengi zaidi kuvutiwa na masomo hayo ya teknolojia na ufundi na kufaulu vizuri.
Amesema hilo litawezekana kama wataendelea kuhakikisha kunakuwepo na walimu wa kutosha, vitabu na vifaa vya kujifunzia kwa vitendo.
“Masomo yanayohusisha teknolojia na ufundi yanatakiwa kufundishwa kwa vitendo zaidi kuliko nadharia, hivyo ni muhimu mwanafunzi kutengenezewa mazingira wezeshi ya kujifunza kwa vitendo,” amesema.
Akizungumzia kuhusu ufaulu wa masomo hayo mdau wa elimu, Catherine Sekwao amesema uwekezaji zaidi unahitajika ili ufaulu katika masomo hayo kuongezeka.
Amesema kwa kuwa masomo hayo ni mapya ni muhimu Serikali kuendelea kuwekeza katika kupata walimu wenye stadi za kutosha, vitabu na hata zana za kufundishia kwa vitendo.
“Kama Serikali itafanyia kazi maeneo hayo kwa ukamilifu katika masomo yote ya amali naamini itasaidia kuongeza ufaulu,” amesema.
