Wananchi walilia kituo cha Polisi cha kisasa

Geita. Wananchi wa Kata ya Mgusu, Wilaya ya Geita, wameiomba Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kusaidia ujenzi wa kituo cha Polisi cha kisasa katika kata hiyo.

Wanasema kwa sasa askari wanaofanya kazi katika eneo hilo wanategemea jengo la Ofisa Mtendaji wa Kata kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.

Ombi hilo limetolewa leo Jumatano, Februari 4, 2026 na Diwani wa Kata ya Mgusu, Yohana Buhabi, kwa niaba ya wananchi wakati wa hafla ya ufunguzi wa nyumba pacha za makazi ya askari Polisi zilizojengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML).

Akizungumza katika hafla hiyo, Buhabi amesema kukamilika kwa nyumba hizo kumeondoa changamoto ya makazi kwa askari na sasa kipaumbele kinapaswa kuelekezwa kwenye ujenzi wa kituo cha Polisi ambacho tayari kimetengewa eneo.

“Baada ya kukamilika kwa nyumba hizi, tunaomba kupatikana kwa kituo cha Polisi cha kisasa. Tayari tuna eneo kwa ajili ya ujenzi, hivyo kupitia mpango wa Serikali wa ujenzi wa vituo vya Polisi katika ngazi ya kata, tunaomba kata yetu ipewe kipaumbele. Wananchi wako tayari kushiriki kikamilifu,” amesema Buhabi.

Nyumba za makazi ya Polisi zilizojengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na mgodi wa GGML.

Ujenzi wa nyumba pacha za makazi ya askari katika Kata ya Mgusu ulianza mwaka wa fedha 2019/2020, baada ya wakazi wa mitaa ya Mgusu, Manga, Machinjioni na Nyakabale kuamua kuanzisha mradi huo kwa kuchangia fedha taslimu pamoja na vifaa vya ujenzi.
Hatua hiyo iliwawezesha kujenga msingi na boma la nyumba hizo.

Baada ya kufikia hatua hiyo, mwaka 2023 uongozi wa kata uliwasilisha ombi la ufadhili kwa ajili ya kukamilisha ujenzi, ambapo ombi hilo lilikubaliwa.

Hadi kukamilika kwake, ujenzi wa nyumba hizo umegharimu zaidi ya Sh milioni 90, kati ya hizo Sh milioni 19.3 zilitokana na nguvu za wananchi, huku mgodi wa GGML ukichangia zaidi ya Sh milioni 77.

Kukamilika kwa nyumba hizo kunatajwa kuokoa gharama zilizokuwa zikitumika awali kulipia kodi ya pango kwa askari waliokuwa wakihudumu katika kituo hicho.

Awali, uongozi wa kata ulikuwa ukitumia takribani Sh milioni 5 kwa ajili ya kodi ya makazi ya askari, fedha ambazo sasa zimeelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigella(wa tano kutoka kushoto) akiwa na baadhi ya Viongozi wa  kamati ya ulinzi na usalama mkoa pamoja na mwakilishi mgodi wa GGML,Dijan Campbell baada ya uzinduzi wa nyumba za makazi ya Polisi kata ya Mgusu wilayani Geita.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, amesema uwepo wa kituo kidogo cha Polisi katika kata hiyo umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya kihalifu, hasa ikizingatiwa kuwa Mgusu ni eneo lenye shughuli nyingi za uchimbaji madini.

Ameushukuru Mgodi wa GGML kwa mchango wake katika ujenzi wa nyumba za askari, akisema hatua hiyo imekuwa chachu ya utendaji kazi bora wa Jeshi la Polisi.

Aidha, kamanda huyo ameuomba uongozi wa mgodi huo kuangalia uwezekano wa kusaidia ujenzi wa kituo kipya na cha kisasa cha Polisi katika eneo hilo.

“Kama walivyoonyesha nia njema katika ujenzi wa nyumba za askari, kupitia nafasi ya mgeni rasmi naomba pia watusaidie kujenga kituo cha Polisi chenye hadhi. Kata ya Mgusu ina idadi kubwa ya watu na inakua kwa kasi, hivyo inahitaji kituo kinachokidhi mahitaji ya sasa,” amesema Kamanda Jongo.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, akijibu ombi la ujenzi wa kituo cha polisi, amesema mgodi wa GGML umeonyesha utayari wa kusaidia ujenzi wa kituo hicho cha kisasa.

Hata hivyo, amesema ofisi yake itachangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuanza hatua za awali za ujenzi.

Aidha, Shigella amemwagiza Ofisa Mtendaji wa Kata na Diwani kuanza mara moja mchakato wa mawasiliano na mgodi, ili kuhakikisha maandalizi ya ujenzi yanaanza kwa wakati.

“Jengo la Ofisa Mtendaji haliwezi kukidhi mahitaji ya askari wetu. Tuanze safari ya mchakato huu. Diwani kwa kushirikiana na Ofisa Mtendaji wa Kata na Ofisa Tarafa, andaaeni eneo, na Kamanda wa Polisi Mkoa awasilishe ramani mapema ili ujenzi uanze,” amesema Shigella.

Dijan Campbell, mwakilishi kutoka mgodi wa GGML akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi nyumba za makazi ya Polisi kata ya Mgusu mkoani Geita.

Naye mwakilishi wa mgodi wa GGML, Dijan Campbell, amewashukuru viongozi wa Serikali katika kata hiyo kwa kulipa kipaumbele suala la usalama, akibainisha kuwa usalama ni msingi wa maendeleo ya taasisi na jamii yoyote.

“Tunafurahi kutimiza ahadi tuliyoitoa Januari 2023. Ujenzi huu ni kielelezo cha ushirikiano imara kati ya mgodi na wananchi. Tutaendelea kushirikiana na viongozi wa serikali za mitaa katika kuchochea maendeleo endelevu,” amesema Campbell.