KOCHA wa Esperance, Maher Kanzari ameondoka Tanzania na kurejea Tunisia akiwa na kumbukumbu ya kiungo mkabaji wa Simba, Yusuph Kagoma, baada ya nyota huyo kuwasumbua katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.
Kagoma alikuwa mhimili mkuu wa Simba katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo, akitawala eneo la kati katika kulinda na kushambulia, hali iliyovuruga kabisa mipango ya Esperance na kuwafanya washindwe kucheza vizuri.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kanzari hakusita kumtaja Kagoma kama chanzo kikuu cha matatizo yaliyowakumba kwenye dakika 45 za mwanzo.
“Tulikuwa na mpango wetu wa kushambulia mapema lakini katikati ya uwanja kulikuwa pagumu sana, niwe muwazi yule mchezaji namba 21 (Kagoma) alidhibiti mchezo kwa kushirikiana na mwenzake namba nane (Allasane Kante), walikatiza mipango yetu,” amesema Kanzari.
Kutokana na udhibiti huo wa katikati ya uwanja, Esperance ilishindwa kabisa kuifungua Simba katika kipindi cha kwanza, hali iliyosababisha wekundu wa Msimbazi kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na Shomary Kapombe na Yusuph Kagoma.
Takwimu za mchezo zinaonyesha sababu kwa nini Kagoma alikuwa tishio kwa Esperance. Kiungo huyo alikamilisha pasi zote 32 kati ya 32 alizopiga, sawa na asilimia 100 ya pasi sahihi.
Zaidi ya hapo, Kagoma alipiga pasi 10 sahihi kati ya 10 katika eneo la mwisho la uwanja wa Esperance, akichangia moja kwa moja katika ujenzi wa mashambulizi ya Simba na kuiweka timu pinzani katika presha.
Katika kubadili kasi ya mchezo, Kagoma alionyesha uwezo mkubwa kwa kupiga pasi ndefu tatu sahihi kati ya tatu, zote zikiwafikia walengwa wake bila makosa na kusaidia Simba kuhamisha mpira kwa haraka kutoka nyuma kwenda mbele.
Ingawa hakuunda nafasi kubwa za wazi za kufunga, mchango wake wa kimkakati ulikuwa muhimu huku takwimu zikionyesha alama ya kuhusika katika utengenezaji nafasi kwa 0.02, ishara ya ushiriki wake katika mchakato wa kutengeneza nafasi.
Katika upande wa ulinzi, Kagoma alihusika katika mapambano manne ya ana kwa ana, akishinda pambano moja la chini kati ya manne, huku akifanya makosa mawili tu katika dakika zote alizocheza, bila kusababisha kosa lolote lililopelekea bao au shuti hatari kwa timu yake.
Kanzari alikiri kuwa mambo yalianza kubadilika baada ya Kagoma kupata majeraha na kushindwa kuendelea na mchezo.
“Baada ya kutoka nje (Kagoma), tulipata uhuru zaidi wa kucheza, tulianza kutawala eneo la kati na ndipo mpango wetu ukaanza kufanya kazi,” amesema kocha huyo.
Esperance ilisawazisha mabao hayo katika kipindi cha pili, ikitumia vyema nafasi iliyojitokeza baada ya Simba kupoteza umiliki katika eneo la kati na kuwa na mianya mbele ya mabeki wa kati.
Hata hivyo, licha ya kucheza kwa dakika 58 pekee kisha nafasi yake kuchukuliwa na Naby Camara, Kagoma alibaki kuwa mchezaji mwenye alama za juu zaidi kwa Simba katika mchezo huo, akipata wastani wa alama (rate) 7.8 kati ya 10.
Sare hiyo iliyopata Simba, imehitimisha nafasi yake ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya nane katika misimu tisa kuanzia 2018-2019 kwani pointi moja iliyokusanya ikicheza mechi nne, haiwezi kutoboa hata ikizichapa Petro Atletico na Stade Malien itakwamia saba zinazoweza kufikiwa na wapinzani wake hao wawili, huku Stade Malien ikiwa tayari ipo juu na pointi nane.
Katika kundi hilo, kuna mchezo baina ya Esperance yenye pointi sita na Petro iliyokusanya pointi tano, hata wikiendi hii zikipoteza zote, basi matokeo ya aina yoyote zitakapokutana, ndiyo yanainyima Simba nafasi.
