Mwanza. Wawekezaji wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wamefunguka changamoto zinazowakwamisha kuwekeza, zikiwemo tozo na kodi nyingi, uratibu duni wa ofisi za Serikali, ukosefu wa miundombinu ya viwanda pamoja na migogoro ya fidia.
Wakizungumza leo Jumatano, Februari 4, 2026, wakati wa Kongamano la Uwekezaji kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa lililoandaliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) kama sehemu ya kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani.
Mwekezaji wa mkoani Mwanza, Pius Mkaungwa amesema wawekezaji wazawa wanahitaji usaidizi wa Serikali katika majadiliano na wawekezaji wa kigeni ili kufaidika, kwa kuwa sheria za uwekezaji ni nzuri lakini utekelezaji wake unawatesa walio wengi.
“Wawekezaji wazawa tupate usaidizi wa kutulinda hasa katika majadiliano na wawekezaji wa nje. Ukiangalia sheria zipo nzuri, lakini utekelezaji wake ndio changamoto,” amesema.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga akizungumza na wawekezaji wa Kanda ya Ziwa jijini Mwanza.
Theodore John kutoka Taasisi ya Wawekezaji wa Ndani ameeleza kuwa watendaji hawana ufahamu wa mchakato wa uwekezaji, hali inayosababisha kucheleweshwa kwa miradi na kudaiwa kodi mapema, na kuwa hata uratibu wa ofisi za Serikali haupo kwenye maeneo ya viwanda na uwekezaji yaliyotengwa.
“Tuna tatizo la elimu ya uwekezaji. Sisi tunapokwenda kwenye maeneo yaliyotengwa na Serikali, wale watendaji hawana elimu ya uwekezaji na jamii haina elimu ya uwekezaji,” amesema John.
Ameongeza, “Unapotenga eneo la viwanda, Tanesco hana taarifa kwamba hilo ni eneo la uwekezaji wa viwanda… unakuta hakuna maji, hakuna umeme. Ukianza kufuatilia unaambiwa hatuna bajeti hiyo. Tanesco, watu wa maji na ardhi wanatakiwa washirikiane ili mwekezaji anapokuja akute miundombinu inayohitajika kwa wakati huo.”
Kuhusu taasisi za kifedha, John amesema bado zina mtazamo wa kibiashara badala ya kiuwekezaji, hali inayomfanya mwekezaji kushindwa kupata mkopo kwa urahisi.
Ofisa Biashara, Viwanda na Uwekezaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Hashimu Kimwage, amesema changamoto kubwa ni fidia na miundombinu katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda.
“Halmashauri nyingi zimeandaa kongani za viwanda kwa ajili ya wawekezaji, lakini kumekuwa na changamoto kubwa sana ya fidia. Uwezo wa kulipa fidia bado upo chini… kuna hitaji Serikali kuu kupitia wizara zake kusaidia,” amesema Kimwage.
Ametaja changamoto nyingine ni miundombinu katika maeneo ya uwekezaji kwa kuwa yana changamoto ya barabara, maji, umeme na mawasiliano.
“Tukiweka miundombinu katika maeneo haya ya viwanda, itasaidia sana kuvutia wawekezaji,” amesema.
Mwekezaji mwingine, Mikidadi Sengo, amesema kodi nyingi hazina mpangilio na humletea ugumu mwekezaji kulipa pamoja na kumletea usumbufu unaofanya wengi kushindwa kuendeleza uwekezaji.
“Kodi imekuwa kilio cha wawekezaji wengi wa ndani. Kuna kodi nyingi sana ambazo hazina mpangilio maalum, kuanzia Serikali kuu pamoja na halmashauri. Wawekezaji wengi hawafahamu juu ya kodi, hivyo inakuwa changamoto kubwa kwao,” amesema.
Mfanyabiashara wa mazao ya uvuvi, Agness Noel, amesema Serikali irudie kumulika sheria ndogo ndogo na kubwa za uvuvi ili kuwawezesha wachakataji wa ndani kufikia masoko ya kimataifa.
Katibu Mkuu wa Wafanyabiashara Wamiliki wa Baa na Mahoteli, Michael Lugo, amesema, “Kikubwa kinatusumbua ni sheria ambazo zipo, zinakuwa ngumu kidogo kwa wawekezaji wa ndani kuwekeza.
“Mimi mwenyewe namiliki baa, lakini kodi ninazokutana nazo kwenye biashara inakuwa ngumu kupanua wigo au hamasa zaidi kwenda mbele. Kwa mfano, kuweka bango tu la biashara, lile bango linatakiwa kulipiwa kodi… watu wa afya wanakuambia kuna tozo ya usimamizi, tozo ya ukaguzi, fumigation na mambo mengine,” amesema Lugo.
Amesema hata katika leseni kuna kodi ya majengo, TRA kodi ya pango, lakini pia wakilipia umeme wanakatwa makato kwenye LUKU, hivyo tozo zinakuwa nyingi kwenye biashara kiasi kwamba wanashindwa kuwaza zaidi ya pale walipo.
“Tunaomba sheria ambazo zipo ziangaliwe na kuzifumua ili muweze kumwezesha huyu mwekezaji aone fursa nyingi zaidi ambazo zipo. Pia tozo zijumuishwe kwa pamoja,” amesema Lugo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wajasiriamali wa Kiadventista, Michael Antony amesema taasisi za Serikali hazina ushirikiano, nyingi zikitishia kufungia biashara pasipo kusikiliza changamoto za wawekezaji.
“Kila mtu akija kwenye eneo la biashara anatishia kwamba nafunga biashara. Hata akija mtu wa Osha anakwambia usipofanya hivi nafunga biashara. Niliomba ikiwezekana hizi taasisi za umma zifanye kazi kwa kushirikiana ili zipunguze mzigo kwa wanaotaka kuwekeza,” amesema Antony.
Akijibu changamoto hizo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema Serikali imeanza kuchukua hatua za kuboresha mfumo wa kodi na kuondoa mzigo kwa wawekezaji wa ndani.
“Serikali imesikia kilio cha wawekezaji. Rais (Samia Suluhu Hassan) aliunda tume ya kodi za Serikali kuu na zile za mitaa ili kuona tutakuwa na mfumo upi wa kikodi ambao utawezesha biashara zaidi na kuleta ushindani baina ya sekta binafsi ya ndani na uwekezaji kutoka nje,” amesema Kapinga na kuongeza;
“Tunaweka mazingira wezeshi ambayo sekta binafsi na wawekezaji wa ndani wataweza kushindana kwenye soko la ndani na nje ya nchi. Mheshimiwa Rais mwenyewe amelishikilia na analifanyia kazi.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Tiseza, Dk Aziz Mlima amesema wamepokea maelekezo ya Waziri na kuyatekeleza ili kuboresha mazingira ya uwekezaji, pia amekiri kupokea maoni na changamoto zilizotolewa na wawekezaji na wafanyabiashara wa Kanda ya Ziwa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema utekelezaji wa kampeni hiyo katika Kanda ya Ziwa utaongeza kasi ya uwekezaji wa ndani, huku akibainisha kuwa mikoa ya kanda hiyo inachangia takribani asilimia 25 ya Pato la Taifa.
