Dar es Salaam. Watanzania wenye shida ya macho kama mtoto wa jicho, presha ya macho, kutokuona mbali wameitwa kwenda kufanyiwa uchunguzi kisha kupata matibabu ikiwemo upasuaji na kupewa miwani bure.
Neema hiyo imetangazwa leo Jumatano Februari 4, 2026 na Mkurugenzi wa kliniki ya macho ya Optical Center, Dk Mkunde Kibwana itakayofanyika Kawe Dar es Salaam huku akisema upasuaji maalumu wanaoufanya ni wa mtoto wa jicho.
Dk Mkunde amesema huduma hiyo inatolewa kwa Watanzania wote watoto kwa watu wazima itakayoenda hadi Machi mwaka huu ambapo wameanza Kigamboni, kwa sasa wapo Kawe na wanazunguka Dar yote na kila Mtanzania kutoka mkoa wowote anaruhusiwa kwenda.
Amesema changamoto wanayoina kwa watu wengi wanaofika katika kliniki hiyo tangu zamani ni mtoto wa jicho, presha ya macho (glaucoma), kutokuona mbali, ambapo watu hao wanashindwa kuwa na miwani ambayo inawasaidia kuona kutokana na kushindwa kumudu gharama.
Shaib Yassin akionesha miwani na dawa alivyopewa katika kliniki ya macho inayoendelea hapa jijini Dar es Salaam.
Akitaja sababu za shida hizo za macho amesema zinatokana na kuzaliwa nayo akitolea mfano mtoto wa jicho, pia umri ambapo kadiri unavyosonga uwezo wa kuona hupungua, ugonjwa wa Kisukari, mtindo wa maisha pamoja na kutochunguza macho mara kwa mara.
“Mfumo wa maisha kwa sasa uko tofauti kwa sikuhizi kuna watoto ambao wanashida ya kutoona mbali kwasababu wanaanza kutumia vifaa kama simu, kompyuta wakiwa bado wadogo, hawachezi nje au kujishughulisha nje.
Amesema mfumo wa sasa wa maisha unawafanya watoto wengi kushinda ndani hawashughulishi macho nje kwahiyo akisema mtoto akizaliwa lazima jicho lifundishwe kuona mbali na karibu.
“Zamani tulikuwa tunawachaji hela wakija kwenye kliniki zetu za macho ila kwa mwaka huu tumepata wadau waliogharamia vifaa na huduma hizi, kwahiyo watu wanaokuja wanapata bila gharama yeyote,” amesema.
Akielezea baada ya kupata huduma, Shaibu Yassin kitoka Mikocheni B, amesema anashida ya macho inayomfanya kutoona vizuri hasa maandishi inayomsimbua kwa muda mrefu.
“Nimefka hapa nimepewa huduma nimepewa miwani bure. Jicho ndio maisha mwanadamu anapokuwa amekosa jicho anakosa hata imani ya kuona anamaisha mazuri,” amesema.
Jaffar Muhidin, mkazi wa Kawe amesema anashida ya macho ambayo inamfanya kuona ukungu hali inayomsababisha asione mbali.
“Shida hii imenianza zaidi ya mwaka sasa mwanzo macho yalikuwa yanawasha, Nashukuru nimefika hapa naendlea na huduma,” amesema.
Naye, Fatuma Mussa, mkazi wa Kawe amesema jicho lake la kushoto linachangamoto hivyo anapaswa kuonana na daktari bingwa ndio namsubiri hapa waweze kunitibia.
“Nilishawahi kupewa miwani huko zamani lakini sikuweza kusaidika. nimeteseka zaidi ya miaka minne,” amesema mama huyo.
