Winga Azam FC atimkia Kenya

WINGA wa Azam raia wa Senegal, Pape Doudou Diallo, amekamilisha uhamisho wa kujiunga na Shabana FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu, baada ya nyota huyo kukosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara.

Diallo aliyejiunga na kikosi hicho cha Azam Julai 30, 2025, akitokea ASC La Linguere de Saint-Louis aliyoichezea kwa mkopo kutokea Generation Foot, msimu wa 2024-2025, aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Senegal baada ya kufunga mabao 11.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu Msaidizi wa Azam, Rashid Seif, amesema mchezaji huyo ametolewa kwa mkopo kwenda katika kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu ya Kenya, kwa lengo la kupata nafasi ya kucheza zaidi mara kwa mara.

Nyota huyo anayeweza kucheza wingi zote ya kulia na kushoto huku akicheza pia nyuma ya mshambuliaji kwa ufasaha, amekosa nafasi ya kuonekana zaidi katika kikosi hicho cha Azam, jambo lililowafanya pia mabosi wa timu hiyo kumuachia akacheze.

Usajili wa Mzee Hassan Mzee ‘Aziz KI’, aliyejiunga na kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari 2026, akitokea KMKM ya visiwani Zanzibar, kumechangia kwa kiasi kikubwa pia nyota huyo kutolewa kwa mkopo, ili akapate nafasi sehemu nyingine.

Nyota huyo aliyezaliwa Desemba 26, 2002, bado ana mkataba na Azam hadi Juni 30, 2027, ambapo amejiunga na Shabana iliyo nafasi ya tatu kwa pointi 31 katika Ligi ya Kenya, baada ya kushinda mechi nane, sare saba na kupoteza nne.