Apigwa risasi, aporwa Sh54 milioni, akitoka benki

Songwe. Watu wanaodaiwa kuwa majambazi wamempiga risasi mkazi wa Tunduma, wilayani Momba mkoani Songwe, Yengo Mwapina na kumpora Sh54 milioni akiwa njiani kutoka benki.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, tukio hilo la unyang’anyi wa kutumia silaha limetokea Februari 4, 2026, saa 4 asubuhi katika eneo la Kisimani, Mtaa wa Unyamwanga, Kata ya Tunduma.

Kamanda Senga amesema Mwapina alivamiwa na watu watatu wasiojulikana, ambao walimfyatulia risasi kabla ya kumpora fedha hizo alizokuwa ametoka kuzichukua katika Benki ya NBC, Tunduma.

Amefafanua kuwa risasi hiyo ilimsababishia jeraha kiunoni upande wa kushoto, kabla ya watuhumiwa hao kutokomea kusikojulikana wakiwa na fedha hizo.

Mjeruhi alipelekwa Kituo cha Afya Tunduma kwa matibabu ya awali, kisha kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe kwa matibabu zaidi.

Kamanda Senga amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linaendelea na uchunguzi wa kina pamoja na msako mkali ili kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani.

Katika tukio jingine, Kamanda Senga amesema mkazi wa Kijiji cha Lukululu, wilayani Mbozi, Feriki Kareai, amefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi pembezoni mwa Mto Itemba.

Amesema tukio hilo limetokea Februari 2026, saa 7 mchana, katika Kijiji cha Lukululu, Kata ya Mlangali, Tarafa ya Iyula, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha Kareai alikuwa akichimba kifusi hicho kwa lengo la kutafuta madini ya dhahabu, hali iliyopelekea kifusi kuporomoka na kumfukia, na kusababisha kifo chake,” amesema Kamanda Senga.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limetoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini kiholela bila kufuata taratibu za usalama, kwani ni hatarishi na zinaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha.