Dodoma. Maofisa Habari na Mawasiliano serikalini wametakiwa kutumia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii ili kuelimisha na kuhabarisha watu kuhusu kazi za Serikali.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi Februari 5, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk John Jingu wakati wa kikao kazi cha kuwajenga uelewa maofisa habari na Mawasiliano wa Serikali.
Dk Jingu amesema mpango wa kutangaza mafanikio kupitia maofisa habari wa Serikali linahusu zaidi kujenga kizazi chenye usawa kupitia haki za kiuchumi.
Amesema kuwa pasipo kuwepo kwa usawa katika jamii, haitawezekana kujenga kizazi chenye maendeleo ya kweli na endelevu lakini jambo la muhimu ni kuhakikisha kazi za Serikali lazima zitangazwe.
“Ni muhimu zaidi kutangaza mambo mema lakini kazi zinazofanywa na Serikali yenu, tumieni majukwaa mbalimbali kuweka hadharani shughuli za Serikali ili Umma utambue,” amesema Dk Jingu.
Ofisa Maendeleo ya Jamii ambaye ni Mratibu wa Programu ya Kizazi chenye usawa, John Mapunda amesema lengo la kutoa mafunzo kwa Wakuu wa Vitengo vya Habari na Mawasiliano Serikalini ni kuwawezesha kufikisha kwa ufanisi.
Mapunda amesema wanalenga kupeleka ujumbe kwa jamii kuhusu mafanikio, fursa na mabadiliko chanya yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa programu hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais Tamisemi, Roida Andusamile amesisitiza umuhimu wa uratibu na mshikamano miongoni mwa vitengo vya mawasiliano serikalini ili kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi kwa wakati.
Andusamile amewataka wanahabari wa Serikali kutumia lugha inayoeleweka ambayo haiwezi kupotosha maana.