MABOSI wa Fountain Gate wamefikia uamuzi wa kuhamishia mechi zote za nyumbani za timu hiyo za Ligi Kuu na mashindano ya ndani kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, baada ya kuutumia mwanzo Tanzanite Kwaraa uliopo mjini Babati, Manyara.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya timu hiyo kucheza mechi ya mwisho juzi ya Ligi Kuu Bara na kutoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, ikiwa ni pendekezo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla.
Katika mechi hiyo ya mwisho kwenye Uwanja wa Tanzanite, wenyeji Fountain Gate walitangulia kupata bao kupitia kwa Kassim Haruna ‘Tiote’ dakika ya 43 kwa shuti kali nje ya eneo la 18, huku, Fabrice Ngoy akiisawazishia Namungo FC katika dakika ya 68.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Fountain Gate, Wendo Makau, amesema wamepata mwaliko wa kwenda kuutumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, ambapo kwa sasa uamuzi wa mwisho tayari umeshafikiwa.
Mkuu wa mkoa huyo, ni mlezi wa Mbuni ya Arusha inayoshiriki Ligi ya Championship msimu huu, ambapo Makalla alitangazwa kushika wadhifa huo rasmi tangu Oktoba 23, 2025, alipokutana na kuzungumza na menejimenti na wachezaji wa kikosi hicho.
Kwa sasa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid unatumiwa na timu za Mbuni na TMA zinazoshiriki Ligi ya Championship, huku mara ya mwisho kwa klabu ya Arusha kuuchezea kwa ajili ya Ligi Kuu ilikuwa ni JKT Oljoro iliyoshuka daraja msimu wa 2013-2014.