Dar es Salaam. Wakati dunia ikiwa kwenye kilele cha mapinduzi ya nne ya viwanda, teknolojia ya akili unde (AI) inatajwa kuwa injini mpya ya uchumi kimataifa.
Kitaalamu, AI ni uwezo wa mashine au mifumo ya kompyuta kuiga akili ya binadamu katika kufanya kazi kama vile kujifunza, kutatua matatizo na kutoa maamuzi.
Tofauti na kompyuta za zamani zilizofuata amri tu, AI ya sasa inajifunza kutokana na data na kuboresha utendaji wake kila siku bila kupewa maelekezo mapya.
Kuibuka kwa AI kumetajwa kuwa moja ya nguzo za uchumi wa kisasa, ikibadili namna watu wanavyofanya kazi, kuendesha biashara na kutoa huduma.
Teknolojia hii sasa inaonekana siyo tu kama nyenzo ya kisayansi, bali pia kama chanzo kipya cha fursa za kiuchumi kwa mataifa yanayoendelea, ikiwemo Tanzania.
Teknolojia hiyo kwa sasa inatumiwa katika shughuli za uzalishaji, kiafya, biashara, burudani ambapo hata sasa Tanzania ina azma ya kutumia teknolojia za kidigitali kama moja ya kichocheo katika wakati huu ambao zinazidi kushika kasi hasa katika matumizi ya AI.
Hadidu za rejea zinaonyesha kuwa uchumi wa AI unakadiriwa kutarajia kuongeza takriban Dola trilioni 15.7 kwenye pato la dunia ifikapo mwaka 2030.
Pia katika mkutano wa matumizi ya AI uliofanyikia Rwanda mwaka jana ulionesha Afrika inatarajia kupata jumla ya dola za Marekani trillion 2.9 ifikapo mwaka 2030 kutokana matumizi ya teknolojia ya AI.
Maeneo ya kiuchumi yanayotumia AI
Ikumbukwe kuna uhitaji wa wataalamu wa kuipa AI maelekezo “Prompt Engineers” na wachambuzi wa data, ajira ambazo zinaweza kufanywa na kijana aliyeko Tanzania kwa ajili ya kampuni iliyoko nje ya nchi.
Kuna zana za AI zinatumika katika maisha ya kila siku kama Chatbots ambazo zinatumika kwa huduma kwa wateja na biashara, mifumo ya uchambuzi wa taarifa (kwa benki, soko na mipango ya biashara), zana za ubunifu wa maudhui (maandishi, picha, muziki na video), AI katika afya (uchunguzi wa magonjwa na usimamizi wa taarifa za wagonjwa) pamoja na AI katika kilimo (utabiri wa mavuno, hali ya hewa na udhibiti wa magonjwa ya mazao).
AI inatumika kwenye kilimo biashara (Agri-Tech) ambapo inaweza kutabiri mabadiliko ya hali ya hewa, kupima afya ya udongo kupitia picha za satelaiti na kutambua wadudu kabla hawajaleta madhara. Hii inapunguza gharama na kuongeza tija kwa mkulima.
Sekta ya teknolojia ya fedha kupitia mifumo ya AI, benki zinaweza kutoa mikopo kwa haraka kwa kuchambua uwezo wa mtu kulipa (Credit scoring) bila kuhitaji dhamana ya ardhi pekee.
Pia, biashara za mtandaoni AI inasaidia wafanyabiashara wadogo kuwafikia wateja sahihi kwa gharama nafuu kuliko matangazo ya redio au magazeti.
Kwa upande wa dunia, nchi kama Marekani, China, na Singapore zimeanza kuingiza AI kwenye mifumo ya usafirishaji kupitia magari yanayojiendesha na viwanda ambavyo roboti zinafanya kazi kwa usahihi wa asilimia 100.
Kiuchumi, AI imekuwa injini ya kuongeza tija na kupunguza gharama ambapo biashara huitumia kuboresha huduma kwa wateja bila kuongeza wafanyakazi wengi, kuchambua soko na tabia za wateja kwa usahihi.
Aidha, kugundua mianya ya hasara na udanganyifu wa kifedha pamoja na kuharakisha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa. Kwa kufanya hivyo, kampuni huongeza faida, ushindani na ufanisi wa kiutendaji.
Kwa upande wa Tanzania, matumizi ya AI bado yako katika hatua za awali lakini fursa ni kubwa. Kuenea kwa intaneti, simu janja na huduma za kifedha za kidijitali kumeweka msingi mzuri wa ukuaji wa AI.
Sekta kama benki, mawasiliano, afya binafsi, elimu mtandaoni na biashara za mtandaoni zinaanza kunufaika na teknolojia hii.
Wataalamu wanasema endapo kutakuwa na uwekezaji zaidi katika elimu ya Tehama, sera rafiki za ubunifu na usalama wa taarifa, AI inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuchochea uchumi wa Tanzania, hasa kwa vijana na wajasiriamali.
Hata hivyo muamko umeanza kukua ambapo tayari tunaona matumizi ya AI kwenye huduma za afya ikiwemo katika kuchambua picha za X-ray, sekta ya mawasiliano na vijana wabunifu wanaoanza kutengeneza miradi mbalimbali (Startups) zinazotumia AI kutatua matatizo ya usafirishaji.
Serikali kupitia Wizara ya Habari na Teknolojia tayari imeanza mchakato wa kuandaa Sera ya Taifa ya AI ili kuweka mazingira wezeshi.
Akizungumza na Mwananchi mtengeneza maudhui ya AI, Beatrice Materu anasema anaitumia teknolojia hiyo kutengeneza video za matangazo akisema ndipo dunia ilipo hivi sasa. “Zamani ukitaka kutengeneza video iwe tangazo au muziki lazima ukodi vifaa, ukodi wanamitindo, mnakuwa wengi lakini AI unatengeneza tu wazo unataka iweje unaipa malekezo inakuletea tangazo lako,” anasema.
Beatrice anasema AI imemrahisishia kufanya kazi zake za uzalishaji maudhui na alianza kujifunza teknolojia hiyo baada ya kuona ndipo dunia ilipo na inapoelekea.
“AI ipo lazima tuelewe hilo, Mfano unaweza ukatumia AI kubadilisha wasilisho la Powerpoint kuwa video au unaweza ukatengeenza video ikiwa na muendelezo wa scene,” anasema. Beatrice anasema AI ni fursa ya kiuchumi kwa kuwa inaingiza pesa, mfano watu wanaofanya biashara mtandaoni hawana ulazima wa kutafuta watu wakatengeneza matangazo bali wanaweza kutumia AI.
Mtaalamu wa teknolojia Francis Nyonzo anasema kwa sasa bado watu wanakataa na kukubali AI kwa wakati mmoja ukirejea makosa yanayofanywa katika kazi zake hasa utengenezaji wa maudhui.
“Tujiulize matokeo ya AI ni yapi kiuchumi ripoti ya Jukwaa la Uchumi duniani (WEF) ilisema kazi za afya, walimu na mainjinia watabaki na kazi zao hadi ifikapo miaka ya 2030. Ijapokuwa kazi za watu wengi kama watengeneza maudhui zitachukuliwa inabidi tuonyeze ubunifu tusijiegemeze kwenye AI,” anasema.
Nyonzo anasema watu wenye utaalamu wa AI watakuwa na nafasi kubwa ya kupata pesa kuliko wale wasiofahamu kadiri siku zinavyokwenda.
“Fursa za AI tuzungumze kwanza ufahamu wa AI yenyewe kwamaana ukiifahamu iitakuwa rahisi katika utendaji wa kazi za sekta yeyote…”
Mkurugenzi Mtendaji wa Koncept Group, Krantz Mwantepele anasema akili unde ni fursa ya kipato kwa kufungua ajira mpya, kupunguza gharama za kuanza kazi.