Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kuwaadhibu madereva na makondakta wa daladala wanaowanyanyasa wanafunzi.
Profesa Mbarawa ametoa maelekezo hayo kwa mamlaka hiyo jana, Jumatano Februari 4, 2026 katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dodoma.
Hata hivyo, baadhi ya makondakta na madereva wamedai kuwa, mazingira ya biashara yanawalazimu kufanya hivyo.
Wadau hao wa usafiri wa daladala, wamesema kabla Serikali haijachukua hatua, inapaswa kufanya utafiti kubaini uhalisia wa tatizo, kwa kuwa shida haipo kwa makondakta na madereva pekee, wakati mwingine hata wanafunzi ni tatizo.
Wamesema baadhi ya wanafunzi wanachagua kupanda daladala zenye muziki pekee, wengine wakikaa kwenye viti wanagoma kuwapisha watu wazima, ilhali nauli wanazolipa ni chini ya nusu ya inayolipwa na mkubwa.
Kwa mujibu wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), tatizo ni kubwa, huku kikitahadharisha kuwa, ili hatua zichukuliwe kunahitajika uchunguzi wa kina, utakaohusisha wadau wote.
Msingi wa agizo la Profesa Mbarawa, ni malalamiko ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Jangwani jijini Dar es Salaam, aliyeandika barua kulalamikia kubaguliwa na makondakta wa daladala kwa kuwa hawalipi nauli kamili.
Kwa mujibu wa barua hiyo iliyonukuliwa na Profesa Mbarawa, wanafunzi inawalazimu kusimama barabarani kwa muda mrefu wakisubiri usafiri, wanachelewa kufika shuleni na wakati mwingine wanashindwa kabisa kufika.
Hata hivyo, changamoto ya usafiri kwa wanafunzi haijaanza sasa, ilikuwepo enzi na enzi. Kwa sababu ya changamoto hiyo, baadhi ya wanafunzi walilazimika kupigana na makondakta ili kupanda kuwahi shule na kurudi majumbani.
Kwa sababu ya changamoto hiyo, ndipo shule za umma kama Olympio na Bunge za Dar es Salaam zilipoamua kuanzisha utaratibu wa usafiri maalumu wa wanafunzi kwa ajili ya shule hizo.
Jana, Jumatano Februari 4, 2026 Profesa ameielekeza Latra kuhakikisha uthibitishaji wa madereva na kusajili wahudumu kwenye mabasi, unafanywa kwa kasi katika miji yote nchini na kutoa adhabu kali kwa madereva na makondakta watakaobainika kuwanyanyasa wanafunzi.
Pia, ametaka kuimarisha udhibiti wa nauli maalumu za wanafunzi, staha ya huduma na usalama wao kwa wakati wote na kuendelea kutoa elimu kwa watoa huduma na watumia huduma wajue haki na wajibu wa kila mmoja.
Ametaka Latra kuhakikisha treni za abiria, daladala zote nchini na mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani zimeandikwa namba za bure ili abiria wapige wanaponyanyaswa, huku Polisi wakifanya ukaguzi wa mara kwa mara vituoni.
Hata hivyo, amesema mikakati ya Serikali ni kuanzisha huduma za mabasi maalumu yaendayo haraka kwa ajili ya wanafunzi, hususan asubuhi na jioni.
Hatua nyingine amesema ni kutenga mabehewa maalumu kwa ajili ya wanafunzi kwenye treni za mijini (Dar es Salaam), ili kupunguza msongamano, kuongeza usalama na kutoa unafuu wa usafiri kwa wanafunzi.
“Kurasimisha na kusimamia utozaji wa nauli maalumu ya Sh200 kwa wanafunzi katika mabasi yaendayo haraka na daladala, kwa mujibu wa taratibu na kanuni zilizowekwa. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata huduma hizi kwa gharama nafuu,” amesema.
Mikakati mingine, amesema ni kutekeleza sheria na kanuni za kuthibitisha madereva na kusajili wahudumu wa vyombo vya usafiri wa umma yaani mabasi na treni.
Baada ya agizo hilo la Waziri Mbarawa, Mwananchi imezungumza na mmoja wa viongozi wa juu wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), aliyeomba hifadhi ya jina lake, akisema kabla ya Serikali kutoa adhabu, inapaswa kufanyike utafiti wa kina kupata uhalisia wa tatizo.
Amesema wanafunzi wanaowahi kufika vituoni, hususan asubuhi, mara nyingi hupata huduma, lakini kutokana na wingi wa abiria na mahitaji ya kibiashara, wahudumu hulazimika kuzingatia mapato yanayoingia.
“Wanafunzi wanaowahi kwenye vituo wanahudumiwa, lakini muda wa biashara ukiwa na wateja wengi ni lazima uangalie hesabu inayoingia,” amesema.
Katika mazingira ambayo baadhi ya abiria hulipa nauli ndogo (Sh200) huku wengine wakitakiwa kulipa nauli kubwa, amesema kipaumbele lazima kitatolewa kwa wanaolipa zaidi.
“Kuna mambo mengi ya kuzingatia. Mbona mabasi ya wanafunzi yanatoza nauli kubwa, lakini hiyo imefanyika kwa mipango maalumu iliyowekwa kwa ushirikiano na wazazi,” amesema.
Hata hivyo, amesema wazo la kubeba wanafunzi wengi kwa wakati mmoja katika mazingira ya usafiri na miundombinu ya Jiji la Dar es Salaam ni gumu kutekelezeka na linaweza kusababisha hasara kwa waendeshaji.
“Hatukatai kubeba wanafunzi, lakini Serikali izingatie daladala ni biashara kama biashara nyingine, tunalipa kodi. Malalamiko ya wanafunzi yalipaswa kufanyiwa utafiti na kutafutiwa suluhu badala ya kulaumu daladala,” amesema.
Amesema kuna maeneo ambayo daladala hubeba wanafunzi wengi pale ambako hakuna abiria wengi, mfano Kigamboni, lakini katika baadhi ya maeneo wanafunzi huachwa kutokana na umbali mfupi wa wanapokwenda.
“Pia, inapaswa wawe na nauli kamili kwa sababu chenji siku hizi hununuliwa. Kilichofanyika ni kuwachonganisha wafanyabiashara na Serikali, ilhali utafiti ungefanyika kwanza kubaini ukweli wa jambo hilo,” amesema.
Dereva wa daladala mkoani Dar es Salaam, Abdallah Said amesema kazi ya udereva ni sawa na kazi nyingine yoyote na madereva wanalazimika kuheshimu masharti ya waajiri wao, ikiwamo kufikisha hesabu zinazotakiwa, la sivyo hupoteza ajira.
Amesema dereva anaweza kulazimika kuacha kazi endapo atashindwa kukidhi kiwango cha hesabu kinachotakiwa na mmiliki wa chombo, hata kama sababu ni kubeba wanafunzi.
“Mimi ni binadamu nafanya kazi hii. Sipendi kumuacha mtoto njiani wala siwezi kufurahia, tena mwenyewe nina watoto. Lakini inafika wakati, hasa asubuhi na jioni, wanafunzi ni wengi na wateja ni wengi. Unafungua biashara asubuhi na jioni unatakiwa kufunga hesabu unafanyaje?” amehoji.
Mwenyekiti wa Umoja wa Makondakta kutoka Mkoa wa Mwanza, Self Nassor amesema ni muhimu utafiti ufanywe kwa sababu hata wanafunzi wanachagua gari ya kupanda.
“Wengi wanataka kupanda gari yenye muziki na yale ambayo hayana muziki hawapandi na wengine wanalipa nauli kamili na wanakaa kwenye siti,” amesema.
Amesema changamoto hiyo ipo na si kwamba makondakta wanashida peke yao, baadhi ya wanafunzi hata wakipata siti, hawataki kuwapisha watu wazima.
Katibu Mkuu wa Chakua, Hashim Ramadhan amesema wamekuwa wakikumbana na migogoro hiyo mara kwa mara.
Amesema makondakta wamekuwa wakiwalazimisha wanafunzi kulipa kati ya Sh500 hadi Sh700, na wanafunzi wasiokuwa na kiasi hicho hunyimwa usafiri.
Amesema wasichana ndio waathirika wakubwa zaidi wa hali hiyo, akisema baadhi yao hutoka shuleni saa tisa alasiri lakini hufika nyumbani hadi saa tatu usiku kutokana na kusubiri usafiri kwa muda mrefu.
Kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali, Ramadhan amesema zitakuwa na tija endapo zitatekelezwa kwa vitendo kwa kushirikisha wadau wote, pamoja na ufuatiliaji wa karibu na utoaji wa adhabu kwa wanaokiuka sheria.
“Kama zitabaki kuwa ni maneno matupu bila vitendo, tabia hii haiwezi kukoma,” amesema.
Juma Selim, mzazi wa mwanafunzi jijini Dar es Salaam, amesema amewahi kumpokea mwanaye akiwa na jeraha lililosababishwa na kusukumwa na kondakta, wakati akigombea daladala.
“Mtoto alikuwa anapambana apande, kondakta anamsukuma asipande wapande wakubwa kwa sababu nauli ya mwanafunzi ndogo, akaanguka akaumia. Kuna mengi wanakutana nayo watoto. Serikali isimame hasa kuwalinda wanafunzi,” amesema.
Mzazi mwingine, Neema Mollel mkazi wa Arusha amesema imekuwa kawaida mwanaye kumsimulia vituko vya makondakta kila siku anaporudi kutoka shuleni. Siku amemsukuma, amemsimamisha mlangoni, kubanwa na mambo mengine hatari kwa mwanafunzi.
“Mwanangu ananiambia hawaruhusiwi kupanda hadi daladala iwe imejaa kwanza. Sasa ikijaa mtoto mfupi anaumia sana anakosa pumzi ni mateso, wanateseka. Wengine wanawakataa. Mwanangu anatoa shuleni saa 10 lakini nyumbani anafika saa moja usiku, wakati alipaswa afike saa 11 jioni,” amesema.
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Suleiman Ikomba amesema kuwaacha wanafunzi barabarani bila usafiri wa kwenda au kurudi shuleni si jambo jema na lina madhara kwa Taifa.
Amesema kuna haja kwa mamlaka husika kuchukua hatua stahiki kushughulikia suala hilo, kwa busara za kawaida si sahihi kuwaacha wanafunzi barabarani, hasa wanapokuwa wanawahi kufika shuleni.
“Kwa macho ya kawaida ya ndani, si jambo jema kuona watoto wanaachwa barabarani na mabasi wakati wanatakiwa kuwahi shule,” ameongeza.
Ikomba amesema kuchelewa kwa mtoto kufika shuleni au kurudi nyumbani kunamuathiri kisaikolojia, hasa ikizingatiwa mtoto anaishi kwa kutegemea watu wazima.
“Hatuwezi kujenga kizazi kinachochukia wafanyabiashara wa magari tangu wakiwa wadogo kwa sababu ya kuachwa njiani,” amesema.
Amesema jambo hilo si madereva wa daladala pekee, bali pia kwa watu binafsi wenye vyombo vya usafiri, kubeba jukumu la kuwasaidia wanafunzi pale inapowezekana.