ZIKIWA zimesalia dakika 180 kwa Azam FC kusaka tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kocha mkuu wa kikosi hicho, Florent Ibenge, amesema timu hiyo imeitolea macho zaidi mechi moja ya matumaini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge amesema hatma yao ya kwenda robo fainali itakuwa ndani ya dakika 90 zijazo mbele ya Union Maniema ya DR Congo.
Amesema mchezo huo utakaochezwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar ambao Azam itakuwa nyumbani, wanajipanga kulipa kisasi, ingawa wanatambua haitakuwa rahisi kutokana na uimara wa wapinzani wao.
“Nimewaambia wachezaji wangu wanatakiwa kucheza kama fainali mchezo huo ili washinde na waandike historia mpya na kwenda kutafuta pointi ugenini dhidi ya Wydad.
“Hii ni mechi ya kwenda kulipa kisasi kwani Maniema walitamba kwenye uwanja wa kwao na sasa ni zamu yetu, hivyo hakuna cha kutuzuia kushinda.”
Aliongeza kuwa: “Wapinzani wote waliosalia katika mechi zilizobaki waliwafunga katika michezo ya kwanza, ila huu ambao utakuwa wa mwisho kwenye uwanja wetu wa nyumbani ndio wa kufa au kupona ili kupata alama tatu muhimu.”
Ikumbukwe kuwa, Azam ilikutana na Maniema ugenini na kuchezea kichapo cha mabao 2-0, kisha ikafungwa 1-0 dhidi ya Wydad ikiwa nyumbani.
Baada ya mechi hizo, Azam ilikutana na Nairobi United na kuwachapa mabao 3-1 katika michezo miwili mfululizo na kuchota pointi sita kibabe. Ilianza ugenini kushinda 2-1, kisha nyumbani 1-0.
IBE 02
Azam iko Kundi B la Kombe la Shirikisho Afrika, ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 6, vinara ni Wydad yenye pointi tisa sawa na Maniema. Nairobi United inaburuza mkia ikiwa haina pointi.
Baada ya kucheza na Maniema, Februari 15, mwaka huu, Azam itakuwa Morocco kumalizana na Wydad katika mechi ya sita ya hatua ya makundi.
Ili Azam ifuzu robo fainali bila ya kuangalia matokeo ya wapinzani wake, inatakiwa kuichapa Maniema na Wydad ili kumaliza kundi ikiwa na pointi 12.