Je, Fedha za kidijitali zinaweza kuziba ufa wa usawa kati ya mijini na vijijini Tanzania?

Kwa miongo kadhaa, uchumi wa Tanzania umekuwa na taswira mbili tofauti: upande mmoja ni miji inayokua kwa kasi kama Dar es Salaam na Mwanza, ambako huduma za kibenki na fursa za kibiashara zinapatikana kila kona na upande wa pili ni vijijini, ambako mkulima wa mpunga au mfugaji analazimika kusafiri mwendo mrefu kufuata huduma za kifedha.

Hata hivyo, mapinduzi ya huduma za fedha kwa njia ya simu (FinTech) yameleta matumaini mapya.

Swali kuu linabaki, Je, teknolojia hii ina uwezo wa kuziba ufa wa kiuchumi uliopo kati ya mkazi wa mjini na yule wa kijijini?

Ukweli ni kwamba fedha za kidijitali zimevunja kuta ambazo mabenki ya asili yalishindwa kuzivunja.

Katika takwimu za hivi karibuni, tunaona kuwa ushiriki wa wananchi katika mfumo wa fedha umeongezeka kwa kiasi kikubwa kupitia miamala ya simu kwani sasa mkulima wa kijijini anao uwezo wa kupokea malipo ya mazao yake moja kwa moja kwenye simu, bila kupitia madalali wa mjini ni hatua kubwa kuelekea usawa.

Hii inamwondolea hatari ya kubeba fedha taslimu na inampunguzia gharama za usafiri. Kidijitali imekuwa “daraja” linalomunganisha mzalishaji wa vijijini na soko la kitaifa na hata la kimataifa.

Hata hivyo, ili fedha hizi za kidijitali ziweze kweli kuziba ufa wa usawa lazima ziende mbali zaidi ya kutoa na kuweka fedha. Changamoto kubwa vijijini bado ni upatikanaji wa mitaji.

Wakati wakazi wa mijini wanaweza kutumia mali zao kama dhamana ya mikopo mikubwa, wakulima wengi hawana hati miliki za ardhi.

Hapa ndipo mifumo ya kidijitali inapopaswa kuonesha maajabu yake kwa kutumia “data” za miamala kama kigezo cha ukopeshi.

Ikiwa mfumo utaweza kumtambua mkulima mwaminifu kupitia historia yake ya kununua mbolea na kuuza mazao kwa simu, basi tutakuwa tumeanza rasmi safari ya kuondoa umaskini wa vijijini.

Lakini, kuna vikwazo vinavyoweza kukwamisha ndoto hii. Changamoto ya kwanza ni miundombinu na gharama za matumizi kwani Katika maeneo mengi ya vijijini, upatikanaji wa mtandao wa intaneti wa kasi (3G au 4G) bado ni wa kusuasua.

Aidha, kodi na tozo kwenye miamala ya simu zinaweza kuwa mzigo mzito kwa mwananchi wa kijijini ambaye kipato chake ni kidogo na cha msimu.

Ikiwa gharama ya kutuma na kutoa fedha itabaki kuwa juu, wale walio pembezoni wataendelea kutumia mfumo wa fedha taslimu, jambo ambalo linawaweka nje ya mfumo rasmi wa kiuchumi.

Vilevile, elimu ya kidijitali ni nyenzo muhimu na Haidhuru kuwa na teknolojia ya kisasa ikiwa mtumiaji wa mwisho hana uelewa wa jinsi ya kuitumia kwa tija.

Kuna haja ya kuwekeza katika kampeni za kuelimisha jamii za vijijini kuhusu usalama wa fedha zao na namna ya kutumia majukwaa ya kidijitali kutunza akiba na kuwekeza.

Bila elimu hii, fedha za kidijitali zinaweza kuongeza usawa kwa kuwaingiza wananchi kwenye madeni ya mikopo ya kidijitali yenye riba kubwa bila wao kuelewa athari zake.

Kwa kuhitimisha, fedha za kidijitali zina uwezo mkubwa wa kuwa mkombozi wa usawa nchini Tanzania. Zinaweza kufanya mzunguko wa fedha kuwa jumuishi zaidi na kupunguza utegemezi wa vijijini kwa miji.

Lakini, mafanikio haya yanategemea utashi wa kisiasa katika kupunguza tozo, kuboresha miundombinu ya nishati na mawasiliano vijijini, na kuhakikisha kuwa sheria za nchi zinalinda watumiaji wadogo.

Tukifanya hivyo, teknolojia haitakuwa tu anasa ya mjini, bali itakuwa injini ya maendeleo itakayomwinua mtanzania wa kila hali, popote alipo.