Mwanza. Maofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wa kanda za Kusini, Mashariki na Kaskazini wanatarajiwa kufundwa mbinu za kukabiliana na uvunaji na usafirishaji haramu wa mikoko unaofanyika katika ukanda wa Bahari nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya wiki mbili leo Alhamisi Februari 5, 2026 Kamanda wa TFS Kanda ya Ziwa, Ebrantino Mgiye amesema uvunaji haramu wa mikoko ni changamoto itakayodhibitiwa na maofisa hao baada ya kupewa mbinu mbalimbali ya kudhibiti uharifu huo.
“Tumeona umuhimu wa mafunzo haya ili kuwaweka tayri…kwenye ukanda huu tuna changamoto ya uvunaji na usafirishaji haramu wa mazao ya mikoko. Tunafahamu Msitu ya mikoko inatoa mchango mkubwa sana wa kulinda bainaoi kwa maana ya kuzuia upepo mkali, lakini pia ni mazalia ya viumbe baharini,” amesema Mgiye.
Mikoko inayovunwa kiharamu hutumika kwa ajili ya kuni na mkaa kutengeneza mbao na fito za ujenzi, zana za uvuvi kama mitumbwi pamoja na kusafirishwa kinyume cha sheria kwa ajili ya biashara.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, katika mwaka wa fedha 2023/24 kupitia doria zilizofanywa na TFS, magunia 21,596 ya mkaa uliovunwa bila kufuata utaratibu, mbao 24,036 zenye ujazo wa mita 1,498, kuni zenye ujazo wa mita 90, na magogo 1,256 yenye ujazo wa mita 415 yalikamatwa na kutaifishwa.
Mgiye amesema kupitia mafunzo hayo kwa maofisa uhifadhi wanaojihusisha zaidi na jukumu la kulinda rasilimali za mikoko, yatasaidia maofisa hao kudhibiti uvunaji haramu, kulinda misitu ya mikoko na kuhakikisha rasilimali hizo muhimu za taifa zinabaki salama.
Amesema mikoko huzuia mmomonyoko wa ardhi na kulinda fukwe, kudhibiti upepo wa baharini, ni mazalia ya samaki na viumbe wengine wa majini lakini pia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa hunyonya na kuhifadhi kaboni.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akifungua mafunzo ya kukabiliana na uvunaji haramu na usafirishaji wa mikoko kwa maofisa wa TFS yaliyofanyika jijini Mwanza.
Mkuu wa Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ndagile Makubi, amesema mafunzo hayo ya wiki mbili yatawapa maofisa hao zaidi ya 11 maarifa ya kufanya kazi zao kwa ufanisi na usalama, mbinu, ujuzi na uzalendo katika kulinda rasilimali hiyo.
“Lakini pia yatawajengea uwezo wa kuishi majini…watu wengi wanapoteza maisha kwa sabau wanakosa mbinu na uwezo wa kuishi majini, kwa hiyo hapa tutawafundisha hawa wanafunzi mbinu za kuishi majini,” amesema.
Ameongeza; “Tutawafundisha ukamataji, upekuzi na uzuiaji wa vyombo vinavyotiliwa mashaka ya kiuharifu, watafundishwa namna ya kutunza vile vyombo vya majini na vitendea kazi kwa maana ya boti, injini na vitendea kazi vingine, lakini pia tutawaongezea uwezo wa kuogelea.”
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema tayari Serikali imeiona changamoto ya uvunaji haramu na usafirishaji wa mikoko hivyo kuandaa rasilimali watu na mafunzo, vitendea kazi pamoja na kutunga sheria ili kuikabili.
“Hifadhi ya mikoko ni rasilimali muhimu sana katika Taifa letu katika kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, kuimarisha maisha ya jamii ya pwani na kuchangia pato la Taifa,” ameeleza.
Kwa mujibu wa TFS, Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye misitu mikubwa ya mikoko barani Afrika, inayopatikana kando ya pwani yenye urefu wa kilomita 1,424 kuanzia mpaka wa Kenya hadi Msumbiji. Mikoko inakadiriwa kufunika hekta 158,000, huku Delta ya Rufiji ikiwa na mkusanyiko mkubwa zaidi wa hekta 62,000.
Mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni msaidizi misitu, Mwamvua Ramadhani amesema elimu hiyo ina manufaa kwa taasisi na kwa Taifa kwa ujumla kwa sababu maliasili ambazo zingeweza kupotea kwa kukosekana wataalamu wa kufuatilia waharifu kwenye maji zinaweza kupatikana kutokana na mbinu watakazo pewa.
Naye, Mhifadhi Mwandamizi, Christina Ngalawa amesema mafunzo hayo yataongeza uwezo wa TFS kusimamia misitu ya mikoko, maziwa makuu na mito, na kudhibiti usafirishaji haramu.