Mashujaa yachoka unyonge Ligi Kuu, yaivimbia Prisons

MATOKEO ya kukosa ushindi katika mechi tano mfululizo yameonekana kuwaumiza Mashujaa FC, huku benchi la ufundi likitoa msimamo kwa nyota wake na kuahidi kurejesha kasi waliyoanza nayo msimu huu.

Huu ukiwa ni msimu wa tatu Mashujaa inashiriki Ligi Kuu, ilikuwa na mwanzo mzuri msimu huu hadi kukaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu kabla ya mambo kuwaharibikia na kujikuta nafasi ya 10 kwa pointi 13.

Katika mechi tano za mwisho, timu hiyo haijaonja ushindi wowote, ikiwa ni kupoteza tatu kwa kuruhusu mabao tisa na sare mbili huku ikiambulia patupu bila bao.

Akizungumza jijini hapa, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Charles Fredi, amesema mechi zilizopita wamepata matokeo mabaya na mwenendo si mzuri akieleza kuwa hali hiyo inawaumiza wote ndani na nje ya timu.

Amesema baada ya matokeo hayo, wamekaa na kutafakari walipokosea, hivyo kuanzia mchezo ujao dhidi ya Tanzania Prisons kesho Ijumaa wanaamini watarejesha ubora wao na kasi waliyoanza nayo msimu.

“Imetuumiza wote, matokeo si mazuri na mwenendo ni mbaya ila tumeona tulipokosea na kuanzia mchezo wa kesho dhidi ya Prisons tunahitaji ushindi ili kurekebisha makosa na kufanya vizuri,” amesema kocha huyo.

Kwa upande wake straika wa timu hiyo, Chrispin Ngushi, amesema wamekuwa na ubutu kwenye kufunga mabao, lakini mazoezi waliyofanya anaamini Mashujaa itarejesha upya makali yake.

“Tumekuwa tunapata nafasi za mabao tunashindwa kutumia vyema, sisi washambuliaji kiu na kilio chetu ni kuona tunaipa matokeo mazuri timu na tunaahidi mechi ijayo tutaanza upya,” amesema nyota huyo.