Dodoma. Wabunge wamemaliza uchaguzi wao leo kwa kumchagua aliyepata shida ya kuzungumza lugha ya Kiingereza alipokuwa akiomba kura kuwania nafasi ya uwakilishi kwenye Bunge la Dunia, huku aliyewahi kuwa Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko akichaguliwa kuwa Mjumbe katika Tume ya Utumishi wa Bunge.
Mbunge huyo wa Ukonga kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Bakari Shingo alishindwa kujieleza kwa lugha ya Kiingereza wakati akiomba nafasi hiyo ambayo alikuwa mgombea pekee.
Uchaguzi huo umefanyika leo Alhamisi Februari 5, 2026, wakati wa kujieleza kulizuka vitimbwi kwa baadhi ya wabunge hasa kwenye lugha ya kiingereza, ambayo ilikuwa kigezo kilichotangazwa kwa waombaji.
Hata hivyo, mbunge huyo ameshinda kwenye nafasi hiyo ya Jukwaa la Mabunge ya Maziwa Makuu.
Lakini, Dk Biteko hakuwepo wakati wabunge wengine wakijinadi ndani ya ukumbi, lakini kiti kilimuombea kura kwa nafasi yake na walioshinda wote ni madaktari kitaaluma, akiwamo Charles Mahela na Catherine Joachim na upande wa Zanzibar, wamechagulia Haji Amour Haji na Mgeni Hassan Juma.
Kwenye Tume ya Utumishi wa Bunge wamo pia Agnesta Kaiza na Ado Shaibu ambao wanawakilisha kundi la walio wachache Bungeni.
Waliochaguliwa kwenye Bunge la Afrika (PA)ni Lulu Mwacha, Iman Mtumwa Vuai, Mariam Mungula, Joshua Nasari na Rashidi Habibu Ali, wakati Bunge la SADC-PF, amechagulia Profesa Joyce Ndalichako, Kassim Hassan Haji, Lutengano Mwalwiba, Mwanahamisi Munkunda na Mohame Khalin Issa.
Kwenye Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), waliochaguliwa ni Dk Pindi Chana, Dk Zeyana Abdalla Hamad, Rashid Shangazi, Asha Feruzi, Elibarick Kingu, Fatuma Ulenge wakati kwa waliowachache amechaguliwa Kiza Mayeye.
Nafasi nyingine ilikuwa ni ya uwakilishi wa Umoja wa Mabunge ya Maziwa Makuu wakuichaguliwa ni Slivia Sigula, Said Salim Hamad, Ezra Chiwelesa, Cosmas Mtesigwa na Bakari Shingo.
Baada ya matokeo, Mbunge wa Geita, Joseph Msukuma aliomba mwongozo wa Spika akihoji namna gani mbunge ambaye hakuwezi kuzungumza Kiingereza amechaguliwa, huku akidai hali hiyo imewanyima fursa hata wao (Msukuma) ambao wangeweza kugombea pia.
Akijibu hoja hiyo, Spika wa Bunge, Mussa Zungu amesema hakukuwa na namna kwa sababu nafasi ilikuwa moja na aliyetakiwa kuchaguliwa alikuwa mmoja kutoka kambi ya waliowachache na amepatikana, hivyo atajifunza mbele ya safari.