MIAKA 49 YA CCM: Mafanikio, mageuzi na changamoto za kizazi kipya

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), leo Februari 5, 2026 kinaadhimisha miaka 49 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977, tukio linalotajwa kuwa la kihistoria katika siasa za Tanzania.

Sherehe hizo zinakwenda sambamba na tathmini ya safari ya chama, mwelekeo wake na mustakabali wake wa baadaye.

Kwa takribani nusu karne, CCM iliyozaliwa baada ya muungano wa Tanganyika African National Union (Tanu) na Afro-Shirazi Party (ASP) ya Zanzibar, imeongoza nchi kwa misingi ya sera na itikadi zake, ikihusishwa na mafanikio mbalimbali ikiwamo kudumisha amani na umoja wa kitaifa na kupanua huduma za kijamii kama elimu na afya.

Hata hivyo, chama hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto zinazoendana na mabadiliko ya nyakati, ikiwamo kuongezeka kwa ushindani wa kisiasa katika mfumo wa vyama vingi, kuimarika kwa uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao, pamoja na shinikizo la uwajibikaji na uwazi.

Changamoto hizo zimeilazimu CCM kufanya marekebisho ya mara kwa mara ya ndani, ikiwamo katiba ya chama ili kuendana na mahitaji na matarajio mapya ya jamii.

Kwa sasa, changamoto inayojitokeza kwa nguvu zaidi ni mabadiliko ya mtazamo wa kizazi cha kidijitali, kinachotegemea Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kinachouliza maswali kuhusu sera na uamuzi wa viongozi na kinachohitaji majibu ya haraka na yenye hoja.

Mitandao ya kijamii imeendelea kuwa jukwaa kuu la mijadala ya kisiasa kwa kizazi hicho, ambacho pia kinakabiliwa na changamoto ya ajira, hali inayolazimu chama kubadili mbinu zake za mawasiliano na ushawishi.

Katibu wa zamani wa Kamati Maalumu ya Itikadi na Uenezi Zanzibar, Catherine Nao anaamini CCM itaendelea kubaki madarakani endapo itazingatia malengo makuu yaliyoainishwa katika kiapo cha mwanachama.

 “Kusema ukweli daima, fitina kwangu mwiko, rushwa kwangu ni adui wa haki sitapokea wala kutoa. Tukiishi katika hizo ahadi za mwanachama, CCM itaendelea kubakia,”anasema Nao.

Anasema licha ya CCM kuwa na viongozi wengi katika ngazi mbalimbali, kuna wakati baadhi yao hushindwa kuishi kulingana na kiapo cha uanachama, hali inayosababisha mtikisiko ndani ya chama.

“CCM huwa tunajitathmini, tunatenga muda wa kukosoana na kusema hapa hapana. Kufanya hivyo, ndio kunatufanya tusonge mbele,” anasema Nao.  

Anasema kabla ya kuingia madarakani Rais hayati John Magufuli Novemba 5, 2015, CCM ilipitia kipindi kigumu, baadhi ya wanachama walikuwa na ugumu hata wa kuvaa sare za chama.

“Katika kipindi cha Magufuli, alirudisha imani ya wananchi na kukifanya chama kipendwe tena. Hata sasa, kama kuna jambo linajitokeza, tunakaa na kulirekebisha,” anasema Nao.

Anasema hakuna anayeichukia CCM bali chama hicho kinapitia hatua za ukuaji, akieleza matumaini yake ni kuona viongozi wakijirekebisha kutokana na hali hiyo.

“CCM haina shida na hakuna anayeweza kuiangusha. Kikubwa ni kuishi kiapo kwa uadilifu ili kuendelea kuwa na mvuto na kupendwa na wananchi,” anasema.

Akikumbuka kipindi cha uongozi wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Nao anasema aliwahi kueleza ndani ya vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa kuwa kuna wakati kitakuja kizazi kipya chenye mahitaji tofauti.

“Kikwete alituambia kitafika kizazi kitahitaji mabadiliko makubwa, uwazi na uwajibikaji na hakitaki propaganda. Kizazi hicho ni cha sasa,” anasema.

Anasema kama chama hakitasimama katika misingi ya uwajibikaji na uwazi, kitakumbana na changamoto, lakini akaeleza anaamini CCM inaweza kukabiliana na mabadiliko hayo endapo itaamua kufanya hivyo kwa vitendo.

“Jamii ya sasa inahitaji uwazi. CCM lazima iwajibike, si kwa ubishi wala ubabe, bali kwa dhamira,” anasema.

Nao anasema miongoni mwa mafanikio makubwa ya CCM ni kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, akieleza changamoto zilizokuwapo zimekuwa zikitatuliwa kwa majadiliano.

“Tanzania imeendelea kujitambua na kusikiliza mahitaji ya wananchi bila ubaguzi, tukiishi kwa sauti moja na lugha moja ya umoja,”anasema Nao.

Anasema licha ya changamoto za ndani na masilahi binafsi ya wanachama, ukubwa wa CCM ni silaha yake kuu na inaendelea kubeba ndoto za Watanzania wengi.

Nao anasema suala la uwazi katika uamuzi unaogusa masilahi ya wananchi, hususan kupitishwa kwa miswada ya Serikali, linahitaji kupewa uzito zaidi.

“Wabunge wanapaswa kuchakata miswada kwa umakini na kusimamia masilahi ya wananchi, na pale panapohitajika mabadiliko wawe tayari kuishauri Serikali,” anasema Nao.

Anasema kuna umuhimu wa chama na Serikali kuelewa mahitaji ya vijana, huku akiipongeza Serikali kwa kuanzisha wizara maalumu za vijana na kuwataka viongozi wake kuwashirikisha vijana kikamilifu katika uamuzi unaowahusu.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Harry Mwinuka anasema CCM ni chama chenye historia ya kipekee nchini kutokana na kuwa zao la muungano wa vyama viwili vilivyoongoza harakati za kudai uhuru wa Taifa.

Anasema tangu kupatikana kwa uhuru, CCM imebeba jukumu la kuongoza dola kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo na ustawi wa kijamii, kisiasa na kiuchumi.

“CCM ni chama cha kihistoria ambacho kimeongoza nchi kwa muda mrefu, kikilenga kutimiza matarajio ya wananchi na wanachama wake, ingawa si Watanzania wote ni wanachama wake,” anasema Mwinuka.

Anasema licha ya mabadiliko makubwa ya dunia, chama hicho bado kinategemewa na kila Mtanzania, hivyo kina wajibu wa kuwahudumia wananchi wote bila ubaguzi, sambamba na kubadili fikra na mtazamo wake ili kuendana na mazingira ya sasa.

Mwinuka anasema vyama vingi vya siasa barani Afrika, hususan vilivyoongozwa kwa muda mrefu, vimekuwa vikikumbwa na changamoto kubwa za kisiasa na baadhi yake kupoteza nguvu au kuondolewa madarakani kutokana na kushindwa kuendana na mabadiliko ya kimtazamo na kifalsafa.

“CCM ili iendelee kuwa imara katika zama hizi mpya, ni lazima ibadilike na kuangalia mahitaji ya sasa ya wananchi, pamoja na aina ya watu inaowaongoza, badala ya kujikita zaidi katika mitazamo ya zamani,” anasema.

Anasema mageuzi ni jambo lisiloepukika, hasa katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya teknolojia, hivyo chama hicho kinapaswa kuwa tayari kuyapokea na kuyasimamia kwa manufaa ya Taifa.

Mwinuka anasema kuna umuhimu wa CCM kuwakumbatia vijana, akieleza kundi kubwa la raia ni vijana wenye mahitaji na vipaumbele tofauti.

“Ni muhimu chama kikaelewa masilahi ya vijana, mambo wanayoyapa kipaumbele na namna ya kuishi nao kisiasa na kijamii,” anasema Mwinuka.

Anasema chama hicho kinapaswa kuwawezesha vijana wenye uwezo kushika nafasi za uongozi na kusukuma ajenda za chama ili kuendana na mahitaji ya sasa, sambamba na kuboresha huduma za jamii na kupunguza gharama za maisha kwa makundi mbalimbali.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa anadai kuwa CCM imeporomoka na haikubaliki katika mazingira ya sasa ya kisiasa, ili iweze kuishi na kushiriki uchaguzi kwa amani, ni lazima ibadili mtazamo na maono yake ya kiuendeshaji.

Hata hivyo, kuhusu madai ya kuporomoka Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM – Zanzibar, Hamis Mbeto anasema wote wanaokituhumu chama hawana hoja kwa sababu bado hawajafanya utafiti na kuja na majibu.

“CCM ni chama kinachoweza kusimamisha wagombea nchi nzima, unasemaje hakikubaliki, vyama vingine havina uwezo huo, wao wanafanya tafsiri za kimjini kwa kiholela,” anasema.

Mbeto anasema CCM ina uwakilishi kuanzia shina hadi Taifa, kusema inapoteza mvuto hiyo ni mihemko na watu kutaka kutengeneza habari chonganishi huku akidai kuwa, chama hicho kikifanya chaguzi zake za ndani dunia nzima inasimama.

Akiendelea kuizungumzia CCM, Ole Ngurumwa anasema chama hicho lazima kitambue dunia ya sasa ni tofauti na ile ya wakati ilipoanzishwa, akieleza kuwa dunia ya leo inahitaji ushindani wa haki, uwajibikaji, uelewa, wasomi na siasa za hoja badala ya propaganda.

“CCM lazima ifikirie kuwa tupo katika dunia nyingine tofauti na ile ya zamani. Ni dunia ya ushindani, uwajibikaji, uelewa na siasa za hoja,” anasema.

Anasema chama chochote kinachotaka kuongoza dola katika mazingira ya sasa, ni lazima kizingatie matakwa ya wananchi kwa nguvu zote na kuacha kuendesha mambo kwa mtazamo wa kulazimisha badala ya kusikiliza sauti za wananchi.

“Wananchi lazima wasikilizwe. Kila jambo linahitaji uwajibikaji. Kama wanataka mifumo mizuri ya uchaguzi, lazima wafanye yale Watanzania wanayohitaji, si yale wanayotaka wao,” anasema.

Ole Ngurumwa ambaye ni mwanasheria kitaaluma, anasema CCM haina budi kukubali kuwa, Tanzania inaendeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Hata hivyo,  Mbeto ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM – Zanzibar, anasema CCM imepita katika mawanda tofauti ndani ya wenyeviti tofauti na makatibu wake ambao wote wamejenga msingi thabiti inayoking’arisha.

“CCM ilizaliwa ili iweze kuzisimamia Serikali zote mbili na kuleta ustawi wa wananchi kwa pande zote, kwa kuondoa umaskini, malazi na ujinga kwa muda wote huo imekuwa ikijipambanua hivyo,” anasema Mbeto.

Anasema ndani ya miaka 49, Serikali ya CCM iko katika mikono salama na imekuwa ikitoa sera zinazokubalika na kutekelezeka.