Lindi. Wakati Serikali ikiendelea kusisitiza msimamo wake mkali juu ya uwajibikaji na uadilifu wa viongozi na watendaji wa umma, changamoto ya miundombinu mibovu ya barabara katika Jimbo la Mchinga, Manispaa ya Lindi, imeendelea kuibua maswali kuhusu ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya kijamii, hususan katika sekta ya elimu.
Hali hiyo inatajwa kukwamisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa matundu manane ya vyoo katika shule mbili za msingi za Mnyangara na Matapwa, zilizopo Kata ya Mipingo, jambo linalowaacha wanafunzi wakilazimika kutumia vyoo vichache, vilivyojaa na visivyo salama kiafya.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma hivi karibuni, kabla ya kuanza mjadala wa hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Novemba 14 mwaka jana wakati wa ufunguzi wa Bunge la 13, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, alisema hotuba hiyo imeweka msisitizo mkubwa juu ya uadilifu na uwajibikaji katika utumishi wa umma ili kuhakikisha rasilimali za Taifa zinawanufaisha wananchi moja kwa moja.
Hata hivyo, kwa wananchi wa Kata ya Mipingo, msisitizo huo bado unaonekana kuwa mbali na uhalisia wa maisha yao ya kila siku, hasa katika maeneo ya elimu ya msingi, ambako wanafunzi wanakabiliwa na mazingira duni ya kujifunzia yanayohatarisha afya na ustawi wao.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni baada ya kufika shuleni hapo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mnyangara, Bakari Meno, amesema kutokana na hali mbaya ya vyoo katika Shule ya Msingi Mnyangara, imewalazimu wananchi kuchukua hatua ya dharura kwa kuchangia fedha ili kuanza mradi huo kwa nguvu zao wenyewe.
Majengo ya shule ya msingi Matapwa kata ya Mipingo, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi inayokabiliwa na changamoto ya matundu ya choo na uhaba wa walimu
Amesema jumla ya Sh2.8 milioni zilitumika kuchimba shimo kubwa la vyoo. Kati ya fedha hizo, Sh2.5 milioni zilitolewa kwenye akiba ya kijiji, huku Sh300,000 zikikopwa kwa mwananchi mmoja kwa makubaliano ya kumlipa baadaye.
“Sisi kama Serikali ya kijiji tulikaa na wananchi tukakubaliana kuanza wenyewe kuchimba shimo, kwa sababu hali ilikuwa hairuhusu watoto wetu kuendelea kujisaidia kwenye vyoo vile vilivyojaa,” amesema Meno.
Amefafanua kuwa baada ya kukamilisha uchimbaji na kufunika shimo, kazi iliyobaki ilikuwa ni ujenzi wa mabanda, uwekaji wa bati na milango. Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ilitenga Sh4.4 milioni kwa ajili ya kazi hiyo na kuitangaza kupitia mfumo rasmi wa manunuzi wa Serikali.
Hata hivyo, juhudi hizo zinaelezwa kukwama baada ya mzabuni aliyekuwa amejitokeza kuomba kazi hiyo kushindwa kufika eneo la mradi kutokana na ubovu wa barabara.
Meno amesema mzabuni huyo amelazimika kurudi njiani wakati akienda kufanya tathmini ya eneo la mradi, baada ya gari lake kukwama kwenye barabara iliyojaa matope na makorongo.
“Kuanzia siku ile hakuna mzabuni mwingine aliyejitokeza. Wote wanaogopa ubovu wa barabara yetu,” amesema.
Baadhi ya majengo ya shule ya msingi Mnyangara iliyoko kata ya Mipingo Halmashauri ya manispaa ya Lindi ambayo wanafunzi wake wako hatarini kupata magonjwa ya kuambukiza kutokana na uhaba wa matundu ya choo unaowakabili kwa muda mrefu. Pembeni ni choo kilichojaa wanachoendelea kutumia kwa sasa
Kutokana na hali hiyo, mwenyekiti huyo ameomba Halmashauri ifikirie uwezekano wa kuzikabidhi fedha hizo Serikali ya kijiji ili isimamie mradi huo moja kwa moja bila kupitia mzabuni, kwa lengo la kuokoa hali ya wanafunzi 289 wanaotumia matundu manne ya vyoo yaliyojaa.
Mzabuni akiri kuiacha kazi
Mwananchi ilifanikiwa kuzungumza na mzabuni aliyekubaliwa awali kutekeleza mradi huo, Ibrahim Makanjira, juu ya hali hiyo, naye amethibitisha kuachana na kazi hiyo akieleza kuwa miundombinu mibovu ya barabara ndiyo chanzo kikuu.
“Ni kweli niliomba tenda ya kupeleka vifaa vya ujenzi wa vyoo hivyo, lakini siku ya kwanza niliyokwenda kukagua eneo la mradi ilinyesha mvua na sikufika. Barabara ni mbaya sana, ingeongeza gharama na kunikosesha faida,” amesema.
Alipoulizwa kama kiwango cha fedha kilichotengwa kwa kandarasi hiyo ndicho kilichomfanya aachane na kazi, amesema tatizo halikuwa fedha, bali ni mazingira magumu ya kufikisha vifaa.
Hata hivyo, amesema yuko tayari kuitekeleza kazi hiyo endapo barabara itarekebishwa.
Matapwa nako hali ni mbaya
Changamoto hiyo pia imeikumba Shule ya Msingi Matapwa, inayopakana na wilaya za Kilwa na Ruangwa mkoani Lindi.
Mkazi wa kijiji cha Matapwa, Omari Nangigi, amesema hali ya shule hiyo ni mbaya kwa vipengele vyote, ikiwamo uhaba mkubwa wa vyoo, walimu wachache na uchakavu wa majengo.
“Hii shule ina walimu wawili tu kuanzia chekechea hadi darasa la saba. Majengo yamechakaa, yana nyufa nyingi na ni hatari kwa watoto,” amesema.
Kwa maelezo yake, Nangigi ameiomba Serikali kuihamisha shule hiyo kutoka ilipo sasa na kuipeleka katika eneo la Mvumbani, ambalo ni salama zaidi kwa wanafunzi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matapwa, Anafi Kipoto, amekiri kuwepo kwa changamoto ya vyoo na majengo, akisema licha ya kuitangaza tenda hiyo mara mbili kupitia mfumo wa Halmashauri, hakuna mzabuni aliyejitokeza kutokana na ubovu wa barabara.
“Lakini kilio chetu kingine sambamba na hiki ni ubovu wa majengo ya shule. Hakuna kiongozi asiyejua kuwa tunahitaji kuhamishwa hapa ilipo shule kutokana na hali hii hatari kwa watoto wetu,” amesema Kipoto.
Mkazi mwingine, Esha Kilogwaga, amesema vyoo vya shule hiyo vimejaa na havifai kutumiwa, huku wanafunzi wakilazimika kuvumilia hali hiyo kwa kukosa mbadala.
“Vyoo vyote vimejaa, havifai hata kidogo. Watoto wanavumilia tu kwa sababu hakuna namna nyingine. Tatizo hili viongozi wote wanalijua, lakini kilio chetu hakisikilizwi,” amesema kwa masikitiko.
Alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mipingo, Paul Kambona, alikataa kuzungumza kuhusu changamoto hiyo, akidai si msemaji.
Diwani wa Kata hiyo, Mussa Mkulile, amesema tatizo la ukosefu wa vyoo salama limekuwepo kwa muda mrefu na sasa zaidi ya wanafunzi 400 wako katika hatari ya kiafya.
Amesema kinachokwamisha ujenzi wa mradi huo ni ugumu wa kupata mzabuni anayekidhi masharti ya mfumo wa manunuzi wa Manispaa, huku wengi wakihofia kukwama kwa magari yao kutokana na ubovu wa barabara, hasa kipindi cha masika.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Mchinga, Salma Kikwete, Katibu wake, Abdallah Mkokoi, amesema ofisi hiyo haikuwa na taarifa kuhusu changamoto ya vyoo katika shule hizo.
Amesema Jimbo la Mchinga lina shule za msingi 43, zikiwemo 12 kongwe zenye miundombinu chakavu.
Hata hivyo, amesema tayari zimeombewa fedha za ukarabati na awamu ya kwanza wamepokea Sh106 milioni kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Msingi Mchinga Moja.
Mkokoi amesema kama wangepata taarifa mapema kuhusu Shule ya Matapwa, wangetumia fedha za mfuko wa jimbo badala ya kujenga nyumba ya mganga wa zahanati ya Matapwa.
Mkurugenzi wa Manispaa asema nini?
Mwananchi pia ilizungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Juma Mnwele, ambaye amekiri kuwepo kwa uzembe katika kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.
“Tundu moja la choo tunajenga kwa Sh1.1 milioni na kwa matundu manane tumetoa Sh8.4 milioni. Fedha hizo zipo kwa walimu wakuu wa shule husika na Mtendaji wa Kata, lakini kama hadi sasa hazijatumika basi ni uzembe,” amesema.
Lakini amekiri ubovu wa barabara kuwa ni moja ya changamoto kubwa, akisema hatua za awali za kurekebisha barabara ya Mkwajuni hadi Matapwa na Mipingo zinatarajiwa kuanza hivi karibuni kwa kutumia grader.
Shimo la choo lenye jumla ya matundu manne lililojengwa kwa nguvu za wananchi wa kijiji cha Mnyangara kata ya Mipingo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi likikwama kujengewa kama lilivyokutwa na mpiga picha wetu
Ameongeza kuwa Manispaa inakabiliwa na upungufu wa walimu, lakini hatua za dharura zimechukuliwa kwa kupeleka angalau mwalimu mmoja wa ziada katika Shule ya Matapwa.
Changamoto pana ya maendeleo
Upatikanaji wa vyoo salama shuleni ni kigezo muhimu cha afya, ustawi na mazingira bora ya kujifunzia, hususan katika maeneo ya vijijini. Ingawa Serikali imekuwa ikisisitiza uboreshaji wa miundombinu ya elimu, utekelezaji wake bado unakumbwa na changamoto za urasimu, ucheleweshaji wa fedha na miundombinu duni ya usafiri.
Kwa Mkoa wa Lindi, hasa katika maeneo ya pembezoni kama Jimbo la Mchinga, hali ya barabara inaendelea kuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hali inayogusa moja kwa moja sekta nyeti kama elimu na afya, huku wanafunzi wakibaki kuwa waathirika wakuu.