Mvua kubwa yatarajiwa mikoa sita, wananchi wapewa tahadhari

Dar es Salaam. Takribani mikoa sita nchini inayopata mvua mara mbili kwa mwaka, ukiwamo Dar es Salaam, inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani wakati wa msimu wa Masika unaotarajiwa kuanza Machi.

Imetabiriwa na wataalamu wa hali ya hewa kuwa hali hiyo inaweza kuongeza hatari ya mafuriko na mlipuko wa magonjwa yatokanayo na maji.

Mikoa inayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani ni pamoja na Kagera na Geita na maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini ya Tanga na Morogoro.

Vilevile, hali kama hiyo inatarajiwa katika Mkoa wa Pwani na visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Januari 5, 2026 jijini Dar es Salaam kuhusu matarajio ya mvua za masika za Machi, Aprili na Mei, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Ladislaus Chang’a amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza Machi na hadi Mei au Juni, 2026.

“Vipindi vya unyevunyevu mwingi na mafuriko vinaweza kutokea na kuathiri ukuaji wa mazao hususani katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani,” amesema Dk Chang’a.

Amesema milipuko ya magonjwa, hasa yale yanayoenezwa na wadudu na maji, inatarajiwa na hiyo ni kutokana na uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Hivyo, amewataka wakazi wa maeneo ya mabondeni kuchukua tahadhari mapema ili kupunguza athari za mafuriko yanayoweza kutokea pamoja na hatari za kiafya.

Aidha, amewahimiza wakulima, wafugaji na maofisa ugani kuendelea kufuatilia taarifa sahihi za hali ya hewa na tabianchi kutoka kwa mamlaka za wilaya na kata ili kujiandaa vyema kukabiliana na changamoto za msimu.

Kwa upande wa Ukanda wa Ziwa Victoria, hususani mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu na Shinyanga, Dk Chang’a amesema mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani kidogo.

“Katika maeneo hayo, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Februari au mwanzoni mwa Machi na kumalizika mwezi Mei mwaka huu,” amesema mkurugenzi huyo.

Hata hivyo, ameonya kuwa baadhi ya maeneo nchini, yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, hali inayoweza kusababisha upungufu wa maji.

“Hali hii inaweza kuathiri uzalishaji wa mifugo na kusababisha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa maji,” amesema Dk Chang’a.
Kwa mikoa ya kaskazini ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mvua pia zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani kidogo, huku zikiaanza Machi na kuhitimishwa Mei.

Amewataka wananchi kufuatilia mara kwa mara taarifa rasmi na tahadhari za hali ya hewa ili kuongeza maandalizi na kupunguza athari za majanga yanayotokana na matukio makubwa ya hali ya hewa.

Kwa mujibu wa TMA, msimu wa mvua za Masika unahusisha Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (Arusha, Manyara na Kilimanjaro), Ukanda wa Pwani ya Kaskazini (kaskazini mwa Morogoro, Pwani ikiwemo Mafia, Dar es Salaam na Tanga), Visiwa vya Unguja na Pemba, Bonde la Ziwa Victoria (Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.