Serikali kuboresha mtandao wa simu intaneti eneo la Kariakoo

Dar es Salaam. Wakati wachuuzi katika soko la Kariakoo na wafanyabiashara wakipaza sauti zao kutaka maboresho ya mtandao ili waweze kufanya shughuli zao kikamilifu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema mitambo iliyopo haina uwezo wa kufikisha mtandao hasa katika maduka ya chini.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, imeelezwa kuwa tayari mazungumzo yameanza na watoa huduma kwa lengo la kuboresha huduma hizo za mawasiliano.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Februari 5, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa TCRA, Dk Jabir Bakari, katika mkutano unaofanyika kila mwaka wa anuani za makazi na maonyesho ya teknolojia ya huduma za posta.

Amesema kwa kutambua changamoto hiyo, tayari majadiliano yanafanyika na kampuni za mawasiliano yakilenga kuongeza uimara wa mtandao katika eneo la Kariakoo.

Dk Bakari amesema mitambo ya mawasiliano iliyopo katika eneo husika ina uwezo wa kutoa huduma za mawasiliano katika maeneo ya kawaida.

Hata hivyo, amesema uwezo huo haujawafikia ipasavyo watu wanaofanya shughuli zao katika maduka ya chini, tofauti na wale waliopo katika maeneo ya juu ambako majengo yalijengwa awali.

Amesema hali hiyo imesababisha wafanyabiashara na wananchi wanaoingia katika maduka ya chini kushindwa kupata mawimbi ya mtandao kwa kiwango walichotarajia, jambo ambalo halijitokezi kwa waliopo katika maeneo ya kawaida na ya juu.

“Ili kuondoa changamoto hiyo, ni lazima mawimbi ya mawasiliano yasogezwe karibu zaidi. Tayari kuna majadiliano yanayoendelea na watoa huduma za mawasiliano pamoja na kazi za kiufundi za kusogeza mitambo karibu na eneo husika, kwa kuwa mitambo ya awali haikuwekwa kwa lengo la kufikisha huduma katika maeneo ya chini,” amesema Dk Bakari.

Ametoa kauli hiyo wakati wafanyabiashara wa Kariakoo wakiendelea kupaza sauti zao kwa siku kadhaa kupitia mitandao ya kijamii, wakilalamikia ukosefu wa uthabiti wa mitandao ya mawasiliano, hali inayowakwamisha kuwasiliana na wateja wao kwa ufanisi.

Changamoto hiyo imekuwa ikijitokeza si katika huduma ya intaneti pekee, bali pia katika kupiga na kupokea simu kwa watu waliopo katika eneo hilo.

Akizungumza na Mwananchi leo, Samson Massawe, mfanyabiashara wa viatu eneo la Kariakoo, amesema kuchelewa kwa maboresho ya mtandao kumesababisha baadhi ya wafanyabiashara kupoteza wateja.

“Wamechelewa, lakini si jambo baya kwani biashara zinaendelea kufanyika. Maboresho haya yataongeza wigo wa biashara kwetu kwa sababu kuna wateja tulipoteza kutokana na kushindwa kujibu ujumbe kwa wakati au kutopatikana hewani,” amesema Massawe.

Kwa upande wake, Dk Jabir amesema mbali na uwepo wa mtandao wa mawasiliano ya uhakika, anuani za makazi ni nyenzo muhimu katika kukuza biashara za mtandaoni.

Amesema watahakikisha maeneo mapya na ambayo bado hayajafikiwa yanajadiliwa ili kubaini changamoto zilizochelewesha utekelezaji wa mfumo wa anuani za makazi, na hivyo kufanikisha mpango huo kama ilivyopangwa.

“Ninaamini shughuli hizi zinapofanyika kila mwaka hutoa fursa ya kutambua changamoto na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu,” amesema.

Dk Bakari ameongeza kuwa mikutano ya aina hiyo hutoa fursa ya kuona umuhimu wa kutafakari mchango wa mifumo ya anuani za uhakika katika utoaji wa huduma za kijamii, kuimarisha usalama, kusaidia wakazi na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya serikali.

“Mfumo wa kuaminika wa taarifa ni msingi muhimu wa mipango na usimamizi bora wa miji na vijijini. Mifumo hii ni nyenzo muhimu katika safari ya taifa kuelekea uchumi wa kisasa na miji inayotoa huduma kwa ufanisi,” amesema.

Amesema katika zama za mageuzi ya teknolojia, sekta ya posta inaendelea kubadilika kulingana na mahitaji ya soko na maendeleo ya kidijitali, hali inayohitaji mifumo madhubuti, huduma jumuishi na suluhisho endelevu za changamoto zinazojitokeza.

Kupitia utekelezaji wa mfumo wa kitaifa wa anuani za makazi na biashara, amesema Shirika la Posta limefanikiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa ufanisi wa shughuli zake, kupunguza gharama za uendeshaji na kuinua ubora wa huduma.

“Maboresho haya yanaonekana wazi hasa kutokana na ukuaji wa biashara mtandaoni na ongezeko la mahitaji ya huduma za kisasa. Mbali na jitihada za serikali, wadau mbalimbali wamekuwa na mchango mkubwa katika kuhimiza sera, kutoa msaada na kushirikiana katika matumizi ya mifumo ya kidijitali,” amesema Dk Bakari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Pan African Postal Union (PAPU), Dk Sifundo Moyo, amesema anuani za makazi ni nyenzo muhimu katika kuharakisha mageuzi ya kidijitali, hususan katika kuimarisha biashara mtandaoni na biashara ya ndani ya bara la Afrika chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

“Biashara mtandaoni ni injini muhimu ya maendeleo ya Afrika na fursa kubwa kwa huduma za posta. Mifumo madhubuti ya anuani hurahisisha manunuzi mtandaoni, huhakikisha uwasilishaji sahihi wa bidhaa na hujenga imani katika malipo ya kidijitali,” amesema.

Ameongeza kuwa katika muktadha wa Afrika, maendeleo hayo yanawawezesha wafanyabiashara wadogo kufikia masoko ya kimataifa, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na ajira.

Posta Masta Mkuu, Macrice Mbodo, amesema mifumo ya kitaifa ya anuani za makazi imechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa kidijitali, upangaji wa maendeleo na ongezeko la mapato ya serikali.

“Anwani za makazi na namba za posta zina mchango mkubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za serikali katika sekta muhimu kama afya, elimu, usalama na huduma za dharura,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Afrika Mashariki (EACO), Caroline Koech, amesema safari ya Tanzania katika utekelezaji wa mfumo wa anuani za makazi imetoa mafunzo muhimu kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Kupitia dhamira thabiti ya serikali na ushirikiano na wadau wa maendeleo, amesema Mpango wa Kitaifa wa Anwani za Makazi umefanikiwa kufikia zaidi ya asilimia 95 ya maeneo ya nchi na kuunganisha mamilioni ya anuani katika mfumo mmoja wa kitaifa unaojumuisha miji na vijiji.

“Mbinu ya utekelezaji iliyochanganya sera madhubuti, uratibu wa taasisi na matumizi ya teknolojia imeonesha kuwa mageuzi makubwa ya miundombinu ya kidijitali ya umma yanaweza kufanyika kwa mafanikio. Uzoefu huu unaifanya Tanzania kuwa rejea muhimu kwa nchi za Afrika Mashariki,” amesema.