Serikali yakata rufaa kupinga hukumu ya Jerry Silaa, wenzake kulipa Sh3 bilioni

Dar es Salaam. Serikali imekimbilia Mahakama ya Rufani kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, iliyomuamuru aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, na wadaiwa wengine, kumlipa mfanyabiashara Johansen Mahururu fidia ya Sh3.2 bilioni kwa kuvunjiwa ghorofa lake kinyume cha sheria.

Tayari Serikali imewasilisha notisi ya kusudio la kukata rufaa mahakamani hapo kupinga hukumu hiyo pamoja na tuzo (decree) yake.

Pia, imeiomba Mahakama Kuu kuwasilisha mwenendo wa kesi, hukumu iliyothibitishwa, vielelezo, na nyaraka nyingine muhimu kwa ajili ya mchakato wa rufaa.

Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi kufuatia kesi iliyofunguliwa na Mahururu kuhusiana na mgogoro wa umiliki wa kiwanja kilichopo Kitalu namba 484 (2196), Block H, Mbezi, Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam, kati yake na Naomi Kwayu.

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa  akisimamia ubomoaji wa nyumba ya makazi Februari 29, 2024. Picha na Maktaba



Katika kesi hiyo, Mahururu alidai kuwa nyumba aliyokuwa akiishi, pamoja na jengo lingine la hoteli ambalo ujenzi wake ulikuwa umefikia ghorofa ya tatu, vilivunjwa Februari 29 na Machi 4, 2024, kwa maelekezo na usimamizi wa Silaa, aliyekuwa waziri wakati huo.

Silaa alitoa uamuzi wa ubomoaji huo akidai Mahururu alikuwa mvamizi wa kiwanja hicho na kwamba mmiliki halali alikuwa Naomi.

Siku 10 baada ya ubomoaji huo, Naomi alipewa hati miliki ya kiwanja hicho kwa jina lingine la Fainess Dawson Kiwia, jina aliloomba litumike.

Kutokana na hatua hiyo, Mahururu, akiwakilishwa na Wakili Barnabas Luguwa, alifungua kesi dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, aliyekuwa waziri wa wizara hiyo.

Wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Kamishna wa Ardhi, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Naomi Kwayu (anayejulikana pia kama Fainess Dawson Kiwia), Juma Rajab Kapungu, aliyedaiwa kumuuzia Mahururu kiwanja hicho, pamoja na Msajili wa Hati.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, Mahakama Kuu, katika hukumu yake ya Desemba 30, 2025, iliyotolewa kwa wadaiwa Januari 21, 2026, ilimpa ushindi Mahururu. Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Sharmilla Sarwatt.

Katika uamuzi wake, Jaji Sarwatt alisema ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani vilithibitisha kuwa Mahururu ndiye mmiliki halali wa kiwanja hicho.

Alisema ubomoaji wa nyumba ya makazi ya Mahururu ulikuwa kinyume cha sheria, akabatilisha umiliki wa Naomi, na kumuagiza Msajili wa Hati kufanya marekebisho ya umiliki huo ili lisomeke jina la Mahururu.

Kutokana na uamuzi huo, Mahakama iliamuru Silaa, Manispaa ya Kinondoni, na Naomi kumlipa Mahururu fidia ya Sh3.18 bilioni ikiwa ni thamani ya nyumba ya makazi iliyobomolewa isivyo halali, pamoja na fidia ya madhara ya jumla ya Sh40 milioni.

Hata hivyo, Serikali imesema haijaridhika na hukumu hiyo na imechukua hatua za awali za kisheria kwa kuwasilisha notisi ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani ya Tanzania.

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa  akisimamia ubomoaji wa nyumba ya makazi Februari 29, 2024. Picha na Maktaba



“Tambua kuwa warufani, kwa kuwa hawajaridhika na hukumu yote na tuzo ya Mahakama Kuu katika kesi ya ardhi namba 32646 ya mwaka 2024 iliyotolewa Dar es Salaam Desemba 30, 2025, wanakusudia kukata rufaa Mahakama ya Rufani ya Tanzania dhidi ya uamuzi huo wote,” imeeleza sehemu ya notisi hiyo.

Katika notisi hiyo, licha ya Silaa kushtakiwa kwa jina lake binafsi na kubebeshwa wajibu wa kulipa fidia, Serikali imemjumuisha kama mmoja wa warufani sita.

Warufani hao ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, Kamishna wa Ardhi, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na Msajili wa Hati.

Wajibu rufaa ni Johansen Mahururu, Naomi Raymond Kwayu (ambaye umiliki wake ulibatilishwa na mahakama), pamoja na Juma Rajab Kapungu.