Teknolojia ya nyuklia yatumika kuchagiza maendeleo ya afya, kilimo, nishati

Arusha. Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki nchini (TAEC), Profesa Najat Kassim Mohammed amesema kupitia taasisi hiyo wameendeleza matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika maendeleo ya sekta ya kilimo, afya na uhifadhi wa chakula nchini.

Akizungumza katika ofisi za taasisi hiyo jijini hapa Februari 4, 2026 wakati wa ziara ya viongozi wa Shirika la Wakala wa Kimataifa la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) waliotembelea taasisi hiyo kujionea utekelezaji wa miradi wanayoifadhili.

Profesa Najat amesema TAEC inasimamia miradi mbalimbali ya kimkakati inayolenga kutatua changamoto na kuongeza tija katika jamii kwa kushirikina na wadau wa maendeleo wakiwemo IAEA.

“Wakala wa IAEA, tunashirikiana nao kwenye miradi ya kimkakati hapa nchini ambayo ipo chini ya TAEC na taasisi zingine, tunao mradi wa kuzalisha mbegu bora ambao upo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI),” amesema Profesa Najat.

Ametaja mradi mingine ni ujenzi wa maabara ya kisasa uliopo Zanzibar kwa ajili ya tafiti za wanyama, ujenzi wa mashine ya Radiolojia kwa ajili kudhibiti vyakula visiharibike mradi ambao upo katika hatua za ujenzi jijini Dar es Salaam.

“Mradi mwingine ambao ni mkubwa zaidi ni ule ambao Tanzania inataka kuongeza vituo vya matibabu na uchunguzi wa saratani, kulikua na vituo vya serikali viwili ambavyo ni Ocean Road na Bugando, lakini sasa tunaongeza vituo kuwa sita ikiwemo KCMC, Benjamin Mkapa, kituo cha Mbeya na kituo cha Mnazi Mmoja Zanzibar.

“Ugeni huu umekuja mbali ya kuimarisha mahusiano na wakala wetu lakini pia kupitia miradi mbalimbali wanayoifadhili ambayo inatuletea manufaa makubwa pindi ikikamilika na kuanza kutekelezwa kikamilifu,” amesema Profesa Najat.

Katika hatua nyingine, amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeanzisha mazungumzo ya Tanzania kuelekea kuzalisha umeme kwa njia ya nyuklia na ugeni huo uliongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kiufundi kwa Afrika wa IAEA, Gashaw Wolde na Ofisa Msimamizi wa Programu za Afrika, Azza Kashan wamefurahia mpango huo.