MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mikoa ya pwani ya kaskazini, baadhi ya maeneo ya magharibi mwa Ukanda wa Ziwa Victoria pamoja kaskazini inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani katika msimu wa mvua za masika(Machi -Mei), 2026.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema hayo leo, Februari 5, 2026 wakati akitangaza utabiri kwa waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa mvua na athari zinazoweza kujitokeza katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
“Mvua za masika zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya Februari na wiki ya kwanza ya Machi 2026 katika Ukanda wa Ziwa Victoria, wiki ya kwanza na ya pili ya Machi katika maeneo ya pwani ya kaskazini, na wiki ya pili hadi ya tatu ya Machi katika nyanda za juu kaskazini mashariki,”amesema Chang’a
Ameongeza,”Mvua hizo zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya nne ya Mei na wiki ya kwanza ya Juni mwaka huu,huku ongezeko la mvua likitarajiwa zaidi mwezi Aprili,
Amesema,TMA imetabiri kuwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kagera na Geita, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma pamoja na maeneo mengi ya pwani ya kaskazini ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Pwani, kaskazini mwa Morogoro na visiwa vya Unguja na Pemba.
Aidha,amesisitiza kuwa mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika nyanda za juu kaskazini mashariki (Arusha, Manyara na Kilimanjaro) na baadhi ya maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu.
Akieleza athari zinazoweza kujitokeza endapo, Chang’a amesema vipindi vya mvua kubwa vinaweza kusababisha mafuriko, kutuama kwa maji na uharibifu wa miundombinu katika baadhi ya maeneo, huku maeneo yatakayopata mvua chache yakikabiliwa na upungufu wa unyevu wa udongo na kushuka kwa kina cha maji katika mito na mabwawa.
“Msimu wa mvua za Masika ni mahsusi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mkoa wa Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Viktoria (mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara), pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma,” amesema Dkt. Chang’a.
Aidha Mamlaka imewaasa wadau wa sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, afya, nishati, maji, ujenzi na usafirishaji kuzingatia utabiri huo pamoja na taarifa za hali ya hewa za kila siku na tahadhari rasmi zinazotolewa na TMA ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.
Chang’a amekumbusha kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019, ni kosa kisheria kusambaza utabiri wa hali ya hewa kutoka vyanzo visivyo rasmi, na kuvitaka vyombo vya habari kuzingatia taarifa rasmi za TMA katika kuhabarisha umma.