UWT Wilaya ya Ilala Yaadhimisha Miaka 49 ya CCM kwa Kutoa Msaada kwa Watoto Yatima

Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Ilala, chini ya Mwenyekiti wake Ndg. Neema Kiusa, imeadhimisha miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutembelea Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Upendo Orphanage Centre, kilichopo Buguruni Kisiwani (Ghana), jijini Dar es Salaam.

Katika maadhimisho hayo, UWT Wilaya ya Ilala ilitoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho, ikiwa ni sehemu ya kuonesha mshikamano, upendo na uwajibikaji wa kijamii kwa makundi yenye mahitaji maalumu.

Aidha, watoto wa Kituo cha Upendo Orphanage Centre kwa kushirikiana na wanachama wa UWT Wilaya ya Ilala walifanya dua maalum kuliombea Taifa letu, pamoja na kumuombea Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili aendelee kuliongoza Taifa kwa hekima na busara.

Kwa pamoja waliomba amani, umoja na mshikamano wa Taifa, wakisisitiza umuhimu wa kuilinda na kudumisha amani ya nchi yetu.