Vikundi 130 Makambako vyakopeshwa Sh1 bilioni

Njombe. Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe imetoa mikopo zaidi ya Sh1.042 bilioni kwenye vikundi 130 ambavyo vinasisitizwa kurejesha kwa wakati mikopo hiyo kwani siyo zawadi.

Kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na halmashauri ni jumla ya mikopo katika vikundi kuanzia Aprili 2024 mpaka sasa.

Hayo yamebainishwa leo Februari 5, 2026 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Salum Mlumbe wakati akikabidhi mkopo wa Sh216.79 milioni kwenye vikundi 19 vya wanawake na vijana katika kata ya Lyamkena iliyopo Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe.

Amesema kati ya vikundi 130, vikundi 79 vya wanawake vimenufaika na mkopo huo wa asilimia 10 unaotokana na mapato ya ndani huku vikundi vya vijana vikiwa 39 na vikundi vya watu wenye ulemavu vikiwa 12.

Amesema wanufaika wa mkopo huo wanatakiwa kutambua kuwa hawajapewa mkopo huo kama zawadi, bali wanatakiwa kutumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili waweze kurejesha kwa wakati.

“Waombaji walikuwa wengi zaidi lakini nyinyi mmepata huo mkopo sasa niwaombe ndugu zangu mtumie kwa malengo yaliyokusudiwa kwa sababu hiyo siyo zawadi,” amesema Mlumbe.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Robert Shejamabu amewataka wanufaika wa mkopo huo kurejesha mikopo kwa wakati ili wengine wapate mikopo hiyo isiyo na riba.

“Mkishapokea fedha hizo zirudi kwa wakati vinginevyo kuna suala la mahakamani ingawa kuna wengine wanasema hizi fedha ni za serikali nikishapewa napotelea kule,” amesema Shejamabu.

Mratibu wa Mikopo Halmashauri ya Mji wa Makambako, Kassim Mamba amesema wananchi ambao wameunda vikundi na hawajafanikiwa kupata, wawe wavumilivu kwa kuwa kila kikundi kitafikiwa.

“Tunashukuru mikopo hii imewasaidia kuinua hali za kiuchumi na kuondoa hali ya utegemezi na kushiriki katika hali za kifedha,” amesema Mamba.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Mji wa Makambako, Daria Nyangoma amesema vikundi 19 ambavyo vimepatiwa mikopo ya Sh216.79 milioni, wanawake wenye vikundi tisa wamepata Sh111. 79 milioni na vikundi 10 vya vijana wakipata Sh105 milioni.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwezesha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani iliyoboreshwa ambapo kila Mtanzania mwenye sifa na vigezo, anaweza kupata mikopo isiyo na riba,” amesema Nyangoma.

Kwa upande wake, baadhi ya wanufaika wa mkopo huo akiwemo Chesko Makweta, amesema mkopo huo umekuwa na tija kwao kwani unaenda kukuza uchumi wao kupitia shughuli za kilimo, ufugaji na biashara ambazo wanazifanya.

“Napenda kuwaambia vijana wenzangu waunde vikundi na kuchukua miradi mbalimbali ili kuepukana na mambo ya kuchoma na matairi barabarani,” amesema Makweta.