KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Mzambia Joshua Mutale ‘Budo’, amekamilisha uhamisho wa kujiunga na Al Adalah Club ya Saudi Arabia, baada ya mabwanyenye hao wanaoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kuonyesha nia ya kumuhitaji mchezaji huyo kwa mkopo.
Nyota huyo aliyejiunga na Simba Julai 1, 2024, akitokea Power Dynamos ya kwao Zambia, ni miongoni mwa wachezaji wa timu hiyo waliotolewa kwa mkopo dirisha dogo la Januari 2026, ili kupisha wengine kwa ajili ya kuongezea nguvu kikosini humo.
Mwanaspoti liliripoti tangu wiki mbili zilizopita kuhusiana na mchezaji huyo kujiunga na Al Adalah Club kwa mkopo, baada ya dili lake la kwenda Kenya Police FC ya Kenya kuungana na nyota mwenzake, Awesu Awesu aliyetimkia huko kutokamilika.
Hata hivyo, baada ya dili la nyota huyo kwenda Kenya kuonekana gumu, Al Adalah Club iliyoanzishwa mwaka 1984, ikiwa na miaka 42, ilionyesha nia ya kumuhitaji ili kuitumikia kwa mkopo, huku kukiwa na kipengele cha kumnunua moja kwa moja.
Budo ambaye tayari amekamilisha uhamisho huo wa miezi sita, mkataba wake na Simba unamalizika mwishoni mwa msimu huu, huku mwanaspoti likitambua mabosi wa kikosi hicho hawana mpango tena wa kumuongezea mwingine pindi wa sasa utakapomalizika.
Katika Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia msimu huu, Al Adalah Club inashika nafasi ya 15 na pointi 15, kati ya timu 18 zinazoshiriki, baada ya kikosi hicho kushinda mechi tatu tu, sare sita na kupoteza 11, kikifunga mabao 26 na kuruhusu 43.