Wasira afunguka rushwa, amani, haki

Bunda. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Watanzania kuungana na kupambana na tatizo la rushwa na ufisadi nchini, kwa maelezo kuwa matatizo hayo bado yapo na ni miongoni mwa changamoto zinazorudisha nyuma juhudi za Serikali katika kuwaletea watanzania maendeleo.

Wito huo umetolewa mjini Bunda leo Alhamisi Februari 5, 2026 na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira kwenye maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa chama hicho.

Wasira amesema Serikali pekee

haiwezi kumaliza changamoto hiyo isipokuwa kwa ushirikiano baina ya wananchi na wadau wengine vikiwamo vyama vya siasa.

Kwa maana nyingine, Wasira amesema hilo ni jukumu la kila mtanzania kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika mapambano hayo.

Amesema watanzania pia wanapaswa kutambua kuwa chama hicho kiko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi kwa maelezo kuwa vitendo hivyo ni dhuluma na vina wadhulumu wananchi maendeleo ya nchi yao.

Amesema hakuna sababu ya wananchi kuendelea kulalamika juu ya rushwa, badala yake wanatakiwa kutoa taarifa kwenye vyombo husika pale wanapobaini kusudi hatua ziweze kuchukuliwa ili kupata suluhisho la kudumu katika masuala hayo.

Amesema chama hicho pia kinawaunga mkono wabunge ambao hivi karibuni walitoa michango yao bungeni kuhusu watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, huku akiwatoa hofu watanzania kuwa kitendo cha baadhi ya wabunge hao kuitwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hakikuwa na nia mbaya, bali taasisi hiyo inataka  kupata taarifa za kina kuhusu madai hayo.

“Kuna watu wameanza oooh ona Shabiby amesema kuhusu rushwa tayari ameitwa na Takukuru, naomba niwaambie Watanzania kuwa Takukuru hawakuwa na nia mbaya. isipokuwa walitaka kupata taarifa vizuri ili wafanyie kazi, niwaombe nanyi pia mtoe taarifa pale mnapokutana  na changamoto hizo,” amesema makamu mwenyekiti huyo.

Amesema hakuna sababu ya watanzania kuendelea kulalamika juu ya uwepo wa vitendo vya rushwa isipokuwa wanatakiwa kuvichukia na kuungana na Serikali kupambana navyo kama CCM inavyofanya kupitia ilani yake ya uchaguzi pamoja na katiba yake.

“Kuna mtu unaweza ukalazimika kutoa rushwa ili kujiokoa sasa ukitoa usiishie hapo, nenda kwenye mamlaka husika toa taarifa ili hatua zichukuliwe kumbukeni hibi vitendo vya rushwa ni siri kati ya pande mbili yaani anayeomba na anayetoa kwahiyo ni vigumu mamlaka husika kujua kinachoendelea sirini,” amesema Wasira.

Amesema rushwa ni tatizo ndani ya nchi na ni miongoni mwa vitendo vya dhuluma  ambavyo chama hicho kinapambana navyo na hakiko tayari kuona haki ya wananchi inadhulumiwa na chombo chochote, kikundi cha watu ama mtu mmoja mmoja.

Kuhusu haki, Wasira amesema haki na amani ni kama yai na kuku kwa maelezo kuwa, kuku akifa basi hakuna mayai na mayai pia yakipasuka hakuna kuku, hivyo msingi wa haki ni amani.

Amesema katika mazingira ya fujo na ukosefu wa amani, haki haiwezi kupatikana na kwa yule anayetaka kuona ushahidi basi aende Gaza ama nchi ya kidemokarisia ya Kongo.

“Anayebisha aende Gaza au Kongo akaone namna ambavyo vita imeua watu, haki imepotea watu wanakufa, hapo ndipo utakapoelewa mahusiano yaliyopo kati ya haki na amani” amesema.

Amesema chama chake kimeahidi kulinda amani ya nchi kwa sababu kinaamini penye amani lazima patakuwa na haki, hivyo kuwataka watanzania kuendelea kukiunga mkono ili amani iendelee kudumu nchini.

Amesema hakuna mbadala wa chama hicho hapa nchini kwa sasa katika kulinda na kusimamia amani na haki kam kinavyofanya CCM.

Wasira amesema kauli mbiu ya maadhimisho ya chama hicho kwa mwaka huu ni ‘Tumechagua amani na umoja kwa maendeleo yetu’.

Amesema kauli mbiu hiyo ni mwendelezo wa dhamira ya chama hicho tangu kilipoanzishwa miaka 49 iliyopita ya kuwaletea maendeleo watanzania.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi amesema chama chake kinaendelea kuwatumikia wananchi hasa katika kusimamia ilani ya uchaguzi ya 2025/30.

Amesema CCM ni kikongwe ndani ya Afrika na dunia kwa ujumla, na mbali na kusimamia utekelezaji wa ilani yao hivi sasa, pia wanashughulika na kujenga umoja ndani ya chama hicho.

Wakizungumza baada hotuba ya Wasira, baadhi ya wakazi wa Bunda wamekipongeza chama hicho kwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa sambamba na kusimamia amani ya nchi huku wakikitaka kionyesha kwa vitendo dhamira hiyo.

“Yapo madai mengi sana yanatolewa hasa nyakati za uchaguzi, tukianza na mchakato wa uchaguzi ndani ya chama kuhusu rushwa, naomba kuanzia sasa CCM waonyeshe kwa vitendo namna wanavyochukia na kupambana na rushwa kwa kuwachukulia hatua wanaojihusisha na rushwa kwenye uchaguzi,” amesema Jerome Newland

Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Machera Obadia amesema watanzania wanataka maendeleo na maendeleo hayo yatapatikana katika mazingira yenye amani na yasiyo na rushwa.