Wizara yatangaza kuwapiga jeki wabunifu zana za kilimo

Dar es Sakaam. Wizara ya Kilimo imesema inawatambua na inawapa kipaumbele wabunifu wa zana za kilimo nchini huku ikisema lengo ni kurahisisha shughuli hiyo muhimu ya kiuchumi.

Wabunifu hao wanaotengeneza zana kama matrekta, mashine za umwagiliaji, mashine za kuvunia mazao, mashine za kupandia mashine za kuongeza thamani, majembe ya kukokotwa na ng’ombe wametakiwa kutengeneza zana hizo wakizingatia ubora.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Februari 5, 2026 na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Athumani Kilundumya wakati akifunga mkutano wa Kwanza wa Kikanda wa Afrika kuhusu Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo (ACSAM) jijini Dar es Salaam kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).

Kilundumya amesema katika kutambua mchango wao wameandaa shindano la ubunifulitakalofanyika sikukuu ya wakulima maarufu Nanenane ambapo mshindi watampatia zawadi.

Hata hivyo, kauli hiyo inakuja wakati Serikali kupitia Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ikizindua mpango wa taifa wa zana za kilimo awamu ya pili wa miaka kumi kuanzia 2025/26 hadi 2036. 

“Kwanza tunaidadi ya watengenezaji wadogo tumeshawatambua na siku ya nanenane tumeandaa eneo lao maalumu waweze kushindana,” amesema Mhandisi Kilundumya.

Amesema lengo la Serikali ni kuanzisha vituo maalumu vya zana za kilimo vipatavyo 1000 nchi nzima. Amesema yote hayo yanafanyika ili asiwepo mtanzania anayelima mwenye atakayekuwa na kipati cha chini.

Naye Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Mwakilishi wa Kikanda ya Afrika, Abebe Gabriel amesema katika mkutano huo mzima wameona kwamba Afrika lazima ibadilike katika suala la mitambo, na sio tu kuhusu mashine lakini pia mifumo inayofanya kazi inajumuisha ubunifu wa kidijitali.

“Mkutano huu umetoa mwelekeo juu ya suala la kilimo cha mashine za kisasa kwa ujumla. Jukumu letu ni kuufanya ubunifu huu kuwa halisi katika kufanya mabadiliko kwa jumuiya zetu,” amesema.

Mkutano huo wa ACSAM umeanzishwa kama jukwaa la kipekee la kubadilishana mbinu bora, kukuza ushirikiano wa kikanda, na kuhimiza matumizi endelevu ya zana za kilimo zinazochangia kuongeza tija na kipato kwa wakulima barani Afrika.