KOCHA wa KMC, Abdallah Mohamed ‘Baresi’, baada ya kupata ushindi wa kwanza na timu hiyo tangu ajiunge nayo, Desemba 30, 2025, akichukua nafasi ya Mbrazil Marcio Maximo, amesema malengo yaliyopo ni kutengeneza safu bora ya ushambuliaji.
Kauli ya kocha huyo inajiri baada ya kushinda bao 1-0, katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa iliyopigwa Februari 3, 2026 kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, ukiwa ni ushindi wake wa kwanza msimu huu, baada ya kuchapwa mbili na kutoa sare mmoja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Baresi amesema ushindi huo umeamsha morali baada ya kipindi kigumu cha kutopata matokeo mazuri, lakini anapambana kuhakikisha anatengeneza safu bora ya ushambuliaji kwa kuwaunganisha wapya na waliokuwa na timu tangu mwanzo.
“Tumepitia kipindi kigumu sana ila siku zote tuliamini tutapata matokeo mazuri, kwa sasa kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kuendeleza mwenendo mzuri, huku tukitengeneza balansi ya kujilinda na ushambuliaji tuliyoongeza watu,” amesema Baresi.
Baresi amesema kuongezeka kwa aliyekuwa mshambuliaji wa Transit Camp, Adam Uledi aliyefunga mabao 11 na kikosi hicho na uwepo wa Eliuter Mpepo aliyetoka Singida Black Stars, umeongeza motisha zaidi na ushindani katika eneo la ushambuliaji.
“Jambo kubwa ni muunganiko mzuri kati yao wa kiuchezaji kwa kushirikiana na Daruweshi Saliboko aliyekuwapo tangu mwanzo, naamini mfumo huo utakuwa mzuri kwa sababu wote ni washambuliaji wazuri, ingawa muda ni mchache sana,” amesema Baresi.
Kocha huyo aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwamo JKT Tanzania na Tanzania Prisons zote za Tanzania Bara, na Mlandege ya Zanzibar, amejiunga na KMC baada ya kuachana na Zimamoto, huku akikabiliwa na mtihani wa kuinusuru isishuke daraja.
KMC msimu huu imecheza mechi 13 za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo imeshinda mbili tu, sare mbili na kupoteza tisa, ikifunga mabao manne na kuruhusu 19, huku kikosi hicho kikiendelea kuburuza mkia kikikusanya pointi nane.