Chalamila aagiza hatua za haraka kukabili msongamano wa wanafunzi

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amemuagiza Katibu Tawala na Ofisa Elimu wa mkoa huo kuchukua hatua za haraka kukabiliana na msongamano wa wanafunzi katika shule za umma, unaotarajiwa kuongezeka kufuatia kuanza kwa utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023.

Chalamila amesema utekelezaji wa sera hiyo unamaanisha kuwa wanafunzi waliokuwa darasa la tano mwaka huu, watahitimu darasa la sita, huku waliopo darasa la tita wakihitimu darasa la saba, hali itakayofanya mwaka 2028 kidato cha kwanza kupokea wanafunzi waliomaliza darasa la sita na la saba kwa wakati mmoja.

Mkuu huyo wa mkoa ametoa maagizo hayo leo Ijumaa, Februari 6, 2026, wakati akizungumza na maofisa elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam na walimu wa shule za msingi na sekondari.

“Taarifa ya Ofisa Elimu wa Mkoa inaonyesha kuwa shule 420 za Serikali zina jumla ya wanafunzi 739,771, huku idadi ya wanafunzi wa shule za Serikali na binafsi kwa pamoja ikifikia 855,000. Pia kuna shule za Serikali ambazo ndani yake kuna shule tatu au nne,” amesema Chalamila.

Amesema mkoa huo hauna budi kukabiliana na hali hiyo kwa pamoja badala ya kulalamikia mfumo au kuwanyima wanafunzi nafasi ya elimu.

“Swali si kulalamikia mfumo wala kukataa wanafunzi. Jibu ni hapana. Ni lazima tukae kama timu na kutatua kwa haraka sana tatizo hili la msongamano wa wanafunzi, ambalo lina tija kwa Serikali ya Tanzania,” amesema.

Chalamila amesema tayari amezungumza na Ofisa Elimu wa Mkoa pamoja na Katibu Tawala kuhusu mfumo wa sasa unaoelekeza wanafunzi wa darasa la tano kuhitimu darasa la sita na kukutana na waliomaliza darasa la saba katika udahili wa kidato cha kwanza mwaka 2028.

Kutokana na hilo, amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuhakikisha mkoa unajiandaa mapema kwa kuimarisha mifumo ya ujenzi wa shule za ghorofa ili kupunguza msongamano uliopo.

“Tumuandikie barua rasmi Katibu Mkuu wa Tamisemi kuhusu mgawanyo wa fedha na maelekezo yanayotoka wizara kwenda kwenye majiji. Badala ya kupoteza muda kuomba vibali vya kubadili matumizi ya fedha, ni bora maelekezo yatoke huko kuruhusu ujenzi wa madarasa kwa mfumo wa ghorofa badala ya mfumo wa msambao,” amesema.

Ameongeza kuwa utaratibu huo utawezesha mawasiliano na uelewa wa pamoja kati ya Tamisemi, mkoa na halmashauri zake, ili maelekezo yatolewayo yaendane na mazingira ya kila mkoa.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Gift Kyando amesema wingi wa wanafunzi ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili sekta ya elimu, akitolea mfano Shule ya Msingi Juhudi yenye zaidi ya wanafunzi 6,000, idadi ambayo ingeweza kuunda shule tatu tofauti.

Kyando amesema changamoto nyingine ni upatikanaji wa chakula shuleni pamoja na usafiri kwa wanafunzi na walimu.

Akizungumzia juhudi za Serikali katika kuwawezesha walimu, Katibu Msaidizi kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Wilaya ya Ilala, Subira Mwakibete, amesema walimu 3,612 wamepandishwa madaraja.

Ameongeza kuwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee, walimu 978 wameajiriwa, huku walimu 78 wakifukuzwa kazi kwa utovu wa nidhamu, wengi wao wakihusishwa na kughushi vyeti.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhinte amewapongeza walimu kwa kujitolea kwao kazini licha ya changamoto zinazowakabili, na kuahidi kuanzishwa kwa tuzo maalumu kwa shule zitakazofanya vizuri kitaaluma.

Katika hatua hiyo, mkuu wa mkoa amemuagiza katibu tawala kuhakikisha kunakuwa na uratibu wa kutambua shule zitakazostahili tuzo hizo ifikapo Aprili mwaka huu, ili zipatiwe tuzo na zawadi.