Kahama. Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imevunja mkataba kati yake na mkandarasi Sichuwan Road and Bridge Constraction Limited, aliyekuwa anajenga mradi wa barabara na madaraja yaliyokuwa chini ya Mradi wa Uboreshaji Miji nchini (Tactic).
Mkataba wa utekelezaji wa mradi huo uliofadhiliwa na Benki ya Dunia, ulisainiwa Novemba mwaka 2023 na ulitakiwa kukamilika na kukabidhiwa kwa manispaa Februari mwaka jana, lakini hadi unavunjwa ni kilomita 1.7 tu ndizo zilizokuwa zimekamilika kati ya kilomita 15.2 zilizopaswa.
Uamuzi wa kuvunjwa kwa mkataba huo, umetangazwa leo, Ijumaa Februari 6, 2026 na mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Masudi Kibetu katika kikao cha baraza la madiwani.
Amesema licha ya mkandarasi kuongezewa muda mara tatu kwa maana wa kawaida na ule wa adhabu hadi kufikia Januari 15, 2026 bado maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo hayakuridhisha.
“Kwenye mkataba wa barabara alizokuwa anatengeneza ni kilomita 15.2, mpaka Februari 15, 2025 alikuwa ametengeneza kilomita 1.7 za lami. Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Januari 19, 2026 tumevunja rasmi mkataba na mkandarasi Sichuwan Road and Bridge Constraction Limited baada ya kutoridhishwa na kasi ya utendaji wake,” amesema.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga Masudi Kibetu akizungumza kwenye baraza la madiwani leo Februari 6,2026.
Awali, Diwani wa Viti Maalumu Manispaa ya Kahama, Herieth Makaga alihoji hatua zinazochukuliwa na halmashauri kuwanusuru wananchi wanaotaabishwa na ubovu wa miundombinu ya barabara hizo.
Mkazi wa Kahama, Avitus Mwaipopo ameiomba halmashauri kuwa makini inapotoa zabuni ili isipate tena wazabuni wasio na sifa na wasiomudu kutekeleza miradi.
“Hapa halmashauri yetu ina funzo, kwa sababu sidhani kama walimjua vizuri mtu wanayemkabidhi kazi. Wakati mwingine wanapotangaza uwepo umakini na uzalendo ili watusaidie sisi wananchi kukuza uchumi wetu badala ya kuturudisha nyuma,” amesema.
Baadhi ya madiwani wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wakiwa ukumbini
Januari 15, 2026 Serikali iliahidi kumchukulia hatua za kimkataba mkandarasi huyo baada ya timu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Miko na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutembelea na kukagua miundombinu hiyo.