Miongoni mwa wizara nyingi ambazo Seri-kali yetu hii imeunda ili kuisaidia nchi kupiga hatua mbele fasta ni hizi wizara tatu zinazoonekana ni muhimu sana kwa uendelevu wa Taifa letu za watoto, vijana na wanawake.
Ni kweli wizara hizi ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi, lakini kuwa muhimu zaidi kuliko hata ya walioijenga na kuilinda nchi hii kwa jasho na damu yao kwa miaka 65, wastaafu hawana wizara yao maalumu ya japo kupigia kelele mitihani wanayopata uzeeni, kuuna jambo dhahiri haliko sawa.
Tukumbuke kuwa Mungu wetu mwema alitoa maagizo muhimu ya kwamba “tuzaane, tuongezeke na tukaijaze nchi”. Mstaafu asiyekuwa sasa, na hata asiye na wizara maalumu, anaamini kuwa ameifanya kazi hii njema ya “kuijaza” nchi kwa watoto na vijana, akishirikiana na huyu “Eva” aliyetolewa kwenye ubavu wake wakati akiwa ametia dozi!
Inawezekana kuwa kwa hapa kwetu, huku mstaafu hutia dozi kwake wakati “Eva” “anatengenezwa” kutoka mbavu zake, kumemponza, ndiyo maana miaka 64 baada ya Uhuru, mwanamke, mtoto wake na kijana wake wanapata wizara maalumu za kuwajali masilahi yao, huku mstaafu aliyeijenga nchi kwa jasho na damu yake wizara itakayomhusu ataishikia kwenye bomba tu!
Mstaafu huishia kujiuliza, hivi miaka 64 baada ya Uhuru huyu mwanamke anajengewa au kufanyiwa nini kisichokamilika mpaka leo anapewa wizara maalumu kwa ajili yake, lakini mstaafu aliyeijenga nchi anaishia kuwa ‘ rafiki mkuu’ wa Kinondoni tu !
Humshangaza sana mstaafu kwamba mpaka leo hakuna mstaafu hata mmoja aliyepewa nafasi maalumu za kuingia bungeni ili wakapanue midomo yao kuhusu wastaafu wenzao walioijenga na kuliinda nchi, pamoja na sasa wanataabika pamoja kwa pensheni ya shilingi laki moja elfu hamsini kwa mwezi! Nikumbushe tu hapa kuwa domo la huyu mstaafu wenu ni pana la kutosha!
Mstaafu anajua kwamba kweli sasa hata vyeo ni vya kurithishana, na hata watoto wa waheshimiwa sasa wanakuwa waheshimiwa wa watoto wengine, lakini kwa mstaafu hakuna kurithishana, na kamwe mtoto wa mstaafu hawi mheshimiwa wa wastaafu wengine! Hakuna anayetaka kurithi tabu za wastaafu, labda kama anataka kurithi njaa tu!
Ndiyo maana, pamoja na kukatwa mishahara kwa miaka 40, bado kiinua mgongo chake kikawa shilingi milioni 30 tu, na pensheni ya mwezi kuwa shilingi laki moja elfu hamsini kutoka Januari mwaka juzi, kutoka shilingi laki moja elfu tano waliyokuwa wakipata kwa miaka 20 nyuma, na waheshimiwa wanaohusika wamekauka kau, kama shati la mtumba!
Wakati mstaafu akilipwa “maumivu” hayo, mwakilishi wake anayesemekana kumwakilisha, na aliyefanya kazi ngumu ya kuunga mkono hoja na kupiga makofi meza badala ya mashavu ya wanaohusika, amelipwa kiinua mgongo cha shilingi milioni… mama wee!… 300; na akipata mshahara wa shilingi milioni… mama wee!… kumi na nne! Kweli, watu wote tuko sawa, lakini kuna wengine wako sawa zaidi kuliko sisi makapuku wa kima cha chini!
Tufupishe maneno. Tunahitaji Wizara ya Wastaafu, kama zilivyo za watoto, vijana na wanawake. Hawa wote sisi tulifanya kazi njema ya “kuijaza” nchi! Inashangaza sana sisi wastaafu tunasahaulika, lakini tuliowaleta duniani kwa maagizo ya Mungu sasa wanaundiwa wizara zao, huku sisi tukiishia kuwa kapuku!
Kubwa la kwanza litakalofanywa na wizara yetu wenyewe itakayoanzishwa ni kuitaka Serikali na vibubu vyote vinavyohusika, kumlipa fasta mstaafu shilingi milioni tano laki tano wanazodai kuwa watampa akishakufa! Narudia tena, acheni utani mbaya na maisha ya mstaafu aliyeijenga na kuilinda nchi hii.
Mpeni mstaafu milioni tano na laki tano zake akiwa hai, sio akiwa tayari mkazi wa Kinondoni. Zitamsaidia nini, au atawatia hasara kiasi gani?
Hao watoto wake na mwenza wake mnaojifanya mnawaonea huruma sana kwa kuwapa hiyo milioni tano na laki tano dingi wao mstaafu akishafariki, eti wagawane kuwatoa majonzi, kama watazipata… kumbukeni kuwa mstaafu aliwaonea huruma kwa miaka 40 aliyofanya kazi na mkamkata mshahara wake kumuwekea akiba ya wafanyakazi. Mpeni anachostahili!
0754 340606 / 0784 340606