**********
Mtandao wa mashirika yanayopinga ukeketaji Tanzania umependekeza kutungwa kwa sheria maalum ya kupinga ukeketaji itakayolinda pia wanawake watu wazima, ili kuziba mapengo yaliyopo kwenye mifumo ya kisheria na kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo hivyo nchini.
Akizungumza leo Februari 6, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Anna Henga, akisoma tamko la pamoja la mashirika takribani 30 yanayopinga ukeketaji, amesema licha ya kupungua kwa vitendo hivyo bado juhudi za makusudi zinahitajika ili kuvikomesha kwa kasi zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Anna Henga, akisoma tamko la pamoja la mashirika takribani 30 yanayopinga ukeketaji.
Amesema Sheria ya Kanuni ya Adhabu kwa sasa inazuia ukeketaji na kulitambua tendo hilo kuwa ni kinyume cha sheria pale linapofanyika kwa mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18, lakini haijawapa ulinzi wa kutosha wanawake watu wazima.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia na Afya – Tanzania (TDHS 2022), kiwango cha ukeketaji kimepungua kutoka asilimia 10 mwaka 2015/16 hadi asilimia 8 mwaka 2022 kwa wanawake wenye umri wa miaka 15–49, huku Arusha na Manyara zikiongoza kwa kiwango cha juu zaidi kwa asilimia 43 kila mmoja.
Utafiti huo unaonesha kuwa asilimia 34 ya waliokeketwa walifanyiwa vitendo hivyo wakiwa chini ya umri wa miaka mitano, mara nyingi kwa madai ya kutibu lawalawa au madudu, huku asilimia 28 wakikeketwa wakiwa na umri wa miaka 10–14, na zaidi ya asilimia 55 ya vitendo hivyo kufanywa na wakunga wa jadi.
Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Kupinga Ukeketaji nchini, Joshua Ntandu Lissu, amesema bado mila na imani potofu zina mchango mkubwa katika kuendeleza ukeketaji, hasa katika mikoa ya Arusha na Manyara, akisisitiza umuhimu wa elimu kwa jamii na uwajibikaji wa wazazi na viongozi wa mila.
Kwa upande wake, Vaileth amesema mapambano dhidi ya ukeketaji yanahitaji mshikamano wa wadau wote, akibainisha kuwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji kila Februari 6 ni fursa ya kukumbusha madhara ya kimwili, kisaikolojia na kijamii yanayowakumba wanawake na watoto wa kike.












