Mtoto wa kiume wa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu wa Libya, Muammar Gaddafi, Saif al-Islam Gaddafi, anatarajiwa kuzikwa baadaye leo katika mji wa magharibi wa Bani Walid, eneo linalotajwa kuwa ngome ya wafuasi wa familia ya Gaddafi.
Saif al-Islam alifariki dunia tarehe 3 Februari, baada ya kushambuliwa nyumbani kwake kaskazini magharibi mwa mji wa Zintan, tukio lililoripotiwa kuhusisha watu wanne wenye silaha.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya ndani ya Al-Wasat, mwili wake uliwasili Bani Walid jana kabla ya mazishi, jambo lililovuta mamia ya waombolezaji waliokusanyika kutoa heshima zao za mwisho.
Saif al-Islam aliwahi kuonekana kama mrithi wa kisiasa wa baba yake wakati wa utawala wa miongo minne wa Muammar Gaddafi. Baada ya kupotea kwenye medani ya siasa kwa muda mrefu kufuatia kuanguka kwa utawala huo mwaka 2011, alijitokeza tena mwaka 2021 akitangaza nia ya kugombea urais, ingawa uchaguzi huo haukufanyika.
Kufuatia tukio la kifo chake, mamlaka yenye makao yake Tripoli imeamuru kufanyika kwa uchunguzi rasmi kuhusu mauaji hayo na kutoa salamu za rambirambi kwa familia. Hata hivyo, upande wa kambi ya mashariki mwa Libya, ambayo ni hasimu wa kisiasa, bado haujatoa tamko lolote kuhusu tukio hilo.
Kifo chake kinaongeza sura mpya ya sintofahamu ya kisiasa nchini Libya, taifa ambalo bado linakabiliwa na mgawanyiko wa kiutawala na migogoro ya mara kwa mara tangu kuanguka kwa utawala wa Gaddafi.
Related
