:::::::
Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, ametoa wito kwa vijana kupewa jukumu la kuongoza zoezi la upandaji miti katika makazi yao ili kuhakikisha linakuwa endelevu na lenye matokeo chanya kwa mazingira ya Taifa.
Akizungumza leo Februari 6,2026 jijini Dodoma katika hafla fupi ya upandaji miti iliyoandaliwa na taasisi ya Habari Conservation Organization (HCO), Mhe. Pinda alisema kuna haja ya kupanga mikakati madhubuti itakayowaunganisha vijana, viongozi wa mitaa na vyama pamoja na serikali ili kufanikisha zoezi hilo.
“Nina mawazo kwamba hatujapangana vizuri. Tutumie vijana katika makazi yetu, tuwaandalie mpango maalum, na kazi yetu iwe ni kupita na kukagua kuona inaendaje. Vijana wapo wengi na wanaweza kufanya maajabu,” alisema.
Aliongeza kuwa yupo tayari kuwa balozi wa kampeni hiyo akiamini kuwa nguvu ya vijana inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika uhifadhi wa mazingira.
Aidha, alimpongeza Mhe. Rais kwa kuamua kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda miti, akisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya dhati ya kulinda mazingira.
Katika hotuba yake, Mhe. Pinda alipinga msemo wa “kata mti, panda mti”, akisisitiza kuwa mara nyingi anayekata mti hasukumiwi kupanda mwingine. Badala yake, alishauri kuwe na mfumo wa makusudi wa kujaza mapengo yaliyotokana na ukataji miti kwa mpango maalum na unaosimamiwa vizuri.
Alitaja changamoto ya umwagiliaji maji, lakini akaeleza kuwa mitaani bado kuna uwezekano wa kuendesha zoezi hilo kwa kushirikisha viongozi wa mashina na matawi ya vyama, pamoja na serikali za mitaa.
Pia alihimiza upandaji wa miti ya matunda ili kutoa hamasa zaidi kwa wananchi kuitunza kutokana na faida zake kiuchumi na kiafya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, alisema mkoa huo umepewa jukumu la kupanda miti elfu 40 ndani ya kipindi cha miaka mitano, mpango ambao ulikamilika mwaka jana, na sasa maandalizi ya mpango mpya yanaendelea.
Alisema pamoja na juhudi zilizofanyika, bado lengo halijafikiwa kikamilifu kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo hali ya hewa ya Dodoma ambayo inahitaji uangalizi mkubwa wa miti inayopandwa.
“Miti imepandwa, lakini siyo mingi kama inavyotakiwa.
Tuna vipaumbele vya kupanda miti katika vyanzo vya maji, taasisi, kaya na maeneo ya kandokando ya mito. Pia tumeanzisha zao la tufaa mwaka 2025 ambalo limepokelewa kwa mwamko mkubwa. Lengo siyo tunda tu, bali mti kusaidia hali ya hewa,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa PPRA, Denis Simba, alisema taasisi hiyo imekuwa mdau mkubwa wa mazingira kupitia utekelezaji wa mfumo wa kidigitali wa ununuzi wa umma (NeST), uliolenga kupunguza matumizi ya karatasi, safari zisizo za lazima na uchafuzi wa mazingira.
Kwa mujibu wa Simba, tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya tani milioni 600 za miti zimeokolewa kutokana na matumizi ya mifumo ya kidigitali badala ya makaratasi na safari za zabuni.
Aliongeza kuwa mradi wa NeST tayari umesajiliwa katika Kamisheni ya National Carbon Trade na unatarajiwa kuingizia taifa mapato ya mabilioni ya fedha kupitia biashara ya hewa ukaa.
Afisa Habari wa HCO, Loyce Joseph, alisema taasisi yao imejikita katika kuhamasisha upandaji miti kwa wingi na kuwataka wananchi kutoliona suala hilo kama jukumu la serikali pekee.
“Dodoma imeongezeka wakazi baada ya serikali kuhamia hapa. Watu wanahitaji hewa safi. Miti tunayopanda itawanufaisha wote na kupendezesha mandhari ya jiji letu,” alisema.
Aliongeza kuwa maono ya uongozi wa mkoa ni kuona Dodoma inakuwa jiji la mfano lenye misitu ya kimkakati itakayosaidia kusafisha hewa na kuboresha mazingira, kama ilivyo kwa majiji mengine yaliyoendelea.
Hafla hiyo imeacha ujumbe mzito kwamba mafanikio ya uhifadhi wa mazingira yanahitaji ushirikiano wa kila mdau, huku vijana wakitajwa kuwa nguzo kuu ya mapinduzi ya kijani nchini.




