Samia abadili muundo wizara ya Profesa Kitila, ateuwa viongozi

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya muundo wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Wizara ya Nishati kwa kuzifanya kuwa na Makatibu Wakuu wawili kwa kila wizara.

Sambamba na mabadiliko ya muundo huo, pia amewateua Dk Tausi Kida kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, huku Dk Fred Msemwa akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Uwekezaji.

Taarifa ya mabadiliko hayo, imetolewa leo Ijumaa Februari 6, 2026 na kutiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, akimrejelea Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kanali Yahya Kido ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera akichukua nafasi ya Fatma Mwassa na Kanali Donald Msengi ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, akichukua nafasi ya Kanali Patrick Sawala atakayepangiwa majukumu mengine.

Aidha, Rais Samia amemteua Balozi Waziri Salum, kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, akichukua nafasi ya Dk Hashil Abdallah ambaye atapangiwa majukumu mengine.

Pia, Dk James Mataragio ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi asilia, huku Felchesmi Mramba akiteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya umeme na nishati jadidifu.

Uteuzi huo pia, umehusisha makatibu tawala wa mikoa, Dk Toba Nguvila ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, akichukua nafasi ya Missaile Musa ambaye amestaafu.

Dk Stephen Nindi ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, akichukua nafasi ya Judica Omary ambaye amestaafu.

Kwa upande wa manaibu Katibu wakuu, Nsubili Joshua ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha anayeshughulikia huduma za hazina.

Joshua anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenifa Omolo ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana.

Aristides Mbwasi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, akichukua nafasi ya Dk Suleiman Serera ambaye atapangiwa majukumu mengine.

Profesa Mohammed Sheikh ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia masuala ya uvuvi, huku Dk Edwin Mhede aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu katika wizara hiyo atapangiwa majukumu mengine.

Rose Ambrose ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Emmanuel Tayari ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Afya anayeshughulikia masuala ya dawa na vifaatiba.

Profesa Peter Msoffe amehamishwa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya mazao na usalama wa chakula, akichukua nafasi ya Dk Stephen Nindi ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.

Dk Fabian Madele ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia masuala ya mifugo na Balozi Barak Luvanda ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya mazingira.

Aidha, Sosthenes Kewe ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mtendaji, Tume ya Taifa ya Mipango anayeshughulikia masuala ya ufuatiliaji na tathmini, akichukua nafasi ya Dk Linda Ezekiel ambaye atapangiwa majukumu mengine.

Pia, Meja Jenerali Marco Gaguti ameteuliwa kuwa Balozi na atapangiwa kituo na Dk Hassan Mshinda ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Uapisho wa viongozi wateule utafanyika kwa tarehe itakayopangwa baadaye.