Dar es Salaam. Wakati ukeketaji kwa wasichana ukitajwa kuwa janga kwenye baadhi ya mikoa nchini Tanzania, takwimu mbalimbali zinaonyesha wasichana wadogo wamekuwa wakipitia unyanyasaji huo kwa kivuli cha kudumisha mila na tamaduni.
Hata hivyo, wadau mbalimbali wamekuwa wakipaza sauti kukemea na kutaka kutokomezwa kwa mila hizo potofu zinazowaathiri wasichana wadogo kisaikolojia.
Baadhi ya mikoa kama Mara, Arusha, Manyara na Singida, inatajwa kuwa kinara kwenye ukatili huo, licha ya jitihada za muda mrefu za Serikali kwa kushirikiana na wadau kutoa elimu kwa jamii husika wakiwemo mangariba.
Takwimu za demografia ya afya za mwaka 2022 zimeonyesha mikoa inayoongoza kwa ukeketaji Tanzania ni Arusha (asilimia 43), Manyara (asilimia 43), Mara (asilimia 28) na Singida (asilimia 20).
Hata hivyo, hivi karibuni imebainika kuwa nyuma ya ukatili huo, kumeibuka biashara ya viungo vinavyotokana na ukeketaji.
Mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa la Pathfinder na Serikali ya Norway kupitia ubalozi wake wa Dar es Salaam, wakionesha hati ya makubailiano ya kutekelezaji mradi wa afya ya vijana na haki za uzazi wa Her future katika mikoa ya Morogoro na Arusha utakaotelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu (2026- 2028).
Katika uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na Mwananchi, imebainika kwamba biashara hiyo inaongeza ugumu wa kutokomeza mila hiyo potofu nchini, licha ya kuwapo sera, sheria na kanuni zinazoipiga marufuku.
Uchunguzi huo uliofanyika katika Wilaya za Butiama, Tarime na Serengeti, mkoani Mara, umebaini imani za kishirikina ndizo huchochea biashara ya siri inayohusisha uuzaji wa sehemu nyeti za wanawake zilizokatwa.
Katika ufuatiliaji huo, imebainika kuwa viongozi wa kimila na mangariba ndio wanaodaiwa kufanya biashara hiyo, ikiaminiwa kuwa wamiliki wa boti za uvuvi huvitumia katika uvuvi na huwalinda dhidi ya mikosi.
Kutokana na hilo, Shirika la Kimataifa la Pathfinder kwa kushirikiana na Serikali ya Norway, kupitia ubalozi wake nchini, wameingia makubaliano ya kutekelezaji mradi wa afya ya vijana na haki za uzazi, unaolenga kukabiliana na ukatili huo kwa wasichana pamoja na mimba za utotoni.
Mradi huo uliopewa jina la Her Future utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu (2026 – 2028) ambapo karibu Sh11 bilioni kimepangwa kutumika ikihusisha mikoa ya Arusha na Morogoro.
Hata hivyo, makubaliano hayo yanaingiwa wakati leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kupinga ukeketaji.
Kwa nini Morogoro na Arusha?
Akieleza kwanini wamechagua mikoa hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa Pathfinder, Dk Joseph Komwihangiro amesema kwanza mradi unalenga vijana walio na umri kanzia miaka 10 hadi 24 katika kutokomeza mila potofu zinazowaandama.
“Kwa ufupi uhitaji kama huu uko sehemu nyingi. Ukiangalia suala la mimba za utotoni Katavi ndio wanaongoza kwa takribani asilimia 42 wanapata mimba wakiwa chini ya miaka 20. Lakini kwa bahati nzuri Katavi kuna nguvu kubwa ya uwekezaji wa Serikali na wafadhili.
“Vilevile Tabora ni mkoa namba mbili kwa mimba za utotoni lakini kwa bahati nzuri tayri kuna uwekezaji upo unaendelea wa Serikali na wadau,” amesema.
Amesema kwa bahati mbaya Morogoro na Arusha bado hakuna uwekezaji akisema mfano Morogoro ni mkoa wa tatu kuwa na kina mama wengi wanaojifungua ambapo humohumo ndipo kuna mimba za utotoni hivyo ni mkoa muhimu katika masuala ya afya ya uzazi.
“Ukija mkoa wa Arusha nao mbali ya masala ya mimba za utotoni kuna tatizo la ukeketaji ambapo asilimia 43 ya wanawake wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 49 wamekeketwa kwa hiyo mradi huu utasaidia juhudi za serikali katika kutokomeza ukeketaji wa wanawake na wasichana,”amesema.
Akieleza zaidi amesema takwimu za kupambana na ukeketaji kwa sasa ni nzuri ambapo kwa sasa kuna asilimia nane ya waliokekektwa hadi mwaka 2022 ukilinganisha na asilimia 18 ya miaka ya 1990.
Amesema bado kuna mikoa kama Singida, Mara, Arusha, Tabora na Manyara bado tatizo lipo hivyo nguvu na jitihada zaidi zinahitajika.
Hivyo katika kutekeleza mradi huo amesema watakuwa wanawafikia vijana wa Arusha na Morogoro waliokatika mfumo wa elimu yaani shuleni pamoja na wale walionje ya mfumo wa elimu.
“Kwa vijana walionje ya mfumo wa shule tutawapatia msaada wa kujitambua, uwezo wa kujiimarisha kiuchumi,” amefafanua.
Akieleza kiini cha ukeketaji amesema lazima mbinu nyingi ziwalenge wazazi kwakuwa wanawakeketa watoto wakiwa bado wadogo hawajielewi hivyo lazima waambiwe madhara yakeikiwemo kifo.
Mradi wa Her Future unachangia juhudi za Tanzania za kuboresha afya ya uzazi, kwa msisitizo katika kupunguza mimba za utotoni, vifo vya akina mama na matukio ya ukatili wa kijinsia (GBV) itashirikisha mashirika ya Femina HIP, Baraza la Wanawake Wachungaji (PWC), na Shirika la Wasichana la Amani la Mwanza.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utiaji saini iliyofanyika Makazi ya Balozi wa Norway Naibu Mkuu wa Ujumbe wa Ubalozi wa Norway nchini Tanzania, Kjetil Schie, amesema Norway imejitolea kuwa bingwa wa kimataifa wa afya uzazi.
“Tutaendelea kusimama na washirika wanaofanya kazi kukuza afya na haki za wanawake, wasichana, na makundi yaliyotengwa Norway inaunga mkono juhudi zinazoongozwa na Watanzania zinazowalinda wasichana, kuwawezesha jamii, na kuhakikisha kwamba maendeleo kuelekea Dira ya 2050 yanaharakishwa na kudumishwa,”amesema.
Naishorwa Masago kutoka Shirika la PWC Arusha ametafsiri ukeketaji na ulemavu akisema kumfanyia hivyo muhusika ni sawa na kumsababishia ulemavu hivyo anashauri wenye tabia hiyo kuacha.
Mkurugenzi wa Femina Hip, Ruth Mlay, amesema ili kuondokana na ukeketeaji kwanza tunapaswa kuachana na mila na desturi zinazoumiza ikiwemo ukeketaji na unyanyasaji.
Naye, Mkurugenzi wa Amani Girls, Revocatus Sono amesema sababu ya ukeketaji ni mila na tamaduni ambazo zinaingiliana kwa jamii tofauti.
“Wapo wanaochagiza mambo haya yaendelee wanapaswa kuwezeshwa kufanya mambo mengine na kuachana na hili suala,” amesema.