Dar es Salaam. Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania (TAB) imewaomba wadau mbalimbali kuendelea kuwasaidia vifaa saidizi, zikiwamo fimbo za kutembelea na mashine za kuandikia maandishi ya nukta nundu, vinavyowawezesha watu wenye ulemavu wa kuona kuendesha maisha yao ya kila siku kwa uhuru na kujiamini.
Ombi hilo limekuja kufuatia kupokea msaada wa fimbo za kutembelea 452 na mashine tatu za kuandikia maandishi ya nukta nundu kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), hafla iliyofanyika leo Ijumaa Februari 6, 2026 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Mratibu wa Idara ya Vijana wa TAB, Bakari Hassan, ameishukuru PSSSF kwa msaada huo akisema vifaa hivyo vitawanufaisha wanachama wa jumuiya hiyo pamoja na wanafunzi wenye ulemavu wa kuona katika shule mbalimbali nchini.
Amesema sehemu ya fimbo hizo zitapelekwa katika mikoa ya Tanga, Dodoma, Arusha, Morogoro na Kilimanjaro ambako kuna mahitaji makubwa ya vifaa saidizi kwa watu wasioona.
“Tutavitumia vifaa hivi na vingine tutavipeleka katika shule zenye uhitaji mkubwa. Hata hivyo, mahitaji bado ni makubwa, hivyo tunaomba wadau wengine wajitokeze kutuunga mkono,” amesema Hassan.
Amesema gharama za vifaa saidizi ni kubwa kiasi ambacho jumuiya hiyo na wanachama wake hawawezi kumudu kirahisi, hali inayowafanya kuendelea kutegemea misaada kutoka kwa wadau mbalimbali.
Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo amesema msaada huo unalenga kuwawezesha watu wenye ulemavu wa kuona kuishi maisha ya heshima, kujiamini na uhuru zaidi katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Mkurugenzi Mkuu PSSSF, Fortunatus Magambo akikabidhi msaada wa vifaa kwa jumuiya ya watu wasioona leo jijini Dar es Salaam.
Amesema vifaa vilivyotolewa vina thamani ya zaidi ya Sh30 milioni, akisisitiza kuwa mfuko huo unaendelea kutekeleza majukumu yake ya uwajibikaji kwa jamii kwa kusaidia makundi yenye uhitaji maalumu.
Ameahidi PSSSF utajengea choo maalumu katika ofisi za Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania ili kuwezesha mazingira rafiki kwa wanachama wa jumuiya hiyo.
“PSSSF itaendelea kutoa msaada pale inapohitajika, lakini pia tunatoa wito kwa taasisi nyingine kushirikiana katika kusaidia makundi yenye mahitaji maalum yaliyopo kwenye jamii,” amesema Magambo.
Awali, Meneja wa PSSSF Kanda ya Ilala, Amina Kassim alisema ulemavu wa kuona unahitaji nyenzo sahihi na bora zitakazowezesha watu wenye hali hiyo kupata huduma muhimu ikiwamo elimu kwa ufanisi.
Amesema mashine za kuandikia maandishi ya nukta nundu zitawawezesha watu wasioona kusoma na kuandika kwa ufanisi zaidi, akibainisha kuwa msaada huo ni uthibitisho wa imani ya PSSSF kuwa ulemavu si kikwazo cha uwezo wa mtu endapo mazingira rafiki yatazingatiwa.
“Msaada huu unaonesha imani yetu kwamba ulemavu si kikwazo cha uwezo, bali kinachohitajika ni kuwepo kwa mazingira na nyenzo sahihi,” amesema Kassim.
Mjumbe wa Bodi ya Jumuiya ya Watu Wasioona Tanzania, Vitalis Mdoe, amesema vifaa hivyo ni muhimu sana kwa watu wenye ulemavu wa kuona kwani vinatumika kama macho yao katika maisha ya kila siku.
“Msione ni vitu vidogo, kwetu vina maana kubwa sana. Tunashukuru PSSSF kwa msaada huu, hasa fimbo hizi tunazozihitaji sana kwa kuwa ni rahisi kukunjwa na kubebwa mfukoni,” amesema Mdoe.
Ameongeza kuwa licha ya msaada huo, changamoto bado ni nyingi kwa watu wasioona nchini, hivyo ameomba wadau kuendelea kuwasaidia ili kuboresha maisha yao na kuongeza fursa za elimu, ajira na ushiriki katika shughuli za kijamii.