TAEC KUTEKELEZA MIRADI MIKUU 4 UKIWEMO ULE WA HUDUMA ZA TIBA NA UCHUNGUZI WA SARATANI NCHINI.

Na Vero Ignatus – Arusha.

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imesema kwa sasa inasimamia na kuratibu utekelezaji wa miradi mikubwa minne (4) ya kimkakati inayotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomiki duniani (IAEA)

Akizungumzia ujio wa ugeni huo Makao Makuu ya TAEC jijini Arusha,Mkurugenzi Mkuu wa TAEC Profesa Najat Kassim Mohammed 4 februari 2026 alisema lengo la ziara hiyo ni pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya IAEA na Tanzania sambamba na kutathmini utekelezaji wa miradi ya nyuklia katika kuongeza thamani katika sekta ya Afya, kilimo pamoja na uhifadhi WA chakula.

Profesa Najat amesema ugeni huo uliongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kiufundi kwa Afrika wa IAEA, Gashaw Wolde, pamoja na Afisa Msimamizi wa Programu za Afrika,Azza Kashan,waliweza kutembelea mradi mkubwa zaidi unaolenga kuimarisha huduma za tiba na uchunguzi wa saratani nchini ambao ni miongoni mwa miradi hiyo minne

Aidha amesema kuwa awali Tanzania ilikuwa na vituo viwili pekee vya huduma hizo ambavyo ni Hospitali ya Ocean Road na Bugando, lakini kupitia mradi huo idadi ya vituo itaongezeka kutoka viwili hadi sita hivyo ujumbe huu wa IAEA umetembelea pia maeneo mbalimbali ya miradi, ikiwemo Hospitali ya Benjamin Mkapa, na unatarajiwa kuendelea na ziara katika Shinyanga na Zanzibar

“Wageni wetu wametambua tofauti kubwa kati ya hali ya sasa na miaka ya nyuma. Leo tuna miundombinu imara, maabara za kisasa na wataalamu waliobobea, jambo linaloonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania katika kuwekeza kwenye sayansi na teknolojia,’ Amesema Profesa Najat.

Profesa Najat ameainisha kuwa Vituo vipya vitakavyotoa huduma hizo ni pamoja na KCMC, kinachotarajiwa kuanza kutoa huduma hivi karibuni, Hospitali ya Benjamin Mkapa, ambayo ujenzi wake uko katika hatua za mwisho, pamoja na Kituo cha Mbeya, ambacho nacho kipo katika hatua za utekelezaji.

Akifafanua miradi inayotekelezwa ni pamoja na ule wa ujenzi wa kituo cha Irradiator jijini Dar es Salaam, ambacho kitahusika na matumizi ya mionzi kwa ajili ya kuhifadhi vyakula, kuua vimelea na kuongeza muda wa matumizi ya mazao bila kuhatarisha afya za walaji.

Vilevile miradi Mwingine ni ule wa wa ujenzi wa maabara ya kisasa ya mifugo Zanzibar, unaotekelezwa kwa ushirikiano na maabara kutoka Vietnam, ukiwa na lengo la kuboresha uchunguzi wa magonjwa ya wanyama kuimarisha usalama wa chakula na kukuza sekta ya mifugo kwa kutumia sayansi ya kisasa.

TAEC kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati imeendelea kufanya mazungumzo ya kitaalamu kuhusu maandalizi ya muda mrefu ya matumizi ya nishati ya nyuklia kama chanzo mbadala cha umeme, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa nishati na kukuza uchumi wa taifa, ambapo dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya sayansi na teknolojia.