Dar es Salaam. Tukiwa tunakaribia kuingia katika msimu wenye kheri na thawabu nyingi, msimu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, Muislamu yampasa asipuuzie misimu huu, bali awe miongoni mwa wenye kushindana katika kufanya mema.
Allah Mtukufu amesema:“Na katika hayo basi na washindane wanaoshindana” (83: 26). Mwezi wa Ramadhani ni fursa ya kipekee ya kuutumia wakati vizuri. Hivi ndivyo inavyopaswa aamini Muislamu, na ndivyo walivyoamini wema walitangulia.
Muislamu, ajitahidi kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa njia sahihi zifuatazo: Mosi. Kuwa na nia ya kweli na kumuomba Allah Mtukufu amuafikishe kuudiriki mwezi wa Ramadhani, hali ya kuwa na afya njema na nguvu, ili awe na hamasa katika kumuabudu kwa kufunga, kusimama usiku (qiyamu Lail).
Mtume wa Allah (Rehema na amani ziwe juu yake) alikuwa akisema kila ulipoingia mwezi wa Rajab: “Ewe Allah, tubarikie (katika mwezi) Rajab na Sha‘ban, na utufikishe (katika mwezi) Ramadhani.” (Ahmad). Tunawajua watu waliokuwa pamoja nasi Ramadhani iliyopita lakini hawapo nasi mwaka huu.
Pili: Kumshukuru Allah kwa Kuuona mwezi wa Ramadhani. Imamu An-Nawawiy (Allah Amrehemu) amesema katika kitabu cha Al-Adhkar: “Tambua kwamba inapendekezwa (sunna) kwa yule aliyepata neema iliyo wazi, au kuondoshewa balaa lililo wazi, asujudu kama shukrani kwa Allah Mtukufu, au amtukuze na kumsifu kwa sifa anazostahiki.”
Miongoni mwa neema kubwa kabisa alizojaaliwa mja ni kuudiriki mwezi wa Ramadhani akiwa na afya njema. Mtume wa Allah alikuwa akiwabashiria Maswahaba wake kuja kwa mwezi wa Ramadhani kwa kusema: “Umekujieni mwezi wa Ramadhani, mwezi wa baraka; Allah amekulazimisheni kufunga ndani yake; hufunguliwa milango ya Pepo na hufungwa milango ya Jahannamu …” (Ahmad).
Tatu: Azma na mipango ya mapema ya kunufaika na Ramadhani. Watu wengi kwa masikitiko makubwa, hata wale wanaojitahidi katika dini, huweka mipango ya kina kwa mambo ya dunia, lakini wachache sana hupanga kwa mambo ya Akhera.
Miongoni mwa mipango hiyo ya Akhera ni kupanga namna ya kuutumia mwezi wa Ramadhani katika ibada na utiifu.
Nne: Inampasa muumini amuabudu Allah kwa ujuzi. Hajapewa udhuru wa ujinga katika faradhi alizozilazimisha Allah kwa waja wake. Miongoni mwa faradhi hizo ni kufunga Ramadhani.
Hivyo, ni wajibu kwa Muislamu kujifunza masuala na hukumu za funga kabla ya kuingia Ramadhani, ili funga yake iwe sahihi na ikubalike kwa Allah. Allah Mtukufu amesema: “Basi waulizeni wenye elimu ikiwa hamjui” (21: 7).
Tano. Kuukaribisha kwa toba ya kweli. Tunapaswa kuukaribisha mwezi wa Ramadhani kwa azma ya kuacha madhambi na maovu, kutubia kwa toba ya kweli kutokana na dhambi zote, kuziacha kabisa na kutozirudia.
Ramadhani ni mwezi wa toba; asiyetubia ndani yake, basi atatubia lini? Allah amesema: “Na tubieni kwa Mwenyezi Mungu nyote enyi Waumini ili mpate kufaulu” (24: 31).
Sita: maandalizi ya kisaikolojia na kiroho
Hufanyika kwa kusoma na kusikiliza mafundisho ya Kiislamu (mihadhara na darsa) yanayobainisha fadhila za funga na sharia zake, ili nafsi ijiandae kwa utiifu. Mtume wa Allah alikuwa akiwaandaa Maswahaba wake kuunufaika na mwezi huu.
Saba: Kupunguza kula. Hii ni miongoni mwa makusudio ya funga ya Ramadhani, kwa kuizoesha nafsi kupunguza chakula, kulipa tumbo nafasi ya kupumzika, na kuipa nafsi nafasi ya utiifu.
Ulaji mwingi hufanya nyoyo kuwa ngumu kama mawe, ukaifanya nafsi izidiwe na uzito wa ibada. Kupunguza chakula husababisha ulaini wa moyo, nguvu ya ufahamu, unyenyekevu wa nafsi, na kudhoofisha matamanio na hasira.
Nane: Kusimama usiku (Qiyam al-Layl): Hii ni Sunna kubwa tuliyoiacha; ni ladha ya ajabu ambayo hatujaionja, na ni pepo kwa Waumini katika maisha haya, lakini kwa masikitiko hatujaingia humo wala kuiona.
Ni chuo kinacholea nafsi, kinachotakasa nyoyo, na kurekebisha maadili. Ni kazi nzito na jihadi kubwa, isiyoweza kufanywa ila na mashujaa wa wanaume na wanawake wanyenyekevu, wenye subira na ukweli… nyakati za usiku wa mwisho.
Ni wasia wa Mtume na desturi ya watu wema waliotangulia: “Shikamaneni na kusimama usiku; kwani ni desturi ya watu wema kabla yenu, ni njia ya kujikurubisha kwa Allah, ni kizuizi cha maasi, ni kafara ya madhambi, na huondoa maradhi mwilini.”
Kuuizoesha nafsi kusimama usiku ni jambo muhimu kabla na baada ya Ramadhani. Ndani yake kuna siri zinazoifungua mioyo, kuvunja minyororo yake, kushusha rehema na baraka, na kufunguliwa milango ya ufahamu ambayo haijulikani ila kwa Allah Mtukufu.
Tisa: Kuzidisha kuisoma Qur’an. Ramadhani ni mwezi wa Qur’an. Qur’an ina fadhila ya pekee katika Ramadhani. Mtume wa Allah alikuwa akisoma Qur’an na malaika Jibril kila usiku wa Ramadhani, kama ilivyopokewa katika Hadithi ya Ibn Abbas. Na Mtume wa Allah alikuwa akirefusha sana kusimama kwake usiku, kama ilivyopokewa katika Hadithi ya Hudhaifa.
Hivyo ndivyo walivyokuwa wakifanya salaf (wema waliotangulia) katika kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhan. 0712 690811