Wagonjwa wanavyoteseka vitengo vya dharura hospitalini

Dar es Salaam. Ni dakika za kuhesabu uhai. Umempeleka mgonjwa, amepata dharura au ajali, lakini wahudumu wanaingia huku na wanatokea kule, umewahi kukutana na kero hii?

Vitengo vya huduma za dharura (Emergency Department) kwenye baadhi ya hospitali za umma na binafsi nchini, vimeendele kuwa maeneo ya kusubiria malipo badala ya kuokoa maisha, hali inayochangia vifo vinavyoweza kuzuilika, uchunguzi wa Mwananchi umebaini.

Hili linabeba sura halisi ya changamoto ya kitaifa, huduma za dharura zinazopaswa kutolewa bila masharti zinazuiwa na malipo, hali inayozua maswali kuhusu uwajibikaji wa hospitali, usimamizi wa Serikali na uhai wa wagonjwa wasiokuwa na uwezo, hasa watoto.

Baadhi ya hospitali za umma na binafsi, zimetajwa kuhusika kukataa wagonjwa mpaka pale watakapokuwa wamelipia fedha za kumuona daktari na huduma za vipimo.

Zingine zimekuwa zikichelewesha huduma hadi malipo yatolewe, wengine wanafika wakiwa wanavuja damu nyingi, lakini huacha wagonjwa wakisubiri kwa muda mrefu wakati wako hatarini na hutumia neno ‘utaratibu wa hospitali’ kama kisingizio.

Hali hiyo ni kinyume na maadili na Sera ya Taifa ya Afya inayosisitiza utekelezaji wa viwango vya huduma na ushirikiano kati ya sekta ya umma, binafsi na wadau wengine ili kupanua upatikanaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na huduma za dharura.

Pia, inakwenda kinyume na Sheria ya Afya ya Umma (Public Health Act) inayotoa mfumo wa kuratibu na kudhibiti afya ya umma pamoja na udhibiti wa magonjwa ya dharura.

Akizungumza na Mwananchi jana Alhamisi Februari 5, 2026, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea amesema utaratibu wa Serikali na Wizara ya Afya kwa mujibu wa sera, mgonjwa anapofika kwenye kituo cha kutolea huduma za afya, mwenye dharura jambo la kwanza ni kumpa huduma kwa lengo la kuokoa maisha.

Amesema hiyo ni hata kwa wale wasiotambulika na mgonjwa akishatengamaa ndipo utambulisho wa majina na mengine unafuata.

“Hospitali zina mifumo ili aweze kupata vipimo lazima majina yatambulike, kama hajulikani aandikwe mgonjwa asiyejulikana vipimo vichukuliwe na inapofanyika kinyume ni makosa, wachukuliwe hatua,” amesema.

Dk Nyembea amewataka wananchi kutoa taarifa kwa mkuu wa hosptali husika wanapokumbana na changamoto yoyote, ili wapatiwe msaada kabla hali ya mgonjwa kuwa mbaya.

Mratibu wa mafunzo ya huduma ya kwanza kutoka Chama cha Msalaba Mwekundu, Almachius Kagenzi amesema kitaalamu kuna umuhimu mkubwa wa kutoa huduma ya kwanza kwa mwenye dharura, ni katika kuokoa uhai wa mtu, pili kuondoa maumivu na tatu kumwondoa katika hatari ya ulemavu ambao ungeepukika.

“Mfano mara nyingi wengi hushuhudia wakisema, tulimtoa nyumbani mzima kufika hospitali wakasema ameshafariki, hapa katikati alipaswa kufunguliwa njia za hewa, kumlaza mlalo salama na akifika hospitali ahudumiwe haraka iwezekanavyo,” amesema Kagenzi.

Ni kutokana na umuhimu huo, Jeshi la Polisi Tanzania limebadili utaratibu ambao awali, ili mgonjwa wa ajali apate matibabu ilikuwa lazima apate PF3 lakini kwa sasa mtu anakwenda hospitali kutibiwa kwanza kisha PF3 inafuata.

Februri 4, 2026 mkazi wa Goba jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa) alipata ajali kwa kumgonga kwa bahati mbaya mwendesha pikipiki aliyekuwa amebeba mwanafunzi wa miaka 11 majira ya asubuhi.

Akisimulia amesema alilazimika kumkimbiza mwanafunzi hospitali binafsi, baada ya kufika alihitajika malipo kwanza ndipo mtoto ahudumiwe, wakati akiendelea na malipo kitengo cha dharura waliingizwa wanafunzi wengine watatu wakivuja damu baada ya kupata ajali.

“Walikuwa na hali mbaya wakivuja damu lakini hawakupewa huduma kwakuwa hawakuwa na fedha. Wazazi wao walipofika walielezwa wazi lazima walipie kwanza ndipo wapate huduma. Nilikaa pale kwa saa mbili mpaka naondoka na mgonjwa wangu hawakuwa wamepata huduma, wazazi wameenda kutafuta hela,” amesema mwanamume huyo.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini pia, changamoto kubwa katika Kitengo cha Dharura cha Hospitali ya Taifa ya Mloganzila, Dar es Salaam.

Mzazi mmoja aliyefika hospitalini hapo saa mbili usiku, Januari mwaka huu baada ya mwanaye kupata ajali, amesema alishuhudia hali inayotia hofu.

“Nilimkuta majeruhi aliyekuwa ameletwa zaidi ya nusu saa iliyopita, hakuwa amefungwa hata bandeji kuzuia damu. Alikuwa anatokwa damu nyingi na hali yake ilizidi kuwa mbaya,” amesema.

Amesema hali hiyo aliishuhudia pia kwa majeruhi wengine waliokuwa katika eneo hilo, akidai kasi ya huduma ilikuwa ndogo kwa eneo linaloitwa la dharura.

Mbali na hilo, majeruhi walicheleweshwa kupelekwa kwenye vipimo muhimu kama X-ray na CT Scan bila maelezo ya msingi.

“Nilipouliza sababu ya kuchelewa, majibu yalikuwa ‘atasubiri.’ Nilipouliza kama kuna foleni au daktari hayupo, hawakutoa majibu ya kueleweka,” amesema mzazi huyo.

Kilichozua taharuki zaidi ni madai ya rushwa katika kitengo hicho. Mzazi huyo anadai daktari mmoja alimwambia wazi kuwa anahitaji Sh100,000 ili amtibu majeruhi haraka, vinginevyo angesubiri hadi asubuhi.

Akijibu tuhuma hizo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili–Mloganzila, Dk Julieth Magandi amesema:“Ni taarifa ambayo naisikia kutoka kwako naomba niichukue niifanyie kazi.”

Hata hivyo, Dk Magandi alihitaji atajiwe tarehe ambayo mgonjwa alifika kupata huduma, akisema: “Tungejua angalau ni ya lini alipata huduma tutapata pa kuanzia.” Jambo hilo lilikataliwa na mlalamikaji akihofia usalama wa mtoto wake ambaye bado anaendelea na matibabu ya ufuatilizi hospitalini hapo.

Licha ya changamoto ya malipo, baadhi ya mashuhuda wameelezea namna wanavyokosa huduma kwa wakati hasa usiku licha ya kulipia fedha za kumuona daktari na vipimo.

Hayo ni baadhi ya matukio yaliyoibua maswali kuhusu tafsiri halisi ya huduma za dharura katika hospitali za umma na binafsi.

Wagonjwa, ndugu wamehoji kama kweli maeneo yanayoitwa ‘Emergency’ yanatoa huduma kwa haraka kama inavyokusudiwa au yamegeuka sehemu ya mateso, ucheleweshaji na vitendo vya rushwa.

Mmoja wa mtumishi wa umma, mkazi wa Dodoma aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema: “Kuna kitu kinapaswa kufanywa na Serikali katika hili, unaweza kuwa na bima kabisa, ukapata ajali, ukipelekwa hospitali unakuwa hujitambui, kwa kuwa huwezi kujieleza kutokana na ugonjwa, unaweza kupoteza maisha.”

Mtumishi huyo amesema kinachopaswa kufanyika, mtu akifikishwa kitengo cha dharura ahudumiwe, lakini hali ni tofauti kwa hospitali nyingi ukifika utakuta watu wanagugumia maumivu na ugonjwa.

Vyama vya kitaaluma vyalaani

Malalamiko ya huduma za dharura hapa nchini yamekuwa mengi, Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kinataja misingi ya kitaalamu, kisheria na kiutu pamoja na utaratibu wa kitengo cha dharura.

Rais wa MAT, Dk Mugisha Nkoroko amesema mgonjwa wa dharura anatibiwa bila masharti ya kuuliza fedha na kutomchelewesha matibabu, hiyo inahusu hospitali zote za Serikali, binafsi na za dini.

Amesema hiyo ipo kwenye Sheria ya Afya Tanzania na kanuni za kitaaluma za madaktari zinazosisitiza kuwa, kuokoa uhai ni kipaumbele cha kwanza.

Dk Nkoroko amesema hiyo inaenda sambamba na rufaa ya kisheria na salama kama hospitali haina uwezo wa kumhudumia, inamweka sawa kwa huduma za awali na kumpa rufaa mara moja, kwa kuwa ni haki ya mgonjwa.

“Hiyo ndiyo kanuni duniani kote, maadili ya wataalamu wa afya ni uhai wa mtu kwanza,” amesisitiza Dk Nkoronko.

Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (Tanna), Dk Ezekiel Mbao amesema chama hicho kinalaani vitendo hivyo, kwa kuwa kazi ya sekta ya afya ni kuokoa maisha ya watu.

“Kada zetu zote zina miiko yake, ukienda vitengo vya dharura unachukua hatua za kutoa huduma haraka inavyowezekana kuhakikisha mgonjwa hewa iko sawa, kupumua na vitu vyote vipo sawasawa hili lipo kinyume kabisa na maisha ya watu,” amesema.

“Tanna tunalaani, kama wanaweka hela kwanza kabla ya kuokoa maisha ya binadamu ni kinyume na maadili, lazima umhudumie kwanza. Dakika moja katika kitengo cha dharura ni muda mrefu unaotosha kuokoa maisha,” amesema.

Chama cha Watoa Huduma Binafsi wa Afya (Apftha), kimekiri kutokea kwa changamoto kadhaa ambazo, zimekuwa zikiwarudisha nyuma wamiliki wa vituo hivyo.

Hata hivyo, wameweka wazi mtu yeyote anayepata dharura ya kiafya ghafla, hakuna anayepaswa kuachwa bila matibabu, lazima apewe huduma ya kwanza kama anavuja damu inatakiwa izuiwe na kama ni ugonjwa udhibitiwe.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Aphtha, Dk Samwel Ogillo amesema vituo vingi hufanya tathmini kwanza kwa mgonjwa anayefika kitengo cha dharura kabla hawajamuuliza malipo, hiyo imewafanya wengi hasa wale wanaolipa kwa bima malipo yao huzuiwa baadaye.

“Sheria ya bima haikubali mgonjwa atibiwe ndipo fomu zijazwe, ukitibu maelezo ukajaza baadaye bima inaweza kukataa kukulipa, lazima bima wajue kwanza na ndiyo maana tunapiga simu.”

Dk Ogillo amevitaja visa kadhaa vya wagonjwa waliotibiwa kwa dharura katika hospitali binafsi na walipotengamaa walikataa kufanya malipo.

Pia, amesema matukio ya Oktoba 29 mpaka 30 yaliacha majeraha kwa watoa huduma binafsi, “Oktoba 29 watu wameenda wameumia wakawatibu baadaye wakaanza kuulizwa kwanini waliwatibu bila PF3 ya polisi, sasa mgonjwa wa dharura ukimuacha mpaka urudi amepoteza maisha.”