Dar es Salaam. Jukwaa la Watendaji Wakuu Tanzania (CEOrt- Roundtable of Tanzania) limesaini Hati za Makubaliano (MoU) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya elimu, viwanda na biashara.
Lengo ni kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi, maarifa na uwezo unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na ushindani wa dunia ya kazi.
Aidha, makubaliano hayo yanalenga kuunganisha uzoefu wa vitendo wa sekta ya viwanda na programu za kitaaluma za vyuo hivyo, kujenga uwezo wa wanafunzi na wahadhiri, pamoja na kuweka mifumo endelevu ya kubadilishana maarifa na uzoefu kati ya viongozi wa biashara na taasisi za elimu ya juu.
Ushirikiano huo unatambua maendeleo ya Tanzania yanayohitaji wahitimu wenye uwezo wa kutumia nadharia walizojifunza darasani katika mazingira halisi ya kazi, wakisaidiwa na viongozi wa biashara wanaoelewa mwelekeo wa uchumi unaokua, changamoto zake na fursa zinazojitokeza.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo jana Alhamisi, Februari 5, 2026, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CEOrt, David Tarimo amesema CEOrt kwa kushirikiana na IAA na CBE imeanzisha mfumo wa kimkakati wa kitaifa unaolenga kuimarisha uhusiano kati ya sekta ya elimu na sekta ya viwanda na biashara, hususan katika maeneo ya utafiti, ushauri elekezi na maendeleo ya rasilimali watu.
Kupitia ushirikiano huo, CEOrt yenye kampuni wanachama zaidi ya 235 kutoka sekta binafsi itatumia uzoefu wake wa kibiashara kuchangia katika kuchambua changamoto za mazingira ya biashara na uchumi zinazoikabili nchi na kushiriki katika kubuni suluhisho la pamoja lenye matokeo chanya kwa maendeleo ya taifa.
Amesema ushirikiano huo pia utavijengea uwezo vyuo hivyo katika kufanya tafiti, sambamba na kuwapa wanafunzi wanaojifunza kwa vitendo fursa ya kukabiliana na changamoto halisi za soko la biashara la sasa.
“CEOrt kupitia kampuni wanachama wake ni miongoni mwa waajiri wakubwa katika sekta binafsi nchini, hivyo ushirikiano huu utatusaidia kwa pamoja kuandaa vijana waliopo vyuoni ili waendane na mahitaji halisi ya soko la ajira.”
Amesema makubaliano hayo yamejengwa juu ya dira ya pamoja ya kuoanisha elimu na mahitaji ya ulimwengu wa biashara, kuendeleza taaluma na kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi kwa kuunganisha vyumba vya madarasa na bodi za wakurugenzi zenye uzoefu wa kibiashara.
Tarimo amesema makubaliano hayo na vyuo hivyo yanaongozwa na malengo ya msingi yanayofanana, ikiwamo kuingiza uzoefu wa sekta ya biashara katika mitalaa ya vyuo, kujenga ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira kwa wanafunzi na wahadhiri, pamoja na kuimarisha mifumo rasmi ya kubadilishana maarifa kati ya viongozi wa biashara na taasisi za elimu ya juu.
Mfumo huo wa utafiti unaotokana na vitendo unalenga kuzalisha suluhisho zenye athari halisi kwa jamii na uchumi, huku ukiimarisha uwezo wa utafiti wa IAA na CBE, na kuwapa wanafunzi fursa ya kushiriki moja kwa moja katika utatuzi wa changamoto zinazoikabili sekta ya biashara na uongozi hapa nchini.
Aidha, unaanzisha mifumo rasmi ya ushiriki kupitia mafunzo ya ziada na mihadhara ya wazi kwa umma, itakayowakutanisha wahadhiri, wanafunzi na wataalamu wa sekta za biashara, uongozi na uchumi.
Katika mpango huo, wanachama wa CEOrt pamoja na wahitimu wa Mpango wa Mafunzo ya Uongozi kwa Wakurugenzi Wakuu (CEOrt Apprenticeship Programme – CAP) watashiriki kama wahadhiri wa ziada, wakileta uzoefu wa vitendo darasani.
Amesema makubaliano hayo pia yanalenga ujenzi wa uwezo wa muda mrefu kupitia programu za maendeleo ya uongozi, mafunzo ya uendelevu, kozi fupi na mafunzo ya vitendo.
Kwa upande wa Chuo cha IAA kimesema mpango wa Mafunzo ya Uendelevu kwa Mameneja wa CEOrt utakuwa sehemu ya mitalaa ya chuo hicho, huku pande zote zikitarajia kuendesha mafunzo ya viongozi waandamizi, programu za uongozi, ushauri elekezi na kambi za mafunzo ya uongozi.
Chuo cha CBE, ushirikiano huo utajumuisha kozi fupi, mafunzo yanayoongozwa na sekta ya biashara, pamoja na mafunzo kwa vitendo kupitia viambatanisho vya kazi ili kuhakikisha wahitimu wanahitimu wakiwa na ujuzi, uzoefu na mtazamo unaowawezesha kuchangia kikamilifu katika mageuzi ya kijamii na kiuchumi ya Tanzania katika dunia ya sasa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Profesa Eliamani Sedoyeka, amesema ushirikiano huo una mchango mkubwa katika kuzalisha viongozi na wataalamu wenye ushindani katika sekta ya biashara nchini.
Profesa Robert Mashenene, Makamu Mkuu wa Chuo cha CBE anayesimamia taaluma, Ushauri na Utafiti, amesema makubaliano hayo yatasaidia kupunguza pengo la uzoefu wa vitendo lililopo kwa kuwapa wanafunzi fursa za kujifunza moja kwa moja kutoka kwa vinara wa biashara.