Dar es Salaam/Mikoani. Baadhi ya wanafunzi nchini wameeleza adha wanazokumbana nazo wanapotumia usafiri wa umma, huku wakitaka kuwepo kwa sheria mahsusi itakayolazimisha na kusimamia usafiri kwa wanafunzi.
Februari 4, 2026, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa aliiagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kuwaadhibu madereva na makondakta wa daladala wanaowanyanyasa wanafunzi.
Hata hivyo, wanafunzi hao wamesema kwa kuwa nchi inaendeshwa kwa misingi ya kisheria, ni vyema hata usafiri wa wanafunzi ukaongozwa na sheria badala ya kuachwa kwenye miongozo inayotolewa na viongozi mara kwa mara.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi leo Ijumaa, Februari 6, 2026, wanafunzi kutoka Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Kilimanjaro wamesema kutokuwepo kwa sheria kunawafanya waendelee kubaguliwa na kunyanyaswa bila msaada wa kudumu.
Mather Komba, mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule moja ya sekondari jijini Dar es Salaam, amesema umefika wakati wa kuundwa kwa sheria itakayosimamia usafiri wa wanafunzi.
“Tunasikia viongozi wakisema kwa mujibu wa sheria, basi hata usafiri wetu uwe kwa mujibu wa sheria. Konda akikataa kutupakia awajibishwe kisheria,” amesema mwanafunzi huo.
Amesema tamko la Profesa Mbarawa, kuhusu kulinda haki za wanafunzi lilipaswa kusimamiwa na sheria.
“Bila sheria tutaendelea kuteseka, halafu tunalaumiwa eti tunapenda kukaa vituoni, wakati makondakta wanakataa kutupakia,” amelalamika.
Frida Mwakalebela, mwanafunzi wa shule ya sekondari jijini Mbeya, amesema usafiri mgumu ni chanzo cha wanafunzi wengi kuchelewa kufika shuleni na kuathiri mwenendo wao wa masomo.
Amesema hali hiyo pia huwaathiri kisaikolojia, kwa kuwa mara nyingi hudhalilishwa na kufokewa vituoni.
“Tunabaguliwa kwa sababu ya nauli ya Sh200 tunayolipa. Asubuhi unaweza kukaa kituoni daladala zinakupita, zikisimama zinawabeba watu wazima na sisi tunabaki na hakuna mzazi anayetutetea wote wanatuangalia tu hata tukitukanwa,” amesema Frida.
Amesema wakati mwingine hulazimika kulipa hadi Sh500 au kutembea kwa umbali mrefu kutokana na kunyimwa usafiri.
Mwanafunzi mwingine, Tukali Daniel amesema msaada mkubwa kwa wanafunzi hutolewa na madereva wa magari binafsi, huku daladala zikiwachukua wachache au kuwaacha kabisa.
“Wanaruhusu wawili tu wakati tupo wengi. Msaada wetu mkubwa ni watu wenye magari binafsi,” amesema.
Mwanafunzi mwingine aliyekataa kutajwa jina alisema shule yao ina usafiri maalumu wa wanafunzi, lakini gharama zake ni kubwa kwa wazazi wengi.
“Ada ya usafiri imepanda kutoka Sh26,000 ambayo tulikuwa tunalipa mwezi uliopita (Januari) hadi Sh36,000 mwezi huu wa pili. Mzazi akishindwa, unabaki kupambana na daladala au kutembea,” amesema.
Hali kama hiyo imeripotiwa pia katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro na Edward Mroso, mwanafunzi wa kidato cha tatu akisema uhaba wa daladala na gharama kubwa za bajaji zimeongeza mzigo kwa wazazi.
“Sasa tunalipa Sh500 hadi Sh700 kwenye bajaji,” amesema mwanafunzi huyo.
Sara Mongi alisema waendesha bajaji wengi huwakwepa wanafunzi kwa kuwa nauli yao ni ndogo.
Katika Mtaa wa Relini na Mabogini, wanafunzi wa shule za msingi Azimio, Juhudi na Mandela walisema hukumbwa na changamoto zaidi jioni.
Jijini Mwanza, mwanafunzi Salum Ally alikiri wakati mwingine wanafunzi wenyewe huchangia tatizo kwa kuchagua magari, lakini akasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa utaratibu wa kudumu wa usafiri wa wanafunzi.
Hata hivyo, Upendo Mushi, mwanafunzi wa Sekondari ya Pamba, amesema anahofia ndoto yake ya kufaulu kupotea kutokana na ugumu wa usafiri, akisema hutembea hadi kilomita 13 kwenda na kurudi shule kila siku hali inayomfanya akose hata muda wa kujisomea kutokana na uchovu.
Awali, Profesa Mbarawa alitoa agizo la kuchukuliwa hatua kali dhidi ya madereva na makondakta wanaowanyanyasa wanafunzi.
Agizo hilo lilitokana na barua ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza wa Shule ya Sekondari Jangwani, Dar es Salaam, akidai wanafunzi hubaguliwa na makondakta wa daladala kwa kuwa hawalipi nauli kamili.
Waziri huyo alisema Serikali imezielekeza Latra na Jeshi la Polisi kuimarisha usimamizi wa nauli, usalama na staha ya huduma, kuanzisha mipango ya mabasi na mabehewa maalumu ya wanafunzi, sambamba na kuweka namba za bure za kutoa taarifa za unyanyasaji.