Iringa. Wakati vijana wengi nchini wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira, kundi la vijana mkoani Iringa limegeuza soko la Masai (Masai Market) kuwa tegemeo la maisha kwa kuuza bidhaa za asili na za kitamaduni na bado soko hilo linaendelea kutegemea zaidi wanunuzi wa kigeni kutokana na mwitikio mdogo wa wateja wa ndani.
Soko hilo lililopo Manispaa ya Iringa limekuwa kimbilio la vijana wengi waliotumia ubunifu na rasilimali za kitamaduni kujipatia kipato ambapo huuza bidhaa mbalimbali zikiwemo shanga, mikufu, vikuku, mikoba ya ngozi, sanamu, vinyago, batiki na mapambo yanayotengenezwa kwa mikono.
Kwao, biashara hiyo si chanzo cha mapato pekee, bali pia ni njia ya kutunza na kuendeleza utamaduni wa Kitanzania unaozidi kusahaulika katika jamii ya kisasa.
Wakizungumza na Mwananchi leo Februari 5, 2026, baadhi ya wafanyabiashara wamesema Masai Market imewasaidia kujitegemea kiuchumi na kuwaepusha vijana wengi na vitendo viovu vinavyotokana na ukosefu wa ajira.
Soko hilo halionekani kama soko la kawaida bali kama makumbusho ya wazi yanayoonesha kazi za mikono zenye historia na maana.
Vinyago vinavyoonesha mashujaa, wanawake, wanyama wa savanna na barakoa za kijadi huvutia macho ya wapita njia.
Batiki zenye rangi za kuvutia huonekana kama nguo zinazobeba simulizi za tamaduni huku vikapu vilivyosokotwa kwa ustadi vikionyesha uvumilivu na juhudi za wasanii waliovitengeneza.
Paschal Silvester, mfanyabiashara aliyekulia katika soko hilo, amesema biashara hiyo ni maisha yake.
“Hapa hatuombi kazi, tunaitengeneza kwa mikono yetu,” amesema.
Silvester ameongeza kuwa miezi ya Julai hadi Oktoba huwa kipindi cha kilele cha mauzo kutokana na wingi wa watalii.
Neema Mwaisumo, mwanamke wa Kitanzania anayependa kuvaa shanga za asili, amesema mapambo hayo humpa hisia ya utambulisho.
“Ninapovaa hizi shanga nahisi kama mababu wamenibariki na utambulisho wao,” amesema.
Wauzaji wengi ni wanaume, hasa wanaojihusisha na uchongaji wa vinyago, kazi inayohitaji nguvu na uvumilivu.
Deo Mtasiwa, mchongaji wa vinyago, anasema: “Kazi hii inahitaji nguvu na kukaa muda mrefu. Wengi wetu tumeanza tangu ujana.”
Wanawake nao hawako nyuma, wakijihusisha na ushonaji wa batiki, utengenezaji wa shanga na usukaji wa vikapu.
Kwa wafanyabiashara hao, utamaduni si pambo la sherehe bali ni rasilimali inayoweza kuleta kipato na kuitangaza Tanzania na wanunuzi wanapochukua bidhaa hizo, hubeba historia na utambulisho wa nchi.
Hata hivyo, wafanyabiashara hao wanakiri kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa mitaji, misimu isiyotabirika ya watalii na idadi ndogo ya wanunuzi wa ndani.
Noin Amrasi, mfanyabiashara katika Masai Market, amesema utegemezi wa wateja wa nje ni changamoto kubwa.
“Wateja wa ndani ni wachache, na wengi huona bidhaa hizi ni za watalii tu,” anasema.
Mfanyabiashara mwingine, Monica Julius, amesema licha ya changamoto, bado anaendelea na biashara hiyo kwa kuwa ni tegemeo la familia yake.
“Tunahitaji wananchi wa ndani waone thamani ya bidhaa za asili kwa sababu zinawakilisha utamaduni wetu,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa Iringa wamesema sababu ya kutonunua mara kwa mara ni gharama wanazoziona kuwa juu na mtazamo kuwa bidhaa hizo si za matumizi ya kila siku.
Mkazi wa Iringa, Rehema Mgongolwa, anasema: “Bado kuna mtazamo kuwa bidhaa za asili si sehemu ya matumizi ya kawaida.”
Shanga, vinyago na mimufu, yenye mvuto wa asili na utamaduni zikiwa tayari kwa wateja katika eneo la Masai Market, mkoani Iringa. Picha na Christina Thobias
Hata hivyo, wateja wa ndani wanaonunua bidhaa hizo wamesema huvutiwa na ubora, uimara na upekee wa kazi za mikono.
Kwa upande wa wageni, Masai Market imeendelea kuwa kivutio kikubwa. Yorvan Akas, mtalii kutoka Italia, anasema bidhaa za asili hubeba hadithi na maana ya kipekee.
“Katika nchi nyingi za nje, bidhaa kama hizi huuzwa kwa bei kubwa zaidi kuliko hapa,” anasema.
Mdau wa masuala ya utamaduni mkoani Iringa, John Msigwa, anasema Masai Market ina mchango mkubwa katika kukuza utalii wa kitamaduni na kutoa ajira kwa vijana.
Amesema biashara hiyo huchangia kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na mapato ya taifa kupitia sekta ya utalii.